Sakata la Mlinga na Mkuu wa wilaya kuwachoma wanafunzi sindano Limeibuka Bungeni. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 3 May 2018

Sakata la Mlinga na Mkuu wa wilaya kuwachoma wanafunzi sindano Limeibuka Bungeni.

 
Picha za Mbunge wa Ulanga, Mhe Goodluck Mlinga (CCM) na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Asumpter Mshana zikiwaonyesha wanawachoma chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi wasichana, zimezua mjadala mzito bungeni baada ya wabunge kuitaka serikali kuwalipa fidia wanafunzi waliochomwa sindano hizo.

Katika picha hizo, viongozi hao wanaonekana wakiwachoma wasichana sindano ya begani kama ishara ya uzinduzi wa chanjo hiyo hali iliyosababisha wabunge hao kuijia juu serikali na kuitaka kuwachukulia hatua madaktari walioruhusu baadhi ya wabunge na wakuu wa wilaya na wanasiasa kufanya kitendo hicho, kuwalipa fidia na kuleta orodha ya watoto walioathirika kwa kuwa sindano za chanjo yoyote huwa hazichomwi kiholela.

Mjadala huo umeibuka leo bungeni jijini Dodoma baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika ambapo wabunge watatu waliomba muongozo kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kuahirisha shughuli za Bunge ili kujadili tukio hilo la dharura.

Wa kwanza alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest (Chadema), ambapo alisema amepata taharuki kuona watu ambao hawana taaluma ya udaktari au uuguzi wakichoma sindano watoto ambapo wanaweza kuwasababishia maradhi ikiwamo kupooza.

“Wakati tupo hapa ndani yapo mambo mengine yanaendelea kujitokeza kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambapo kumetokea madaktari wa ghafla wa dharura,

“Sasa naomba Spika Bunge liagize waliokubali kuchoma sindano waagizwe kuomba radhi na hao watoto wapewe fidia na kama haitoshi tupewe taarifa wale madaktari walioruhusu kitendo hicho kifanye mabaraza husika yanachukua hatua gani dhidi ya hao watu, alisema.

Hoja hiyo iliungwa mkono Mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Anna Gidarya naye aliomba muongozo wa Spika wa Bunge na kumwomba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kutoa kauli kuhusu zoezi la chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi.

Kwa upande wake Mbunge wa Temeke (CUF), Mhe Abdallah Mtolea alimuomba Spika wa Bunge kuahirisha shughuli za bunge kwa kutumia kanuni ya 47 (4) ili kujadili suala hilo.

“Matendo yaliyokuja kati siku mbili hizi za uzinduzi yanapeleka kuwafanya wazazi kuogopa kuwaruhusu watoto wao kwenda kupata hii chanjo. Matendo yaliyojitokeza ni haya Mshama ambaye si daktari lakini amekwenda kumchoma mtoto kama ishara ya uzinduzi", amesema Mhe Mtolea.

"Pia Mhe  Mlinga naye ameenda kwenye uzinduzi jimboni kwake na yeye akachukua sindano kumchoma mtoto wakati si mtalaamu na hata kama angekuwa mtaalamu siku hiyo hakuwa kwenye orodha ya watu waliopaswa kutoa chanjo", amesema Mhe Mtolea.

“Vitendo hivi vinawafanya wazazi kuwa na woga kwamba nikimruhusu mwanangu aende kwenye chanjo anaweza kuwa wa kwanza kuchomwa sindano na mgeni rasmi ambaye si mtaalamu,” amesema Mhe Mtolea.

Akijibu mwongozo huo Spika Ndugai alisema anaiachia serikali iendelee kulitazama jambo hilo kwa ukaribu kwa sababu ni madai mengi na mazito.

Akitoa ufafanuzi Waziri Ummy amesema: “Uchomaji wa sindano una taratibu zake, huwezi kuchoma sindano ovyo ovyo, lakini jambo la pili nimesimama hapa kuwahakikishia Watanzania wote kwamba Mlinga na Asumpter hawakuwachoma sindano watoto husika, walikuwa wanafanya majaribio tu,” amesema Ummy na kuzomewa na baadhi ya wabunge.

Aidha, aliagiza waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuzingatia miongozo ya utoaji wa huduma za afya kwani hata kitendo cha kushika sindano kama si mtalaam si kitendo cha kitaaluma.

2 comments:

Popular