Wateja wa benki zilizofilisiwa na BOT kulipwa kiasi kisichzidi milioni 1.5. - KULUNZI FIKRA

Friday, 5 January 2018

Wateja wa benki zilizofilisiwa na BOT kulipwa kiasi kisichzidi milioni 1.5.

 
  Bila kujali ni kiasi gani walitunza, wateja kwenye benki tano zilizotangazwa kufilisika, wataambulia si zaidi ya Sh1.5 milioni ya amana zao kwa mujibu wa sheria.

 Juzi Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu aliwaaga Watanzania baada ya kuiongoza taasisi hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa kwa miaka 10 mfululizo na kueleza kuwa tayari benki zilizofilisika zimekabidhiwa katika Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kwa taratibu za kisheria.

 Kaimu mkurugenzi wa bodi hiyo, Richard Malisa alimhakikishia Profesa Ndulu kuwa taratibu za malipo hayo zitafanyika haraka iwezekanavyo huku kiwango cha juu kitakacholipwa kwa wateja kikiwa ni Sh1.5 milioni.

“Mwenye amana za Sh100,000 atalipwa kiasi hicho na mwenye Sh50,000 atalipwa hiyo ila kiwango cha mwisho ni Sh1.5 milioni. Kwa hiyo, kama wewe una Sh5 milioni utakacholipwa ni Sh1.5 milioni,” alisema.

 Taasisi tano zilizotangazwa kufilisiwa ni Benki ya Wanawake Convenant na Efatha. Nyingine ni benki za wananchi; Njombe na Meru pamoja na Benki ya Wakulima Mkoa wa Kagera (KFCB) ambazo zinaungana na FBME, Twiga Bancorp na Benki ya Wananchi Mbinga zilizofilisika na kufutiwa leseni mwaka jana.

 Nyingine tatu zimewekwa chini ya uangalizi ambazo ni Benki ya Ushirika Kilimanjaro, Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) na Benki ya Wananchi Tandahimba ambazo, endapo zitashindwa kukidhi vigezo, baada ya muda, nazo zitafilisiwa.

 Kuhusu athari za kufungiwa na kufilisiwa kwa benki hizo Profesa Ndulu alisema jumla ya amana za benki zote nane ni Sh67.6 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 0.38 ya benki zote 58 zilizopo nchini hivyo kutokuwa tishio.

“Hakuna athari zozote za kiuchumi zinazoweza kujitokeza kutokana na kufungiwa kwa benki hizi. Lakini, endapo tungeziacha ziendelee kujiendesha hivyohivyo, madhara yake yangekuwa makubwa,” alisema.

 Profesa Ndulu alitaja sababu za benki ndogo kutofanya vizuri kuwa ni kutokana na kukosa mtaji, wigo mdogo wa biashara, ukubwa wa bodi zinazozisimamia pamoja na gharama kubwa za uendeshaji.

 “Tumewashauri waungane, wawe shirikisho halafu hizo benki nyingine ziwe matawi kusaidia mfumo wao wa undeshaji uwe mmoja kupunguza gharama lakini utekelezaji umekuwa mgumu,” alisema.

 Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Benki za Kijamii (Cobat), Lukwaro Senkoro alikiri kupewa ushauri huo na BoT lakini akasema muda haukuwa rafiki kwao kuutekeleza ingawa hatua za makusudi zilichukuliwa.

 Alisema katika jitihada hizo za kukamilisha mchakato wa kuziunganisha benki za wananchi, chama hicho kilianza kwa kukutana na bodi za wakurugenzi wa benki husika ambazo ziliafiki ushauri huo na kuahidi kwenda kuzungumza na wanahisa wao.

 “Huko ndiko kulikosumbua,” alisema. “Benki sita zilikubali kuungana lakini tatu wanahisa wake wanahitaji muda wa ziada kufikiri kuhusu suala hilo,” alibainisha.

 Alisema kwenye mkakati wao, walishafanikiwa kumpata mwekezaji atakayeiwezesha Benki ya Taifa ya Wananchi ambayo ingeanzishwa lakini baada ya benki tatu kutangazwa mufilisi, mchakato huo utakuwa umefika mwisho.

 Alisema ushauri wa BoT ni wazo jipya lililohitaji kujadiliwa na wadau kabla ya kuridhia kuungana na kujiendesha chini ya mwamvuli mmoja hivyo kuhitaji muda wa kutosha wa uelimishaji.

“Ushauri ulitolewa Juni na tulipewa mpaka Oktoba tuwe tumekamilisha taratibu ili Novemba mwaka jana tuungane.

 Tumepambana mpaka mwisho lakini hatujafanikiwa. Kwa sasa mpango huo hautekelezeki,” alisema kwa masikitiko.

    Wateja waduwaa
 Taarifa za kufilisiwa kwa benki hizo zilianza kusambaa jana asubuhi hivyo kuwashtua wateja wake. Baadhi ya wateja wa KFCB waliishia nje ya lango la benki hiyo baada ya kukosa huduma.

 Zablon Zakayo alikuwa miongoni mwa wateja waliolalamikia kukosa huduma baada ya kuagizwa na mafundi wenzake kwenda kuchukua Sh600,000 kwa ajili ya shughuli zao.

    “Mimi ni kiongozi wa umoja wa mafundi wa kuchomelea vyuma,” alijitambulisha Zakayo.

  Mteja mwingine, Oscar Anta alisema alienda kuchukua fedha za wanachama wa kikundi chao cha ujasiriamali ili wagawane kwa ajili ya kulipa ada za watoto lakini ilishindikana bila kuelezwa hatima ya fedha zao.

Mwingine alikuwa Adelifunsi Archard, aliyeiomba Serikali kuwasaidia wateja wa benki hiyo kupata fedha zao ili watekeleza mipango yao.

Wateja wa Meru Community Bank Limited (MecoB) walioenda kupata huduma waliwakuta wafanyakazi wa taasisi hiyo wakihojiwa na maofisa wa BoT na kuchunguza baadhi ya nyaraka.

 Mmoja wa wateja hao ambaye hakupenda kutajwa jina, aliiomba Serikali kuhakikisha fedha zao zinaendelea kuwa salama. “Kama Serikali imejiridhisha kuwa benki imekosa sifa, naunga mkono lakini kwa nini Serikali haikuisadia kuongeza mtaji?” alihoji.

  Kwenye mkutano wa nne wa mwaka wa benki hiyo uliofanyika Desemba 2016, wanahisa waliiagiza bodi ya wakurugenzi kumtafuta mwekezaji mwenye uwezo ili kuinusuru dhidi ya tishio la kukosa sifa za kisheria zilizowekwa na BoT.

 Wakati huo, aliyekuwa mwenyekiti wa bodi, William Maeda (sasa marehemu) alisema benki hiyo iliyoanzishwa mwaka 2011 ilikuwa na mtaji wa Sh400 milioni. Mwaka 2016 ilikuwa na wanahisa 1,320 ambao ni watu binafsi waliokuwa na asilimia 74 ya hisa zote. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Meru lilikuwa na asilimia 10 na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) kilikuwa na asilimia saba.

    Mtaji

Awali, zilikuwa zinahitajika Sh500 milioni kuanzisha benki lakini Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 inazitaka taasisi zote za fedha kuongeza kiasi hicho cha mtaji mpaka Sh2 bilioni.

Mwaka 2012, Profesa Ndulu alizitaka benki zisizo na kiasi hicho nyingi zikiwa za jamii kuongeza mtaji mpaka kiasi kinachopendekezwa na sheria na akazipa miaka mitano, mpaka mwaka jana lakini nyingi hazijafanikiwa kutimiza matakwa hayo.

 Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mpaka Juni mwaka jana, ni Benki ya Maendeleo, Benki ya Uchumi na Benki ya Wananchi Mufindi (Mucoba) kwa upande wa benki za jamii ndizo zilizokuwa zimefanikiwa kutimiza sharti hilo kati ya 12 zilizopo.

    Profesa Ndulu aaga

 Mbali ya kuzungumzia hatua ya kuzifilisi benki hizo tano, Profesa Ndulu alitumia nafasi hiyo kuwaaga wafanyakazi wa BoT na Watanzania kwa ujumla huku akijivunia mambo kadhaa aliyoyafanya ndani ya miaka 10 ya uongozi wake.

 Mpaka anaondoka, alisema anaacha asilimia 65.5 ya Watanzania wanatumia huduma za fedha ikilinganishwa na mwaka 2006 walipokuwa na asilimia tisa.

    “Dunia ilipoingia kwenye mtikisiko wa uchumi mwaka 2008/2009 hadi 2010/2012, BoT ilihakikisha kunakuwapo utulivu wa uchumi nchini. Mtu mmojammoja hawezi kuona ukuaji wa uchumi kwa sababu Serikali inatoa huduma kwa wananchi wote kwa ujumla,” alisema.
    

No comments:

Post a Comment

Popular