TAKUKURU yamshikilia Anthony Diallo. - KULUNZI FIKRA

Friday, 1 December 2017

TAKUKURU yamshikilia Anthony Diallo.

 TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), imemtia mbaroni, Anthony Mwandu Diallo, ikimtuhumu kugawa mrungula katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mwanza.

Taarifa kutoka Mwanza zinasema, Diallo alitiwa mbaroni leo Ijumaa, majira ya saba mchana wilayani Ukerewe, ambako inaelezwa kuwa alikwenda visiwani humo kugawa fedha ili kuwashawishi wajumbe wa mkutano mkuu mkoani humo, kumchagua kuwa mwenyekiti wao.

Uchaguzi mkuu wa CCM kwenye ngazi ya mikoa umepangwa kuanza kuanzia Jumamosi hii mkoani Mwanza uchaguzi huo umepangwa kufanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza, Ernest Makale amethibitisha kushikiliwa kwa Diallo na taasisi yake.

Amesema, “ndio tunamshikilia Anthony Diallo, kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi. Tumefanya hivi,  baada ya kupata taarifa kuwa anagawa fedha kwa wapiga kura katika uchaguzi utakaofanyika kesho.”

Anasema, taasisi yake inaendelea kumhoji Diallo na  baada ya hapo hatua nyingine zitachukuliwa kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu.

Diallo, anayegombea nafasi hiyo kwa mara ya pili, katika uchaguzi huu, anakabiliwa na kibarua kigumu cha kukabiliana na mpinzani wake wa karibu, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Meck Sadick.

Sadick ambaye aliamua kustaafu nafasi yake ya mkuu wa mkoa kwa hiari, anaonekana kuungwa mkono na wajumbe wengi wa mkutano huo, jambo ambalo linadaiwa kumlazimisha Dialo, kuamua kutembeza fedha kutetea kiti chake.

Kulunzifikra blog  imeshindwa kumpata mwanasiasa huyo kujibu madai hayo, Mwandishi alipomtafuta kwa simu yake ya mkononi majira ya saa 15: 51 (Jana), mara zote simu yake  ilikuwa inaita bila kupokelewa.

Hata hivyo, mara kadhaa Diallo amekuwa akikana madai kuwa anatumia fedha kutafuta ushindi.

Amesema, tuhuma kuwa anatumia fedha kuhalalisha uenyekiti wake, zimekuwa zikitolewa na baadhi ya wapambe wa mshindani wake huyo.

Diallo ambaye amepata kuwa waziri katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete na mmiliki wa kituo cha televisheni cha Star TV na Radio Free Africa, amekuwa akiandamwa pia na tuhuma za kumchafua mgombea mwenzake.

No comments:

Post a Comment

Popular