Mapacha wa mimba moja wanaweza kutofautiana baba. - KULUNZI FIKRA

Sunday 25 March 2018

Mapacha wa mimba moja wanaweza kutofautiana baba.

Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba cha Muhimbili (MUHAS),jijini Dar es Salaam Dkt  Peter Wangwe, amesema upo uwezekano wa mwanamke kupata mimba ya watoto pacha toka kwa baba tofauti huku wakipishana muda.

Dkt Wangwe ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Akinamama na Uzazi MUHAS, amesema katika mazungumzo na  kulunzifikra blog ofisini kwake mwishoni mwa wiki kuwa, mwanamke anaweza kupata mimba ya mapacha kutoka kwa baba wawili tofauti ikiwa atakutana kimwili na wanaume wawili katika kipindi cha siku chache wakati ambapo mayai yake yamekomaa.

“Kuna uwezekano wa mwanamke kupata mimba ya pacha wa aina moja kati ya mbili yaani, pacha wanaofanana maarufu kama ‘identical twins’ na mapacha wasiofanana maarufu kama ‘fraternal twins’,” amesema Dkt Wangwe.

“Pacha wanaofanana lazima wawe wa baba mmoja hata kama mama amekutana na wanaume tofauti au niseme, mimba inakuwa ya mara moja hata kama amekutana na baba kwa nyakati tofauti katika kipindi cha urutubishaji kwa sababu chanzo ni yai moja ambalo hutengana baada ya kurutubishwa.”amesema Dkt Wangwe.

Pia Dkt Wangwe amesema pacha hao hufanana kila kitu tangu sura, jinsia, kundi la damu na wao hata kupeana viungo inapohitajika kitabibu, ni rahisi. Kuhusu pacha wa baba tofauti, Dk Wangwe alisema, inawezekana mwanamke kupata mimba ya watoto pacha toka kwa wanaume tofauti au kwa mwanaume mmoja, lakini kwa nyakati au siku tofauti katika kipindi kimoja.

Mtaalamu huyo alisema katika kipindi cha upevushaji mama akikutana na mwanaume kwa vipindi tofauti mathalani leo na kesho, anaweza kupata mimba za watoto wasiofanana kupitia mchakato wa mayai kutungwa mengi kwa wakati mmoja hali inayoitwa kitaalamu ‘superfecundation.’

No comments:

Post a Comment

Popular