Viwanda vitano vimepingwa faini ya milioni 180 kulipwa ndani ya saa 24. - KULUNZI FIKRA

Friday, 5 January 2018

Viwanda vitano vimepingwa faini ya milioni 180 kulipwa ndani ya saa 24.

 WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe  Luhaga Mpina amewaamuru wamiliki wa viwanda vitano vya kuchakata minofu ya samaki vilivyoko Mwanza, kulipa faini ya Sh milioni 180 ndani ya saa 24 baada ya kubainika kupokea na kuchakata samaki wasioruhusiwa.

Kwa mujibu wa Waziri Mpina, wamiliki wa viwanda hivyo wamekiuka Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2009, sambamba na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004. Waziri Mpina alisema amechukizwa na kitendo cha viwanda hivyo kufadhili uvuvi haramu na kueleza kuwa ni bora kutokuwa na kiwanda hata kimoja cha samaki kuliko kuendelea kuwa na viwanda vinavyofadhili uvuvi haramu.

Alitishia kuvifunga viwanda vyote, vitakavyobainika kuchakata samaki wasioruhusiwa na kutaifisha samaki, magari na boti zinazobeba samaki hao wasioruhusiwa. Mpina alitoa uamuzi huo jana kwa nyakati tofauti, wakati alipofanya ziara kutembelea viwanda vinavyochakata samaki jijini Mwanza. Mbali ya kuvipiga faini viwanda hivyo, pia alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Yohana Budeba kuwasimamisha kazi maofisa watatu wa Kitengo cha Udhibiti wa Usalama na Ubora wa Mazao ya Uvuvi Kituo cha Mwanza kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kulisababishia taifa hasara kubwa.

Maofisa hao ambao pia aliagiza wachukuliwe hatua kali za kinidhamu ni Philemon Mugabo, Dorina Mlenge na John Bosco Rubajuna. “Haiwezekani mimi nije hapa kukagua samaki waliovuliwa na watendaji wa serikali ngazi zote wapo na sijawahi kupata taarifa yoyote wizarani ya hatua zilizochukuliwa iwe kwa kupigwa faini au la.

“Hivyo watumishi wa serikali wote wanaohusika na Kitengo cha Udhibiti wa Usalama na Ubora wa Mazao ya Uvuvi Kituo cha Mwanza wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wasimamishwe kazi kuanzia leo na wachukuliwe hatua kali za kinidhamu,” alisema Mhe  Mpina.

Alitaja viwanda vilivyokutwa vikichakata samaki wasioruhusiwa wakiwemo samaki wazazi na samaki wachanga na idadi ya kilo zilizokamatwa kwenye mabano kuwa ni Nile Perch Fish (920), Victoria Fish (131), Nature Fish (150), Omega Fish (580) na Tanzania Fish Processing (842). Pia magari 41, boti 15 vilikamatwa huku nyavu haramu 294 zikikutwa zikiwa na samaki wachanga na wazazi, ambapo sheria inakataza kuvuliwa samaki chini sentimita 50 na juu ya sentimita 85.

Majina ya viwanda hivyo na faini walizotozwa ni Nile Perch Sh milioni 25, Tanzania Fish Processing Sh milioni 50, Victoria Perch Sh milioni 30, Nature Fish Sh milioni 25 na Omega Fish Ltd Sh milioni 50.

Alisisitiza kuwa adhabu hiyo ni ya kwanza na ya mwisho na kwamba ikithibitika tena, wenye viwanda wanaendelea kufadhili uvuvi haramu hatua za kuvifunga viwanda na kutaifisha mali ikiwemo mitumbwi, boti na magari yatakayokuwa yanabeba samaki hao itafuata. Mpina alisema ukanda wa Ziwa Victoria ulikuwa na viwanda 13 vya kuchakata samaki vilivyokuwa na uwezo wa kuchakata tani 1,065 kwa siku. Lakini kutokana na kushamiri kwa uvuvi usiozingatia sheria, kumesababisha viwanda vitano kufa kutokana na kukosekana malighafi.

Kwamba viwanda vinane vilivyobaki sasa, vinachakata tani 171 tu kwa siku huku ajira zikiwa zimeporomoka kutoka ajira 4, 088 na kufikia 2,179 tu. Mpina alisema tayari Rais Magufuli alishatoa maagizo kwa wavuvi kuachana na uvuvi haramu sambamba na wenye viwanda kutofadhili uvuvi huo; huku pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye akisisitiza jambo hilo.

Alivitaka viwanda kuwa chimbuko na chemchemi ya kupinga uvuvi haramu kwa kutokubali kupokea samaki waliovuliwa kinyume cha sheria, wakiwemo samaki wazazi na samaki wachanga na kuwataka kutoa taarifa haraka kwenye vyombo vya dola pindi wanapoletewa samaki wa aina hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Yohana Budeba alisema kama watumishi wa wizara yake wangesimamia majukumu yao kikamilifu, mambo hayo aliyobaini Waziri Mpina yasingejitokeza huku akikiri kupokea maagizo yake yote na atayasimamia kwa haraka kuona yanatekelezwa. Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Nile Perch Fisheries Limited, Peter John alisema wameridhika na adhabu iliyotolewa na kukiri mbele ya Waziri Mpina kuwa hawatarudia tena kufanya kosa hilo.

No comments:

Post a Comment

Popular