Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ilivyopita kwa Shida. - KULUNZI FIKRA

Wednesday 9 May 2018

Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ilivyopita kwa Shida.

 
Ulikuwa ni mvutano wa hoja usio na mwisho. Kama si Kanuni ya 53(8) ya Bunge, wabunge wa kambi ya upinzani wangezidi kuvutana na kiti cha Spika pale walipokaa kama kamati ya mipango na matumizi kupitia Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Hoja iliyozuia mvutano na sintofahamu ni kuhusu masuala ya utekaji na watu kupotea ambayo kwa siku za karibuni yamekuwa yanatajwa nchini.

Wakati wabunge wa upinzani wakiendelea kuyajadili na kuitaka Serikali kuyapa uzito mkubwa, Serikali na baadaye kiti cha spika wanasema masuala hayo yamekwishajadiliwa na kutolewa uamuzi na chombo hivyo, hivyo hayastahili kuibuliwa kwa mujibu wa kanuni hiyo.

Kanuni hiyo ya 53 (8) inasema kuwa mbunge yeyote hataruhusiwa kufufua jambo lolote ambalo Bunge lilishakwisha kuliamulia ama katika mkutano uliopo au ule uliotangulia.

Kutoelewana baina ya pande mbili kulisababisha wabunge wa kambi ya upinzani kususia kikao na kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge kabla mjadala wa bajeti hiyo kuhitimishwa.

Hii ilikuwa baada ya Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini (Chadema), Mhe Godbless Lema kuzuiwa na Mwenyekiti wa Bunge,Mhe  Mussa Zungu kuendelea na hoja yake ya kutaka kushika shilingi katika mshahara wa waziri kutokana na masuala ya utekaji na mauaji.

Uamuzi wa kiti ulisimamia kwamba hoja hiyo ilikuwa imetolewa awali na kujibiwa na Serikali kisha kuamuliwa bungeni katika kikao hicho, kama lilivyoibuliwa na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki (CCM), Mhe Mashimba Ndaki.

Kauli ya Mhe Ndaki

Katika hoja yake, Mhe  Ndaki anasema Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt Mwigulu Nchemba amefafanua kuhusu hoja ya watu kutekwa, kupotea, kuuawa na wakati mwingine kutishiwa.

“Mhe Mwenyekiti, jambo hili limekuwa likijirudiarudia sana na jambo la namna hii linapojirudia rudia na ni jambo baya linaloitia doa nchi yetu, si jambo unaloweza kulitolea maelezo tu halafu likaishia hapa", alisema Mhe Ndaki.

"Nadhani ni jambo ambalo linahitaji mkakati wa kutosha kuhakikisha kuwa haliendelei kusemwa ama kutokea na kuitia doa nchi yetu.”alisema Mhe Ndaki.

Mbunge huyo anaomba Serikali imweleze ni mkakati gani wa kihalisia juu ya mambo hayo ili yasiendelee na kulitia doa taifa letu.

Akijibu suala hilo, Dkt Mwigulu Nchemba anasema utekaji ni uhalifu kama uhalifu mwingine na kwamba si vizuri kutaja matukio hayo kila mara kwa sababu yameacha makovu katika familia.

“Ilitokea watoto wadogo ambao hawana siasa wala madeni tukiona wakitekwa na wengine na hata kupoteza maisha yao lakini ni jambo ambalo Serikali limejizatiti kukabiliana nalo kama uhalifu mwingine ambao tunakabiliana nao,” anasema  Dkt Mwigulu Nchemba.

Anayataja matukio ya mauaji ya maalbino na wanawake katika kanda ya ziwa yaliyowahi kutokea nchini na kuongeza kwamba wao kama Serikali wanaendelea kujizatiti katika intelijensia, doria kupambana nayo kama matukio mengine ya uhalifu.

Dkt Mwigulu Nchemba anasema Serikali haina makubaliano na wahalifu kuwaambia wasifanye uhalifu ila ina njia ya kukabiliana nao kuhakikisha kuwa wanaukomesha.

Kauli ya Mhe Lema

Na alipopewa nafasi Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema anaanza kwa kutangaza kuondoa shilingi katika mshahara wa waziri endapo asingekubaliana na majibu yake.

“Nimesikiliza majibu ya waziri alipokuwa anatolea ufafanuzi jambo la watu kupotea. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ieleweke hakuna mbunge anayepigania hadhi ya binadamu na uhai, mwenye nia ya kuchafua taswira ya nchi ila wanaotaka kuzuia mijadala ya namna hii ndiyo wanaotaka kuchafua taswira ya nchi. Mtu mmoja thamani yake ni kubwa sana,” anasema Mhe Lema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu alimkatisha Lema na kumweleza kuwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge, jambo ambalo limeshafanyiwa maamuzi na lililopitishwa na Bunge halirudiwi tena.

Kufuatia uamuzi huo, baadhi ya wabunge wa upinzani walianza kulalamika bila ruksa wakionyesha kutokubaliana na majibu ya kiti, lakini Zungu aliwajibu kuwa jambo ambalo Lema anataka kulizungumzia lilishatolewa uamuzi.

“Waheshimiwa, nimeshaisikia hoja yake na amemnukuu waziri (zinasikika kelele kutoka kwa wabunge wa upinzani) na waziri ametoa majibu. Haya, mheshimiwa Lema,” anamruhusu kuendelea na hoja yake.

Akiendelea, Lema anasema analo jina na namba ya simu ambayo inasemekana ni ya mtu aliyemuua Daniel (John, katibu wa Chadema Kata ya Hananasifu).

Aliongeza, “Inspekta Jenerali wa Polisi katika gazeti (sio Mwananchi) la Novemba 30 mwaka jana kwamba Kibiti, Pwani kuna watoto 1,300 wamepotea”.

Wakati akiendelea, Dk Nchemba anatoa taarifa kuwa Mkuu wa Polisi nchini hakusema kuwa watoto wamepotea, bali kwamba alichosema ni kuwa hawako shuleni.

“Pia kwenye shule, mheshimiwa mwenyekiti, Tabora hata na Iramba jambo hilo lipo. Na sisi kama Serikali tulisema tuhamasishe ufuatiliaji na ndio maana unaona wakuu wanafuatilia watoto ambao hawako shuleni,” anasema.

Anasema kama Serikali walikuwa wanadhani kama watoto hawako shuleni inawezekana wamekwenda kufanya mafunzo na kusisitiza kuwa IGP hakumaanisha kuwa watoto hao wamepotea, bali alimaanisha hawako shuleni.

Baada ya ufafanuzi huo, Zungu hakumruhusu tena Lema kuendelea bali alimweleza kuwa kiti chake kimejiridhisha kuwa hoja hiyo imeshazungumzwa na kujibiwa.

Zaidi ya hayo, Zungu anamtaka Lema kuwasilisha serikalini ushahidi alionao kuhusu kifo cha Daniel ili uweze kufanyiwa kazi na kwamba kwa mujibu wa sheria kuendelea kukaa na ushahidi huo, anahusishwa na uhalifu huo.

“Kwa kuwa jina unalo na haujakwenda kukabidhi katika vyombo vya ulinzi unakuja katika Bunge. Bado na kushauri hoja hiyo imeshajadiliwa na waziri alishajibu. Nakupongeza na nakushauri kabla ya saa 2:00 leo mkabidhi jina hilo waziri waanze kulifanyia kazi kisheria,” anasema Zungu.

Lema ang’ang’ania hoja

Hata hivyo, Lema anasimama na kusema kuwa hajamaliza hoja yake na kuhoji, “Unaliendeshaje Bunge?”

Wakati hayo yanaendelea Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe alianza kutoka katika ukumbi huo kwa kutumia mlango mkubwa huku akizungumza kwa sauti, “amezungumza (Lema) ndani ya Bunge unaanza kumtisha...”

Hali hiyo iliharibu utulivu kwani wakati Zungu akiwataka kutoka kama wameamua kufanya hivyo, Lema alikuwa akilalamikia kiti kinavyoendesha Bunge.

“Naona mmeshikwa pabaya leo,” anasema Zungu akiwaambia wabunge hao wa upinzani, lakini nao wanajibu, “umeshikwa pabaya mwenyewe”.

Wakati wabunge hao wanatoka wabunge wa CCM na wale wa chama cha CUF wanaomuunga mkono Mwenyekiti wa Taifa wa Profesa Ibrahim Lipumba walipiga makofi na kubaki bungeni.

Baada ya hapo Zungu alilihoji bunge na kifungu hicho kikapitishwa kwa kura za sauti.

Nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge wa upinzani wanadai wamefikia uamuzi wa kutoka kwa sababu Zungu anaendesha chombo hicho bila kufuata utaratibu na kuwanyima nafasi ya kujadili masuala muhimu yanayohusu maisha ya wananchi.

Muda mfupi baada ya Bunge kupitisha bajeti hiyo, Zungu anasema masuala ya uvamizi na uhalifu yatawaathiri Watanzania wote na kwamba vyombo vya ulinzi vinahitaji msaada wa watu wote.

“Tushirikiane kuvisaidia vyombo hivi na wao waweze kufanya kazi zao vizuri,” anasema.

No comments:

Post a Comment

Popular