Ngoma,Ajibu zilipendwa! - KULUNZI FIKRA

Saturday 2 September 2017

Ngoma,Ajibu zilipendwa!

 KUREJEA kwa Obrey Chirwa katika kikosi cha Yanga kunamaanisha kwamba kombinesheni ya Ibrahim Ajibu na Donald Ngoma imegeuka kuwa zilipendwa.

Kwa uhalisia ulivyo, Chirwa atawatenganisha mastaa hao kiuchezaji hasa kutokana na matokeo ya mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Lipuli, lakini wanaweza kuwemo kwenye kikosi cha kwanza kwa nafasi tofauti.

Kocha George Lwandamina ambaye amefurahishwa na kurejea kwa Chirwa, atatua Dar es Salaam kesho Jumapili akitokea kwao Zambia alikokwenda kwenye msiba wa Baba yake.

Chirwa ametolewa kifungoni baada ya kukosekana na hatia kwenye kesi ya utovu wa nidhamu ya Mei 20 mwaka huu, hivyo yuko huru kuitumikia Yanga katika mechi za ligi baada ya kukosekana katika mchezo wa kwanza dhidi ya Lipuli wa sare ya bao 1-1. Awali aliikosa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Ujio wa mshambuliaji huyo mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kupiga chenga, utaitikisa pacha ya Ajibu na Ngoma ambayo imefunga bao moja tu katika mechi mbili zilizopita. Chirwa huenda akaanza akiwa mshambuliaji namba moja akisimama mtu wa mwisho huku Ngoma ama Ajibu akipangwa kucheza nyuma yake.

Mzambia huyo aliyefunga mabao 12 msimu uliopita, staili ya uchezaji wake inampa nafasi kubwa kuanza katika kikosi hicho ambapo mtihani kwa Lwandamina utakuwa ni kwamba Chirwa aanze na nani katika kikosi hicho kati ya Ajibu na Ngoma.

Hata hivyo Lwandamina anaweza kuamua kuwatumia wote watatu kwa pamoja ambapo Ajibu atacheza winga upande wa kulia huku Chirwa na Ngoma wakicheza katikati. Mtihani mkubwa unabaki kwa Mrundi Amissi Tambwe ambaye akirejea naye huenda akaingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza.

LWANDAMINA ANENA

Akizungumza na kulunzifikra blog akiwa kwao Ndola, Zambia, Lwandamina alisema amepokea kwa furaha taarifa za kurejea kwa Chirwa kwani ubora wa mshambuliaji huyo utaongeza ushindani.

“Tulipokuwa tunamkosa kuna kitu kilipungua, si huyo tu, wote ambao tunawakaosa wana nafasi yao katika timu yetu,” alisema Mzambia huyo.

Lwandamina ambaye amewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Zambia aliongeza: “Tulikuwa tunawatumia Ajibu na Ngoma, lakini ukiangalia hawa ni washambuliaji wenye aina moja ya ushambuliaji, tulikuwa tunahitaji kitu tofauti kitakachowafanya Ngoma na Ajibu wawe bora zaidi.

“Obrey ni mshambuliaji ambaye anaingia ndani ya boksi, anapenda kuwalazimisha mabeki, akiweza kuelewana vyema na wenzake kati ya hawa wawili, nafikiri tutakuwa na safu bora zaidi ya mabao, lakini pia sasa tunaweza kuwa na nafasi ya kuchagua kwa upana zaidi nani aanze na nani aingie kubadili mchezo.” Kocha huyo atakaporejea nchi i kesho, Jumatatu ataanza majaribio ya beki Mkongomani, Kayembe Nkaku, aliyeletewa na Papy Tshishimbi kwa ajili ya usajili mdogo wa mwezi Novemba.

No comments:

Post a Comment

Popular