Kesi ya Viongozi wa Chadema yakwama Kwenda Mahakama Kuu. - KULUNZI FIKRA

Wednesday 16 May 2018

Kesi ya Viongozi wa Chadema yakwama Kwenda Mahakama Kuu.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya  Mhe Freeman Mbowe na wenzake wanane ya kutaka kesi dhidi yao ipelekwe Mahakama Kuu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri aliyeipanga kesi hiyo kusikilizwa leo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya shauri linalowakabili.

Wakati uamuzi ukisomwa na hakimu Mashauri, waliokuwapo mahakamani pamoja na Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema walikuwa ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu katibu mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Salum Mwalimu; na wa Bara ambaye pia ni mbunge wa Kibamba, Mhe John Mnyika.

Wengine ni mbunge wa Tarime Mjini, Mhe  Esther Matiko; katibu mkuu wa Chadema, Dkt Vincent Mashinji na mbunge wa Tarime Vijijini,  Mhe John Heche.

Washtakiwa wengine, mbunge wa  Jimbo la Kawe, Mhe Halima Mdee na Mbunge wa  Jimbo la Bunda,Mhe  Ester Bulaya hawakuwapo mahakamani ikielezwa na wakili wao, Peter Kibatala kuwa walikuwa safarini kutoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam lakini lao gari liliharibika.

Washtakiwa wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 12 katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria na kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali au maandamano yaliyosababisha kifo cha Akwilina Akwilini, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Kibatala aliiomba mahakama kulipanga shauri hilo Juni 8 au 15 ili kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali akisema mawakili watakuwa katika kesi Mahakama Kuu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliomba washtakiwa wasomewe maelezo hayo leo akidai hoja iliyowasilishwa na Kibatala kuwa wana kesi Mahakama Kuu ni ya maneno matupu.

Alisema hoja hiyo ingeambatanishwa na wito wa mahakama au orodha ya kesi zilizopangwa kusikilizwa.

Alidai upande wa utetezi una mawakili zaidi ya wawili na kwamba, kutokana na mazingira hayo waliopo wanaweza kuendelea na usikilizwaji leo asubuhi au mchana.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hadi leo saa nane mchana washtakiwa watakaposomewa maelezo hayo.

Awali, wakili mwingine wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliiomba mahakama kutupilia mbali hoja zilizotolewa na mawakili wa utetezi, Kibatala na Jeremiah Mtobesya akidai zitasababisha ucheleweshaji wa shauri hilo pasipo kuwa na sababu za msingi.

Nchimbi alidai hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi za kutaka kesi ipelekwe Mahakama Kuu hazina msingi wa kisheria na zilikuwa na lengo la kuipotosha mahakama.

Alidai katika mazingira ya mwenendo wa kesi hiyo tangu ilipoanza hakuna swali lolote la msingi lililoibuliwa na upande wa utetezi ambalo linajikita katika uvunjifu au ukiukwaji wa haki ya kikatiba. “Nasema hivyo kwa sababu ukiangalia msingi wa hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi zimejikita katika mashtaka yanayowakabili washtakiwa” alidai.

Alibainisha kuwa, washtakiwa wamesomewa mashtaka zaidi ya mara moja au mbili, waliyasikia mashtaka na wakayaelewa ndiyo maana wakaenda mbele wakayakanusha.

“Kama kweli washtakiwa waliona mashtaka haya si halali, hati ya mashtaka ilitolewa mapema hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi zingewasilishwa kabla washtakiwa hao hawajajibu kuwa wanakana shtaka,” alidai.

Nchimbi alidai ombi la utetezi halina msingi na iwapo mahakama itaona lina msingi ijiridhishe kama kuna swali la msingi linalohusu uvunjifu wa haki ya kikatiba.

Alidai hoja kuwa washtakiwa wamefunguliwa kesi ya jinai wakati walikuwa katika mkutano halali wa kampeni ya uchaguzi mdogo na kwamba kuwafungulia mashtaka hayo ni uvunjifu wa haki ya kikatiba, alisisitiza kuwa ni rai ya upande wa mashtaka kwamba yote yaliyoongelewa na upande wa utetezi hayawezi kuitwa ni maswali ya kikatiba ambayo yangeilazimu mahakama kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu.

Wakili huyo alidai mahakama za juu zimeeleza bayana kuwa suala la uvunjifu wa haki ya msingi ya kikatiba mahakama inatakiwa kuangalia sheria.

Kuhusu hoja za upande wa utetezi kuomba washtakiwa kupitia mawakili wao wapewe vielelezo vyote kuhusu kesi hiyo, Nchimbi alidai haitekelezeki na wala upande wa mashtaka haulazimishwi kufanya hivyo.

Aliiomba mahakama itupilie mbali hoja zote zilizowasilishwa mahakamani na upande wa utetezi.

Wakili Kibatala alidai mchakato wa kijinai ni mchakato mtakatifu ambao haukukusudiwa kuwashtaki watu ambao wanatekeleza majukumu yao kikatiba.

Kibatala alidai wanataka kwenda Mahakama Kuu ili kupata tafsiri ya je ni kweli mtu akiwa anatekeleza majukumu yake ya kikatiba ashtakiwe kijinai.

Aliiomba mahakama ikatae ombi lililowasilishwa na Nchimbi kuwa ayaone maombi ya upande wa utetezi hayana msingi kisheria.

No comments:

Post a Comment

Popular