Kortini akidai kachero wa usalama wa Taifa anamfuatilia Tundu Lissu hospitali Nairobi - KULUNZI FIKRA

Friday 29 September 2017

Kortini akidai kachero wa usalama wa Taifa anamfuatilia Tundu Lissu hospitali Nairobi

 Mwakihaba (40) amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akituhumiwa kuchapisha maneno ya uongo kuhusu kachero wa usalama wa Taifa kumchunguza Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayepatiwa matibabu Nairobi nchini Kenya.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, mtuhumiwa alikanusha shtaka hilo. Alipewa dhamana kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa uhakika. Kwa mujibu wa mashtaka, kila mdhamini akitakiwa kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni tano. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 12, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Uchunguzi dhidi ya shtaka hilo haujakamilika. Mshitakiwa huyo anadaiwa alitenda kosa hilo Septemba 11, mwaka huu Dar es Salaam. Kwa mujibu wa mashtaka kupitia mfumo wa kompyuta, mshtakiwa anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo wakati akijua kuwa taarifa hizo ni za uongo kwa lengo la kupotosha umma.

Ilidaiwa maneno yaliyoandikwa ni pamoja na “Huyo ni kachero wa Usalama wa Taifa anatambulika kwa jina la Jose, ameonekana Nairobi karibu na hospitali aliolazwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, mwacheni mwenzenu.”

Tundu Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari lake wakati akielekea nyumbani eneo la Area D mkoani Dodoma, Septemba 7, mwaka huu na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

No comments:

Post a Comment

Popular