Mwanza: Jeshi la polisi lampa ulinzi mjane aliyemwaga chozi mbele ya Rais Magufuli. - KULUNZI FIKRA

Friday 3 November 2017

Mwanza: Jeshi la polisi lampa ulinzi mjane aliyemwaga chozi mbele ya Rais Magufuli.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetekeleza agizo la Rais John Magufuli kwa kumpatia ulinzi Ana-Joyce Francis, mjane mwenye watoto sita, aliyeangua kilio mbele ya Rais John Magufuli akilalamikia kuporwa ardhi.

Mjane huyo alimtajana mwanasheria Alex Bantulaki kwamba ndiye aliyemdhulumu ardhi yake huku akiachwa anataabika na familia yake asijue lakufanya.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Faustine Shilogile ameiambia Kulunzifikra blog ofisini kwake leo Novemba 3, kwamba agizo hilo limetekelezwa, ingawa hakua tayari kufafanua aina ya ulinzi aliopewa mjane huyo, mkazi wa eneo la Isamilo, jijini Mwanza.

“Kwa sababu za kiusalama, siwezi kuweka wazi ni aina gani ya ulinzi tumempatia; isitoshe tu kusema kuwa agizo la Rais limetekelezwa,” amesema Shilogile

Oktoba 30, mjane huyo, akiwa na lundo la nyaraka alizozifungia kwenye kanga yake, alijipenyeza na kufanikiwa kufikia macho ya Rais Magufuli wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Nyakato jijini Mwanza.

Baada ya kuitwa mbele na Rais Magufuli, mjane huyo, huku akimwaga machozi, amesema kuna njama za kumpora kiwanja chake alichokinunua tangu mwaka 2005.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Rais akauagiza uongozi wa Serikali Mkoa, jiji la Mwanza na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushughulikia suala hilo kwa kuitisha na kupitia nyaraka za pande zote mbili na kumpatia taarifa.

Licha ya kumkabidhi mjane huyo fedha taslimu ambayo kiasi chake hakikujulikana, Rais Magufuli pia aliagiza apewe ulinzi ili asibughudhiwe na yeyote wakati suala lake likishughulikiwa.

No comments:

Post a Comment

Popular