Rais Magufuli asali na wasabato - KULUNZI FIKRA

Saturday 2 September 2017

Rais Magufuli asali na wasabato

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli tarehe 02 Septemba, 2017 wameungana na waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Usharika wa Magomeni Mwembechai Jijini Dar es Salaam kusali Ibada ya Sabato.

Ibada hiyo imeongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania, Baba Askofu Mark Walwa Malekana aliyekuwa pamoja na Askofu wa Jimbo la Mashariki Kati, Baba Askofu Joseph Mgwabi na Askofu wa Jimbo la Kusini Mashariki, Baba Askofu Albert Nziku.

Rais Magufuli amelipongeza Kanisa hilo kwa kutoa huduma ya kiroho kwa waumini wake na pia kutoa huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini, na amewahakikishia waumini na viongozi wake kuwa Serikali inatambua mchango huo na itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini katika kuwahudumia wananchi.

“Baba Askofu nakushukuru sana kwa mahubiri mazuri ya leo ambayo yamenigusa sana, madhehebu ya dini likiwemo hili la Waadventista Wasabato mnatoa mchango mkubwa sana kwa Taifa letu, nakuhakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nanyi” Amesema Mhe. Rais Magufuli.

Pamoja na kushiriki Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 na mifuko 400 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa jipya la Waadventista Wasabato Usharika wa Magomeni Mwembechai, amechangia Shilingi Milioni 1 kwa kwaya za Kanisa hilo na pia ameendesha harambee ya papo kwa papo ya kuchangia ujenzi wa Kanisa, na kufanikisha kupata Shilingi Milioni 25.3.

Baba Askofu Mark Walwa Malekana amemshukuru Mhe.

Rais Magufuli kwa kuungana na waumini wa Kanisa hilo katika Ibada ya Sabato na kuchangia ujenzi wa kanisa, na ameongoza maombi ya kuliombea Taifa na Rais.

No comments:

Post a Comment

Popular