Simba na Ashanti zagombea uwanja wa uhuru - KULUNZI FIKRA

Saturday 2 September 2017

Simba na Ashanti zagombea uwanja wa uhuru

 
 Dar es Salaam. Simba na Ashanti United zimeingia vitani kuwania Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kuutumia katika mechi zao za kirafiki  zitakazofanyia kesho Jumapili.

Simba imepanga kucheza na  timu ya jeshi ya Hardrock  ya Pemba  kesho jioni kwenye Uwanja wa Uhuru wakati Ashanti nayo imepanga kuikabili Yanga kesho kwenye uwanja huo huo .

Awali Simba ilikuwa icheze na Hard Rock jana  lakini ikapigwa stop  na kuambiwa kuwa uwanja huo siku hiyo utatumika kwa ajili ya mazoezi ya  Botswana ambayo  ilikuwa ikijiandaa kucheza na Taifa Stars leo.

Afisa Habari wa Ashanti United, Adam Kinyogoli alisema wanachojua kesho wao ndio wanatakiwa kuutumia uwanja huo kuikabili Yanga hivyo Simba wakatafute uwanja mwingine.

"Tulishaomba kucheza na Yanga Jumapili  kwenye Uwanja wa Uhuru hivyo hiyo mechi ya Simba hatuitambui kwani ninavyojua Simba ilitakiwa kuutumia uwanja huo Ijumaa(jana) lakini  wanajua wenyewe sababu za kuhairisha hiyo mechi siku hiyo"alisema Kinyogoli

Alipoulizwa  Kinyogoli kama endapo wataenda uwanjani na kukutana na Simba itakuaje?alijibu" Itajulikana uko uko kwani ninavyojua kuwa sisi ndio wenye haki ya kuutumia huo uwanja kesho sasa Simba wakija nao shauri yao".

Alipoulizwa tena  je kama wamiliki wa Uwanja wakiwazuia kuutumia uwanja huo na kuiruhusu Simba iutumie watafanyaje, alijibu" Mpaka jioni hii hakuna taarifa zozote za kutuzuia kucheza mchezo huo  na sidhani kama itatotea hilo".

 Naye mkuu wa mawasiliano wa Simba,Haji Manara alisema anachojua ni kwamba kesho wanacheza mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Uhuru hivyo hizo taarifa za mechi nyingie hawana.

"Sisi tunacheza mechi kesho na Hard Rock saa hizo taarifa za mechi ya Yanga na Ashanti sizijui"alisema Manara.

No comments:

Post a Comment

Popular