Makongoro Mahanga anusurika kwenda - KULUNZI FIKRA

Friday, 1 September 2017

Makongoro Mahanga anusurika kwenda

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana katika Serikali ya Awamu ya Nne, Makongoro Mahanga jana alinusurika kutupwa jela kutokana na kushindwa kutekeleza amri ya mahakama kulipa deni kila mwezi.

Mahanga ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Ukonga na Segerea kupitia CCM, aliamriwa kumlipa mwanasheria Kainerugaba Msemakweli kiasi cha Sh14 milioni zikiwa ni gharama za kesi alizozitumia katika kesi ya madai aliyofunguliwa na Mahanga.

Hata hivyo, Mahanga ameshindwa kumaliza deni hilo, baada ya kulipa kiasi cha Sh6 milioni tu mpaka sasa na hivyo kudaiwa Sh8 milioni.

Kutokana na kushindwa kulipa fedha hizo na kutokufika mahakamani bila taarifa, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Juni 16, ilitoa amri kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala kumkamata na kumfikisha mahakamani hapo.

Hata hivyo, hakuweza kutekeleza amri hiyo licha ya kukumbushwa mara kadhaa hadi mahakama hiyo ilipomtaka kamanda huyo mwenyewe afike mahakamani kujieleza ni kwa nini hajatekeleza amri hiyo.

Mahanga aliamriwa awe analipa Sh2 milioni kwenye akaunti ya Msemakweli kila mwezi na kuwasilisha risiti mahakamani hadi deni hilo litakapokwisha, lakini alipofika mahakamani jana baada ya kukamatwa, aliwasilisha risiti ya malipo ya Sh500,000 badala ya Sh2 milioni.

Mahakama ilikataa kuipokea risiti hiyo kwa kuwa kiasi hicho ni kinyume cha makubaliano na pia alikuwa nje ya muda wa makubaliano.

Kutokana na hali hiyo, Mahanga alikuwa anakabiliwa na hatari ya kutupwa jela kwa kuwa Msemakweli tayari alishalipa mahakamani Sh300,000 kwa ajili ya kumhudumia gerezani kama mfungwa wa madai kwa kushindwa kulipa deni hilo.

Hatahivyo, alinusurika baada ya kujitetea huku akieleza kuwa anakabiliwa na matatizo ndipo mahakama ikamwonea huruma na kuamua kumwachia kwa dhamana huku ikimtaka kulipa deni hilo lote lililobakia ifikapo Septemba 7.

Mdhamini wake, Dickson Biseko alisaini bondi ya dhamana ya Sh2 milioni, ili kwamba kama Mahanga hatafika mahakamani siku hiyo pamoja na kiasi hicho, basi yeye ndiye atakayekamatwa.

No comments:

Post a Comment

Popular