Mgogoro wa chama cha CUF wazidi kuwaathiri wabunge wa chama hicho. - KULUNZI FIKRA

Friday 18 May 2018

Mgogoro wa chama cha CUF wazidi kuwaathiri wabunge wa chama hicho.

Mbunge wa Jimbo la Temeke (CUF), Mhe  Abdallah Mtolea amefunguka na kuweka wazi kuwa mgogoro uliopo ndani ya Chama chake umekuwa ukiathiri utendaji wa viongozi (Wabunge) waliopatikana kwa chama hicho kwa namna mbalimbali ikiwepo namna ya utendaji.

Akifanya mahojiano na kulunzifikra media, Mhe Mtolea amesema kwamba mgogoro wa chama chake wakati mwingine unakuwa unawanyima fursa wananchi kuweza kufahamu viongozi wao wanafanya kazi gani kwani mtandao waliokuwa wanautumia kufikisha habari unakuwa umekatika.

"Mgogoro wa chama unatuathiri kwa namna mbalimbali. Kwa mfano sisi wabunge mtandao wa chama unakuwa umekatika. Wananchi wanakuwa wamekatika/wamegawanyika. Mbunge unakuwa umefanya mambo mengi lakini wa kuyasemea kwa wanachi anakuwa hayupo  kwa kuwa ule mtandao tu ule mtandao tuliokuwa tunautumia unakuwa umekatika. Kwa sasa mnasimama nyie wenyewe tofauti na ilivyokuwa awali"amesema Mhe  Mtolea.

Aidha, Mhe Mtolea  ameongeza kwamba "Kuwepo kwa mgogoro kuwafanya mnakuwa hamfanyi kazi za chama zaidi ya kushughulikia migogoro inayoendelea".

Mbali na hayo Mhe Mtolea  amesema mgawanyiko ndani ya chama umepelekea mzigo mkubwa wa ujenzi wa chama umehamia kwa Wabunge ingawa pamoja na michango ambayo watakuwa wanaichangia bado maendeleo ya chama hayataweza kwenda kwa kasi kama jinsi ambavyo wangekuwa wanapata ruzuku.

Mgogoro wa Chama cha Wananchi CUF unasadikika kuanza pale ambapo Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba alipotaka kurejea kwenye nafasi yake ikiwa ni muda baada ya kujiuzulu kipindi cha Uchaguzi mkuu 2015 kitendo ambacho kilisababisha wanachama kugawanyika huku upande mmoja ukimuunga mkono Katibu wa Chama Maalim Seif Sharif Hamad na wengine wakimuunga mkono Lipumba.

No comments:

Post a Comment

Popular