Balozi: Macho ya Dunia kwa sasa ni kwa Rais Magufuli - KULUNZI FIKRA

Tuesday 5 September 2017

Balozi: Macho ya Dunia kwa sasa ni kwa Rais Magufuli

BALOZI wa China nchini aliyemaliza muda wake, Lu Youging amesema macho ya dunia hivi sasa yanaelekezwa kwa Rais John Magufuli, kwa vile ni aghalabu sana kupata kiongozi wa aina yake Afrika na duniani; na ndiyo siri inayosababisha afuatiliwe kwa karibu.

Amesema endapo isingekuwa ni sababu za kidiplomasia, asingeondoka nchini na badala yake angeendelea kubakia katika ofisi yake ili kuhakikisha kuwa anashirikiana na Rais Magufuli katika kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda na kuipaisha kwenda katika uchumi wa kati.

Katika hatua nyingine, Balozi huyo ambaye ameiwakilisha nchi yake kwa miaka sita nchini, ameacha wosia akiishauri serikali na Watanzania, kuwatunza walimu kama lulu, kwa vile ni kupitia kwao nchi itapata maendeleo, akitoboa siri kuwa ni walimu ndiyo waliofikisha nchi ya China katika uchumi wa kwanza kutoka katika lindi la umasikini.

Pia ametaja vikwazo vitatu vinavyotia dosari maendeleo ya Tanzania kuwa ni tatizo la ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei unaotokana na ughali wa bei za bidhaa na ukubwa wa deni la Taifa, lakini akisema mikakati na mbinu za kiutawala za Rais Magufuli ndiyo suluhu.

Mwanadiplomasia huyo nyota na kipenzi cha Watanzania wengi, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wake mahususi wa kuwaaga wanahabari, uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wa Chama cha Urafiki wa Tanzania na China.

Balozi Lu atarejea China wiki ijayo ili kufanya majukumu mengine. Macho ya Dunia kwa Rais Magufuli Akizungumzia mtazamo wa dunia kwa Rais Magufuli, Balozi Lu alisema; “Ni aghalabu sana kupata Rais wa aina yake, si Afrika tu hata duniani.

Ni kiongozi aliyeishitua dunia kutokana na aina yake ya uongozi. “Ni Rais aliyechagua kuwa upande wa wananchi wanyonge. Utashi na akili yake yote ni katika kuboresha maisha ya watu wa chini ambao ni masikini. Dunia imeshikwa na mshangao.

“Anapigana na rushwa na ufisadi kwa nguvu kubwa sana, amefanya mambo makubwa kwenye elimu, kwenye afya, nishati na barabara, sasa tunashuhudia akiipeleka Tanzania kwenye mapinduzi ya viwanda kwa kasi. Naondoka na kuwasihi Watanzania muungeni mkono huyu Rais na manufaa yake mtayaona,” alisema.

Ni kutokana na namna Tanzania inavyoendeshwa sasa; Balozi huyo alishindwa kuficha hisia zake, alipozungumzia hatua ya kupangiwa majukumu mengine na kulazimika kurejea China, ambapo alisema; “Mimi binafsi sitaki kuondoka sasa, lakini kwa vile ni sababu za kidiplomasia ambapo mtu mwingine anapaswa kuja, sina jinsi inabidi niondoke.

“Hata hivyo mapenzi yangu kwa ardhi ya Tanzania, mapenzi yangu kwa watu wa Tanzania hayatabadilika kamwe. Mapenzi yangu ya kuiona Tanzania inafanya mapinduzi makubwa ya viwanda ili kufikia uchumi wa kati hayatabadilika. Nitamsaidia Rais Magufuli popote nitakapokuwepo ili kuona ndoto yake hii inatimia”.

Alitumia fursa hiyo pia kueleza namna viongozi wa Tanzania kuanzia Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere walivyopigania maendeleo ya nchi na kukuza ushirikiano wa kimataifa hususani urafiki na China, ambao alisema utadumu milele.

Balozi huyo alisema katika kipindi cha miaka sita ya kuwepo nchini, ameshuhudia Tanzania ikipiga hatua kubwa kimaendeleo; huku akitaja vyombo vya habari kuwa sehemu ya maendeleo hayo na kuviasa kuwa kina vinapotimiza wajibu wake, viitazame Tanzania na Watanzania kwanza.

“Katika Taifa lolote vyombo vya habari vina jukumu la kuwa sehemu ya kuchochea uchumi. Yapo maeneo wanasema ni mhimili wa nne na yapo wanasema ni mhimili wa tano, lakini kwa namna yoyote itakavyosemwa; vyombo vya habari ni mhimili muhimu katika ukuaji wa uchumi,” alisema Balozi huku akikiri kuwepo kwa uhuru wa habari.

Wosia kuhusu walimu Kuhusu nini nchi ifanye ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, Balozi huyo alisema ni lazima mtazamo wa serikali na Watanzania kuhusu walimu ubadilike, akisema ni lazima sasa walimu waanze kuangaliwa kama kundi namba moja na muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi.

Alisema siri kubwa iliyofanya China kupanda juu kiuchumi kwa kasi ni kutokana na kuwa na wataalamu wa kutosha, ambao alisema ili waweze kuzalishwa ni lazima wawepo walimu wa kutoa ujuzi huo ukiwemo uhandisi katika viwanda.

“China tuliamua kuwapa kipaumbele walimu, kwa vile uchumi ulikuwa wa chini tulifika mahali kama Taifa tukasema hata mishahara watalipwa walimu kwanza na makundi mengine yatasubiri. Tukaanzisha miradi pia ya kuboresha nyumba za walimu, shule, madarasa, madawati na hatimaye tukazalisha wataalamu wengi waliogeuka kuwa kichocheo cha uchumi.

“Ni lazima serikali na Watanzania wote wabadili mtazamo. Wote sasa wanatakiwa kuanza kutoa mchango wa hali na mali kwa maendeleo ya walimu na elimu. Ikibidi hata katika kila kodi mnayoiweka, kuwe na kiasi kidogo kwa ajili ya kuboresha elimu.

Mkifanikiwa katika elimu hakuna atakayewazuia katika ukuaji wa uchumi,” alisema. Alisifu Sera ya Elimu Bure, iliyoasisiwa na Rais Magufuli, lakini akasema pamoja na kuleta manufaa, imeibua pia changamoto kadhaa, zikiwemo za uhaba wa madarasa na madawati na kwamba sasa Watanzania wote washiriki kutatua changamoto hizo, ili lengo liweze kufikiwa kwa asilimia 100.

Alisema pia serikali inapaswa kutazama upya bajeti, inayoelekeza katika sekta ya elimu ili kutoa fedha za kutosha, kuanzisha Mifuko ya kusaidia kuboresha sekta ya elimu, jamii kujengewa utamaduni wa kuanza kutoa michango ya kielimu na kudhibiti rushwa na ufisadi katika sekta ya elimu.

Dosari katika mipango ya maendeleo Kutokana na mapenzi mema na Tanzania, Balozi Lu hakusita kueleza kasoro alizoziona kuwa zinakwamisha jitihada za kukuza uchumi ambapo alitaja deni la taifa, mfumuko wa bei na tatizo la ajira kuwa ni maeneo yanayopaswa kushughulikiwa kwa haraka.

Alizungumzia pia uhaba wa wataalamu na matumizi serikalini. Alisema pamoja na kukusanya kiwango kikubwa cha kodi, kudhibiti rushwa na ufisadi, lakini Tanzania inakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni, ambao unarudisha nyuma mbio za kukuza uchumi.

Alisema tatizo la ukosefu wa ajira ni eneo ambalo pia linakwamisha ukuaji wa kasi wa uchumi, lakini akasifu mpango wa uchumi wa viwanda kuwa suluhu ya kudumu ya tatizo hilo. Alisema kiwango cha ukosefu wa ajira, alichokishuhudia mijini na vijijini kinatisha.

Kuhusu mfumuko wa bei, Balozi huyo alisema ni lazima eneo hilo pia lifanyiwe kazi kwa haraka, kwa vile linaathiri ustawi wa wananchi na kwamba ughali wa bidhaa ni moja ya sababu inayosababisha tatizo hilo. Alisema ni lazima Tanzania ianze kuzalisha bidhaa za kutosheleza mahitaji ya nchi na kuuza nje ili kupata fedha za kigeni kuliko kuendelea kuagiza zaidi bidhaa kutoka nje.

No comments:

Post a Comment

Popular