Jembe laTshishimbi latua usiku wa manane Dar es salaam - KULUNZI FIKRA

Friday 1 September 2017

Jembe laTshishimbi latua usiku wa manane Dar es salaam

 Yanga wanafanya mambo mawili kwa wakati mmoja.
Wanaendelea na Ligi na tayari wameanza usajili wa dirisha dogo. Unavyosoma hapa dakika hii tayari beki aliyeletwa na kiungo mpya wa Yanga, Papy Tshishimbi, yupo kwenye ardhi ya Dar es Salaam. Mchezaji huyo aliyekuja kwa majaribio,  ametua usiku wa kuamkia leo Ijumaa na  anaitwa Kayembe Kanku Fiston akitokea klabu ya SM Sanga Balende yenye makazi yake nje ya Jiji la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mchezaji huyo amepishana na kocha aliyetakiwa kumfanyia majaribio George Lwandamina ambaye imeelezwa kwamba amekwenda kwao kwa dharura baada ya kufiwa na baba yake mzazi na kwamba atarejea Bongo Jumapili.

Tshishimbi amewahakikishia Yanga kwamba mchezaji huyo ni fundi na wataona yake kwenye majaribio ambayo atayaanza baada ya kocha kurejea. Amewaambia viongozi kuwa akishirikiana na kina Kelvin Yondani, Yanga itakuwa imara sana nyuma.

Kuondoka kwa Lwandamina kutamfanya Fiston kuanza majaribio yake akiwa chini ya makocha watatu wasaidizi wa kikosi hicho; Shadrack Nsajigwa,Noel Mwandila na Juma Pondamali, lakini bado akisubiri kuthibitisha uwezo wake kwa Lwandamina ambaye usiku na mchana anaomba Novemba ifike dirisha dogo lifunguliwe asajili beki.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Fiston atajaribiwa kwa wiki mbili ambapo endapo uwezo wake utakubalika, atasaini mkataba wa awali na Yanga na kurejea klabuni kwake.

Imeelezwa kuwa atarejea tena nchini kuja kujiunga na mabingwa watetezi hao wa Ligi Kuu Bara wakati wa usajili wa dirisha dogo la usajili likalaofunguliwa Novemba.

Fiston anamaliza mkataba wake na Sanga Balende mwezi huu ambapo tayari Tshishimbi ameliambia Mwanaspoti kuwa beki huyo amezuia kuendelea na mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na klabu yake hiyo akisubiri kujua hatma yake na Yanga.

Yanga inamsaka mrithi wa Vincent Bossou aliyenyimwa mkataba mpya,  licha ya awali kuwajaribu mabeki watatu katika dirisha lililopita, ilishindwa kukubaliana na uwezo wao.

Hali hiyo ndiyo iliyowalazimisha mabosi wa Jangwani kiasi cha kumuuliza Tshishimbi endapo anamjua beki yeyote shoka anayefaa na ndio wakapewa jina la Fiston.

No comments:

Post a Comment

Popular