Zitto kabwe aifikiria ' ukawa' kuing'oa CCM madarakani - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 30 August 2017

Zitto kabwe aifikiria ' ukawa' kuing'oa CCM madarakani

 Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameeleza umuhimu wa vyama vya upinzani kuungana akisema ndio mkakati pekee utakaoing’oa CCM madarakani.

Zitto alisema hayo wiki iliyopita katika mahojiano maalumu na kulunzifikra blog  kuhusu mambo mbalimbali ya kisiasa yanayoendelea nchini na ndani ya ACT -Wazalendo.

ACT-Wazalendo haikuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, ikiviachia vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi za urais, ubunge na udiwani.

Lakini katika mahojiano na kulunzifikra blog, Zitto alionekana kutambua umuhimu wa umoja katika kupambana na chama hicho kikongwe nchini ambacho kimeongoza nchi kwa zaidi ya miaka 50, kikianzia na jina la Tanu kwa Bara na ASP kwa visiwani.

“Kwa mazingira ya siasa yaliyopo nchini, ushirikiano miongoni mwa vyama vya upinzani kukabiliana na CCM ni jambo lisilokwepeka,” alisema Zitto, mwanasiasa wa kizazi kipya ambaye hajawahi kuwa CCM kama ilivyo kwa wanasiasa wengi wa upinzani.

“ACT Wazalendo tunalitambua hilo ndio maana tunafanya juhudi kubwa kujenga chama chenye nguvu kitakacholeta chachu ya ushindi kwa kushirikiana na vyama vingine.

“Hakuna chama cha siasa chenye nguvu kinachokubali kuungana na kingine kilicho dhaifu. Ndio maana tunajenga chama kuongeza nguvu na ushawishi kisiasa ili tukiungana kusiwepo chama kinachonyonya nguvu ya kingine.”

Kauli ya Zitto ni tofauti na msimamo ambao amekuwa akiuonyesha tangu aondolewe Chadema mapema mwaka 2015 na alitumia kampeni za chama hicho kuponda Ukawa. “Kama unataka siasa za mbwembwe nenda CCM, kama unataka siasa za ulaghai nenda Ukawa, na kama unataka siasa za msingi siasa za issues ni ACT Wazalendo,” alisema Zitto Agosti 28, 2015 wakati harakati za uchaguzi zikiwa zimepamba moto.

hivyo, katika matukio ya hivi karibuni, Zitto amekuwa akishirikiana na viongozi wa vyama vingine, hasa Chadema ambayo ilikuwa na mgogoro naye kwa muda mrefu.

Zitto na Chadema walionyesha dalili za kuanza kuondoa tofauti zao wakati wakipinga uamuzi wa Serikali kufuta matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za Bunge.

Oktoba mwaka huo, Zitto aliisifu Ukawa kwa jinsi ilivyopambana na CCM katika Uchaguzi Mkuu uliopita, lakini akasema ACT-Wazalendo haitajiunga na umoja huo kutokana na miiko iliyojiwekea katika Azimio la Tabora.

Katika uchaguzi huo, Ukawa ilimsimamisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye aliweka rekodi ya upinzani kwa kupata kura milioni 6.07 ambazo ni takriban mara mbili ya kura zote ambazo wapinzani wamekuwa wakipata tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.

Akijibu swali la kituo kimoja cha televisheni kama atagombea urais mwaka 2020, Zitto pia alidokeza umuhimu wa ushirikiano.

“Kwa mazingira yaliyopo sasa, suala la kugombea au kutogombea urais lisiwe maamuzi ya mtu mmoja. Kwa sasa tunahitaji kwenda kwenye uchaguzi wa 2020 vyama vya upinzani tukiwa united front.Tukiwa tunashirikiana, si kuungana kwa sababu vyama vina itikadi tofauti,” alisema Zitto akijibu swali hilo mapema mwaka huu.

Katika kipindi hicho cha kuanzia mwaka 2015, viongozi wa vyama vingine, hasa Chadema walikuwa wakimrushia maneno Zitto na chama chake, wakisema hawatakubali ajiunge Ukawa.

Kuhusu mpango huo wa kuifanya ACT Wazalendo kuwa kubwa, alisema wameandaa mikakati kadhaa ya kukabiliana na changamoto, hasa za kifedha.

“Tumejiwekea mkakati wa kuhimiza kila mwanachama kuchangia Sh1,000 kila wiki, au Sh4, 000 kwa mwezi kugharamia uenezi na ujenzi wa chama; tumegawa kadi zaidi ya 400,000 na iwapo wanachama 100,000 pekee watachanga, tunatarajia kukusanya Sh400 milioni kwa mwezi,” alisema Zitto.

Alisema fedha hizo zitasaidia mikakati ya kujenga chama kuwa cha kimkakati.

Kuhusu kukamatwa mara kwa mara kwa wanasiasa wa upinzani, Zitto alisema:“Naumizwa sana kuona viongozi, hasa wa upinzani wakikamatwa kwa kutekeleza wajibu na majukumu yao ya kikatiba ya kuisimamia, kuikosoa na kuishauri Serikali; kibaya zaidi amri za kukamata viongozi wakiwemo wabunge zinatolewa hadi na wakuu wa wilaya.”

1 comment:

Popular