Moto waua wanafunzi 7 bweneni - KULUNZI FIKRA

Saturday, 2 September 2017

Moto waua wanafunzi 7 bweneni

 Wanafunzi saba wa shule ya sekondari ya wasichana ya Moi iliyopo Kibra jijini Nairobi, wamefariki dunia baada ya bweni lao kushika moto mapema leo.

Waziri wa elimu nchini humo Dkt. Fred Matiang’i ambaye ametembelea eneo hilo amesema tukio hilo lililotokea majira ya saa nane usiku wa kuamkia leo,  limesababisha majeraha kwa wanafunzi 10 ambao tayari wamekimbizwa hospitali ya taifa ya Kenyatta na hospitali ya wanawake ya Nairobi.

Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa Kibra, Enos Maloba, makumi ya wanafunzi walizimia kutokana na moshi lakini walikimbizwa kwenye vituo vya afya vilivyo karibu na eneo la tukio.

Maloba amesema anaamini kwa nguvu zote kuwa moto huo umesababishwa na hitlafu ya umeme  na kuongeza kuwa timu ya wataalamu imepelekwa shuleni hapo kuchunguza tukio hilo.

Waziri Matiang’i amesema rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta, amevielekeza vyombo vyote vya upelelezi vya kiserikali, kuchunguza tukio hilo na kutoa ripoti ya tukio hilo leo Jumamosi hii ya Agosti 2.

 “Hatutaki hili kuwa moja ya zile kesi ambazo tumekuwa tukisema tutachunguza na kisha tutawaambia, tumeamua kufanya uchunguzi wote sasa hivi” alisema Matiang’i.

No comments:

Post a Comment

Popular