Libya yatoa majibu kuhusu biashara ya waafrika weusi inayoendelea. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 30 November 2017

Libya yatoa majibu kuhusu biashara ya waafrika weusi inayoendelea.

 
 Mgogoro wa kuuza watu unaoendelea Libya umechukua sura mpya baada ya vyombo vya habari kuripoti matukio ya kuteswa na kuuzwa kwa Waafrika weusi ambao wanakimbia hali ngumu ya kimaisha katika nchi zao na kwenda Ulaya kupitia Libya.

Libya imekuwa mlango muhimu ambao unaunganisha nchi za Afrika na Ulaya, Waafrika wamekuwa wakisafiri hadi katika miji ya Pwani ya nchi hiyo ili wapate mpenyo wa kuingia katika nchi hizo ambazo zinatajwa kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

Kutokana na nchi ya Libya kuwa katika mzozo mkubwa wa kisiasa ambao umeitumbukiza nchi hiyo kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, maharamia wa baharini hufanya biashara ya kuwasafirisha Waafrika ambao wanavuka bahari kwenda Ulaya.

Hata hivyo, biashara hiyo imegeuka na kuwa ya kuuza watumwa ambao huteswa, kupigwa na kuumizwa

Changamoto iliyopo

Kutokana na kubadilika kwa sera za uhamiaji na idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia Ulaya, baadhi ya nchi zimezuia kabisa wahamiaji toka Afrika kuingia katika nchi zao. Hali hiyo imesababisha wakimbizi wengi kukwama nchini Libya ambapo inasemekana wanapata mateso, kuumizwa na wengine kuuzwa kama watumwa ili wakutumikie kazi katika maeneo mbalimbali ya kazi.

Taharuki hiyo inajitokeza ikiwa zimepita siku chache baada ya Kituo cha runinga cha CNN kuonyesha baadhi ya picha za Waafrika weusi wakiwa kwenye mnada wa watumwa nchini Libya. Wanasiasa, wanaharakati na watu mashuhuri wamejitokeza na kulaani matukio yanayoendelea katika nchi hiyo na kuutaka Umoja wa Mataifa (UN) kuchukua hatua za haraka kunusuru mgogoro huo.

Licha ya CNN kulipoti matukio hayo kwa undani lakini bado kuna maswali mengi ambayo hayajajibiwa ikizingatiwa kuwa kuna taarifa nyingi za uongo zinazosambaa kuhusiana na hali ya Libya kwa wakati huu.


Baadhi ya Wahamiaji wakiwa kwenye boti

Mkazi wa Libya aelezwa undani wa kinachoendelea

Fikra Pevu imepata mahojiano ya Mwanahabari wa chombo kikoja cha kimataifa, Rashid  Chilumba na mkazi mmoja wa Libya ambaye alijitambulisha kwa jina la Abdorahim Nwiji ambapo anasema yale yanayotangazwa na vyombo vya habari vya kimataifa juu ya utumwa unaoendelea Libya ni propaganda ambazo zinalenga kuharibu sifa ya nchi hiyo katika diplomasia ya kimataifa.

Abdorahim anasema, “Sikia kaka, hayo unayoyaona usiyazingatie. Yote unayoyaona yametushtua zaidi walibya kuliko ulivyostuka wewe. Ukweli ni kwamba nchi za Magharibi hasa Ulaya zimekuwa kwenye mzozo wa wahamiaji haramu kwa muda sasa.

Serikali zimezidiwa na wanasiasa wanaounga mkono sera za uhamiaji wameondolewa madarakani au umaarufu wao umesinyaa. Umoja wa Ulaya umegawanyika mno na hata uamuzi wa Uingereza kujitoa kwenye umoja huo sehemu ya sababu zake ni uhamiaji hasa haramu.

Kwa hiyo viongozi wa ulaya wamechanganyikiwa na watu kutoka Afrika wanazidi kumiminika na mipango yao yote ya kuwazuia imeshindikana. Kwa hivyo wameamua kutengeneza video na picha nyingi za propaganda na kuzieneza kwa kasi ili kuwatisha waafrika kuhusu Libya ili waachane na mipango ya kutoroka kwao kwenda Ulaya kupitia Libya.

Hebu ona wewe picha hizo zimekutisha hata kutembelea Libya kihalali vipi wengine walio na mipango ya kwenda ulaya kupitia Libya kwa njia haramu watathubutu?”, anaeleza mkazi huyo wa Libya na kuongeza kuwa,

“Pia sababu ya pili baadhi ya nchi za Ulaya hasa Ufaransa wanataka kuichukua sehemu ya Kusini ya Libya yenye rasilimali nyingi. Hivyo propaganda hii itatengeneza mazingira ya kuingia tena Libya kwa mgongo wa msaada wa kiutu.

Ufaransa ilikuwa mstari wa mbele kumtoa Gaddafi na Rais wa wakati ule Nicolaus Sakorzy alikuwa kiongozi wa kwanza akiongozana na David Cameron wa Uingereza kuja Libya siku chache tu baada ya Gaddafi kufa. Wakasema waliyosema lakini wanataka rasilimali tu hawana lolote”.

Abdorahim ambaye hivi karibuni alikuwa Ulaya kuhudhuria kozi ya kuandaa maudhui ya vyombo vya habari ili kukabiliana na ongezeko la misimamo mikali  hasa katika nchi za Mashariki ya Kati na Kaskazini ya Afrika, anaendelea kusema,

“Kaka sisi ni waafrika na tuna marafiki wengi kutoka Afrika na tuna programu nyingi tu zinazowasaidia waafrika kutokimbilia Ulaya. Hatuwezi kufanya unyama huo.

Biashara ya kusafirisha watu

Abdorahim  anakubali kuwa biashara ya kusafirisha Waafrika kwenda nchi za Ulaya imeshamiri na inawaingizia fedha nyingi.

“Lakini kingine kinachoendelea cha ukweli  ni kwamba walibya wanaingiza hela nyingi sana kwa kuwasaidia waafrika kwenda Ulaya. Wahamiaji wanalipa maelfu ya Dola kuvuka na walibya wanawasaidia kwenda huko siyo kuwauza na sisi tumekuwa tunapigania sana hiyo biashara ya kusafirisha watu kwenda Ulaya ikome.

Halafu ni CNN ndiyo kwa sehemu kubwa imeripoti hizo taarifa na sehemu kubwa ya picha hazitoki Libya, ‘google’ inaweza kukusaidia.

Mfano kituo cha runinga cha France24 kiliripoti kuhusu kijana mmoja kutoka Cameroon akidai Libya ilimchukua kama mtumwa na kumlazimisha kufanya kazi katika shamba la njugu (pistachio) Kusini mwa eneo la Jangwa lakini cha kushangaza Libya hailimi njugu na hata walibya tumeshangaa kusikia tunalima njugu.

Picha halisi kutoka Libya ni zile zinazoonesha makundi ya wahamiaji kwenye kambi wakiwa na wanajeshi wa serikali kwa lengo la kuwahesabu na kuwasaidia kurudi makwao. Unaweza tizama juhudi hizo kupitia tovuti ya shirika la uhamiaji la ulimwengu (IOM) na utawaona walibya halisi”,

Watanzania Walaani

Wananchi wa Tanzania wakiwemo wanasiasa wamelaani matukio yanayoendelea Libya na kutaka hatua zichukuliwe ili kurejesha heshima ya Afrika kwasababu biashara ya utumwa ilikomeshwa miaka mingi iliyopita.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika, “Kwa nini Watanzania waliopo Dar tusichukue hatua dhidi ya udhalilishaji wa Waafrika? Siku ya Ijumaa tukutane ubalozi wa Libya hapa nchini kuongea na Balozi na kumpa risala yetu kupinga Biashara ya Utumwa inayofanyika nchini Libya”.

Kabla ya kutimiza hazma hiyo, Ubalozi wa Libya nchini umetoa tamko na kusema taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu kile kilichotokea kama tukio la mapatano ya mauzo na manunuzi ya watu walio na asili ya Afrika ni kwamba huenda makusudio ya tukio hilo yalikuwa ni kuwatorosha ili wafike katika kituo chao cha mwisho (Ulaya)kama wahamiaji na wala sio kama watumwa.

 Hatua iliyochukuliwa na Jumuiya za Kimataifa

Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (EU) wamekubaliana kuwarejesha wakimbizi hao katika nchi zao, wakati taratibu nyingine za uchunguzi juu ya biashara ya utumwa katika nchi hio zikiendelea.

Akihojiwa na kituo cha runinga cha AFP, kiongozi mmoja kutoka Ufaransa ambaye alishiriki katika kikao cha UN kilichofanyika mwanzoni mwa wiki hii amesema, “Tunawasaidia Waafrika ambao wanataka kurudi kwa hiari katika nchi zao. Hii kazi itafanyika siku chache zijazo kwa kushirikiana na nchi wanazotoka”.

Naye Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ameandika katika ukurasa wa Twitter, “Hali ya Libya ya kuuza watu utumwani; inaogopesha na haikubaliki. Tutafanya kila liwezekanalo kuwalinda raia wetu kokote walipo. Pia tumeanza kuwarudisha Wazimbabwe wote waliokwama Libya na kwingine kote ikiwa ni hatua ya kupinga”.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) linasema kuwa mwaka jana liliratibu safari za wahamiaji 13,000 kurudi kwa hiari katika nchi zao hasa za Kusini mwa Jangwa la Sahara wakitokea Libya

No comments:

Post a Comment

Popular