Ombi la mwanafunzi wa Mkwawa kwa Rais Magufuli limewaingiza Watu Matatani. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 3 May 2018

Ombi la mwanafunzi wa Mkwawa kwa Rais Magufuli limewaingiza Watu Matatani.

Ombi la ujenzi wa mabweni lililotolewa na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (Muce) limemfanya Rais John Magufuli kuviagiza vyombo vya dola kuwachukulia hatua waliohusika na ujenzi wa jengo la ukumbi chuoni hapo.

Mbali ya hilo, wanafunzi hao waliiomba Serikali kubadilisha sheria ya mikopo ili itolewe kwa watu wote kwa uwiano na chuo kiendeshe kozi ya ujasiriamali.

Maombi hayo yalitolewa Jana baada ya wanafunzi kupewa fursa ya kuuliza maswali wakati Rais Magufuli alipofika chuoni hapo akiwa ziarani mkoani Iringa. Mkutano huo ulirushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha TBC 1.

Ombi kuhusu mabweni lilitolewa na Samson Philipo anayesoma mwaka wa tatu chuoni hapo katika kitivo cha Sayansi.

Mwanafunzi huyo alisema kutokana na changamoto ya mabweni, wanaishi mbali na chuo.

Akijibu ombi hilo, Rais Magufuli alisema alikataa kuweka jiwe la msingi katika ukumbi wa jengo lililopo chuoni hapo kwa kuwa lilijengwa kifisadi kwa Sh8 bilioni.

“Mlinipangia niweke jiwe la msingi katika lile jengo nikasema siwezi kuwa part of this problem (sehemu ya tatizo hili), lazima watu washughulikiwe na wizara ya elimu ifuatilie vizuri huu mradi. Hivi umeona mradi kama huu wa kitapeli, halafu leo (jana) mnaniomba mabweni. Nitatoaje mabweni wakati hili hamjatimiza, siwezi lazima nione kwanza matokeo ya fedha hizi za Serikali.

“Naviomba vyombo vya dola vikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na polisi kufuatilia, mkishindwa nitafuatilia mwenyewe", alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema wanafunzi wa Mkwawa wanateseka, hawana mahali pa kukaa kwa sababu ya uzembe wa watu waliopewa dhamana kuongoza chuo hicho siku za nyuma akiagiza aliyewahi kuwa mkuu wa chuo hicho, Profesa Philemon Mushi ahojiwe.

Rais Magufuli alitaka kuchukuliwa hatua kwa wahusika waliokuwa wakilipa fedha kwa mkandarasi, ambaye pia ameagiza atafutwe.

“Kwa mujibu wa sheria ya namba 17 ya mwaka 1997 na mabadiliko yake, inaeleza kuwa mkandarasi yeyote anaweza kufungwa miaka mitano na kurudisha fedha. Ifike mahali tuone uchungu wa fedha,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema Mkoa wa Iringa ni wa pili kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na huenda vijana chuoni hapo wakapata majaribu ya kutafuta fedha kwa ajili kulipia mabweni.

Kuhusu mikopo, swali lililoulizwa na John Fred, Rais alisema utoaji wa mikopo ya elimu ya juu hauna budi kufuata utaratibu na historia ya familia.

Rais Magufuli alisema hatarajii mtoto wa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi (aliyekuwapo katika mkutano huo) wala wa mkuu wa mkoa au wa chuo kupata mkopo wa elimu ya juu.

“Hili suala la mikopo lina changamoto, ndiyo maana tunapotoa tunaangalia historia ya mtu. Huwezi kumsomesha mtoto shule ya msingi binafsi, halafu baadaye aje kuomba mkopo. Hao waliokusomesha wako wapi? Na kama hawapo tutataka uambatanishe nyaraka za kuonyesha hawapo", alisema Rais Magufuli.

Ujenzi wa hospitali

Awali, akiweka jiwe la msingi la hospitali ya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Rais Magufuli alieleza sababu ya kukwamua ujenzi huo uliokwama kwa miaka mitano.

Rais Magufuli alisema watu wa Kilolo ni wachapakazi na wasiopenda rushwa, akirejea namna alivyopata wadhamini alipoomba kuteuliwa kuwania urais ndani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Rais Magufuli alisema mwaka 2015 alifika Iringa kutafuta wadhamini, lakini aliambiwa wote wamenunuliwa, hata alipojaribu kutaka kwenda Isimani nako alielezwa na Lukuvi kuwa wameshanunuliwa.

Pia Rais Magufuli alisema kutokana na hilo ilimbidi kuchagua kuondoka Iringa bila wadhamini au kutafuta mkoa mwingine, hata alipojaribu kuuliza Tosamanganga aliambiwa vivyo hivyo.

“Nilichofanya ndugu zangu nikashika ile barabara ya kuja Kilolo, nikafika katika vijiji viwili vya Ndiwili na Kilabo. Waliponiona wananchi wakaniuliza wewe Magufuli (John) umekuja kufuata nini huku? Nikawajibu nimekuja kutafuta wadhamini", alisema Rais Magufuli.

“Wananchi wakaniambia nisubiri hapahapa na wakajitokeza wadhamini zaidi ya 60 katika vijiji hivi viwili ambao walinidhamini bila kutoa fedha,” alisema Rais Magufuli ambaye alikuwa ni miongoni mwa makada 42 wa CCM waliojitokeza kuomba kuteuliwa kugombea urais ndani ya CCM", alisema Rais Magufuli.

“Walionidhamini katika Mkoa wa Iringa wote wametoka Wilaya ya Kilolo na siwezi kuisahau. Ndio maana mheshimiwa Jafo (Selemani- Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tamisemi) aliponiambia kuna hospitali imekwama tangu mwaka 2011, haijapata fedha na wanataka kujenga hospitali ya wilaya, nikasema pelekeni,” alisema.

Aidha, Rais Magufuli alisema tayari Serikali imeshatoa Sh2.2 bilioni kati ya Sh4.2 bilioni zinazohitajika kukamilisha ujenzi.

“Tutahakikisha hospitali hii inakamilika. Mkandarasi wa hospitali hii, TBA (Wakala wa Majengo Tanzania), fanyeni kazi usiku na mchana ili ujenzi huu ukamilike, ndiyo maana nimekuja kuiwekea jiwe la msingi, nitakuwa naifuatilia ole wenu isikamilike,” alisema Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Popular