Mbeya chunya: Majambazi wateka basi, wapora fedha kisha kuwachapa viboko abiria - KULUNZI FIKRA

Wednesday 30 August 2017

Mbeya chunya: Majambazi wateka basi, wapora fedha kisha kuwachapa viboko abiria

Abiria waliokuwa wakisafiri kwa basi la Kampuni ya Safina, wametekwa na majambazi eneo la Mlima Rogea uliopo wilayani Chunya, Mbeya na kuporwa fedha, simu za mkononi na kisha kuwatandika viboko.

Tukio hilo la aina yake lilitokea jana katika mlima huo, wakati basi hilo likiwa likitokea Lupatingatinga kuelekea Chunya Mjini.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Chunya, Ramadhani Shumbi, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mamba, wilayani humo, akizungumza na waandishi wa habari alisema alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa wakisafiri na basi hilo.

Shumbi alisema saa 12. 45 asubuhi, walipofika eneo hilo la Mlima Rogea, walikuta gogo kubwa likiwa limewekwa barabarani, huku watu sita waliokuwa na bunduki iliyokatwa mtutu, mapanga, shoka na fimbo walitoka vichakani na kupiga hewani risasi tatu.

"Baada ya hapo wakawa wanapiga risasi kwenye vioo vya basi, huku wakitulazimisha abiria kushuka chini, ilituchukua kama dakika 10 hivi tukiwa tumeweka mgomo wa kushuka garini, lakini baadaye baadhi ya abiria wenzetu wenye roho nyepesi, walianza kuruka kupitia madirishani", alisema Shumbi.

Aliongeza kuwa baadaye abiria wote waliamua kushuka, kisha majambazi hayo yaliwapekua na kuanza kuchukua fedha, simu na kwamba hata yeye ni miongoni mwa abiria walioporwa fedha na simu.

"Muda huo abiria wengine walikuwa wanapigwa viboko".

Makamu mwenyekiti huyo alisema ni vizuri sasa Jeshi la Polisi, liweke utaratibu mpya wa kuhakikisha mabasi yanaanza kuondoka Lupatingatinga, kuanzia saa 1.00 asubuhi badala ya saa 11. 00 alfajiri hadi saa 12.00 asubuhi kwa ajili ya usalama wa abiria na mali zao.

Kwa mujibu wa Shumbi, matukio kama hayo ya utekaji mabasi na abiria kuporwa mali zao zikiwemo fedha, yalikuwa yanatokea eneo hilo miaka minane hadi tisa iliyopita, na baada ya ya hapo yalikoma na hakuna tukio lolote lililowahi kutokea na hilo ndiyo la kwanza kwa hivi karibuni.

Aliongeza baada ya tukio hilo abiria walikwenda kituo cha polisi Makongolosi, wakatoa taarifa ambapo polisi mara moja, waliondoka kuelekea eneo la tukio, kwa kupelekwa na mmoja wa abiria.

"Hakuna abiria aliyedhurika ila abiria wanane walipata majeraha madogo madogo", alisema.

Naye Diwani wa Viti Maalumu, Fortunata Mpalamba, alisema saa 12. 45 asubuhi walikuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Kitila, nao wakitokea Lupatingatinga kuelekea Chunya Mjini, ambapo walipokaribia mlima Rogea, walikuta basi la kampuni ya Safina likiwa limetekwa huku abiria wakiwa wamelazwa chini.

Fortulata alisema wakati huo majambazi walikuwa wakiwapekua abiria, wakichukua fedha na simu za mkononi huku basi lao likiwa umbali wa mita si zaidi ya 15 tu kulifikia basi hilo.

"Baada ya dereva kuona hivyo, aliamua kufanya kitendo cha ujasiri ili kuokoa abiria. Alianza kurudisha basi nyuma kwa kasi kama umbali wa nusu kilomita, ndipo akapata sehemu ya kugeuza na kurudi tulikotoka, ambapo aliendesha kwa mwendo wa kasi", alisema.

Juhudi za kumpata Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga, ili kupata taarifa zaidi juu tukio hilo, zilishindikana kufuatia simu yake ya mkononi, kupigwa lakini ikawa inaita tu bila kupokelewa.

No comments:

Post a Comment

Popular