Acacia: Tumeshapunguza wafanyakazi 12000 na wakandarasi 800 ili kupunguza gharama za uzalishaji - KULUNZI FIKRA

Tuesday 5 September 2017

Acacia: Tumeshapunguza wafanyakazi 12000 na wakandarasi 800 ili kupunguza gharama za uzalishaji

Kampuni ya Acacia imesema ina matumaini kuwa mazungumzo baina yake na Serikali kuhusu kuzuiwa kusafirisha mchanga wa madini nje, yatafikia suluhisho, lakini imetangaza kupunguza uchimbaji madini katika mgodi wake tegemeo wa Bulyanhulu.

Tangu kuzuiwa kusafirisha mchanga huo mwezi Machi, kampuni hiyo imekuwa ikilalamika kuwa inapoteza mapato, yapatayo dola 1 milioni za Kimarekani (zaidi ya Sh2.2 bilioni) kila siku na sasa hali inaonekana kuwa mbaya zaidi.

“Ikiwa sehemu ya mipango ya muda ya Acacia kwa mwaka 2017, tunatangaza kuwa tutahitaji kufikiria kupunguza shughuli za uendeshaji na matumizi katika mgodi wa Bulyanhulu kama zuio la makinikia halitaondolewa hadi mwishoni mwa robo ya tatu ya mwaka 2017,” inaeleza taarifa ya Acacia iliyowekwa katika tovuti yao jana.

Acacia imesema kuwa imepoteza dola 265 milioni (zaidi ya Sh583 bilioni) ambazo ni sawa na asilimia 35 ya mapato yake tangu mwezi Machi wakati Serikali ilipotangaza kuzuia usafirishaji wa mchanga huo ambao una mabaki ya madini, hasa dhahabu na shaba iliyoshindikana kuchenjuliwa mgodini.

Licha ya mapato hayo, Acacia imesema zuio hilo limeongeza gharama za uendeshaji kwa zaidi ya dola 15 milioni (zaidi ya Sh33 bilioni) kwa mwezi kwenye mgodi huo, hivyo kuufanya kutokuwa endelevu.

“Hivyo basi, Acacia imeanza programu ya kupunguza shughuli za uendeshaji na matumizi ili kulinda biashara yetu katika muda mrefu ujao,” inasema taarifa hiyo.

“Programu hii inahusisha utunzaji wa mali zote na mitambo ili kuiweka katika hali ya kuweza kurudia kufanya kazi iwapo zuio litaondolewa na mazingira ya uendeshaji kuimarika.”

Hata hivyo, Acacia imeonya kuwa upunguzaji huo wa shughuli za uendeshaji, pia utaathiri jamii.

“Ni jambo la kusikitisha kuwa utekelezaji wa programu hii utasababisha kupunguza nguvukazi kutoka wafanyakazi 1,200 waliopo sasa na majukumu 800 ya wakandarasi,” inasema taarifa hiyo.

Inasema inachukua hatua hizo ili kukabiliana na gharama, lakini ikiendeleza uhusiano wa kibiashara na wadau wake. Tangu mwaka huu uanze, inasema imetumia takriban dola 210 milioni (zaidi ya Sh462 bilioni).

Utekelezaji

Katika utekelezaji wa mpango huo, imesema itafanya majadiliano na wadau wake wa karibu ili kufanikisha lengo hilo. Kwa kuanza, itasitisha shughuli zote za chini ya ardhi na uchakataji wa mawe yenye madini utasitishwa baada ya majuma manne.

Ili kujikwamua na hali hiyo ngumu kiuchumi, Acacia imesema uchenjuaji magwangala, ambao ulisitishwa ili kulinda maji kutokana na ukame unaoendelea kaskazini mwa nchi, sasa unategemewa kuanza mwezi ujao kwa matumaini kuwa kutakuwa na mvua za kutosha na utafanyika kwa kiwango cha wakia 30,000 hadi 35,000 kwa mwaka za dhahabu, wakati shughuli za chini ya ardhi zikiwa zimesimamishwa.

Uamuzi huu utahitaji kutekelezwa kwa umakini hasa kwa kuzingatia msimamo alioutoa Rais John Magufuli mwishoni mwa Julai mwaka jana alipokuwa akiwahutubia wakazi wa mjini Geita na kuuagiza uongozi wa Geita Gold Mine kuwaachia wananchi magwangala na kuonya asitokee kigogo yeyote atakayejimilikisha.

Mchakato huo, Acacia inasema utakamilika ndani ya miezi mitatu ijayo huku ikilazimika kutumia dola 5 milioni (zaidi ya Sh11 bilioni) kila mwezi kabla haijafikia lengo la kutumia dola 3 milioni (zaidi ya Sh66 bilioni) gharama ambazo zitafidiwa na madini yatakayopatikana kwenye uchenjuaji wa magwangala.

Mbadala

Kwa muda wa zuio, mgodi wa Buzwagi ambao muda wake wa uzalishaji unakaribia kuisha kutokana na kuishiwa madini, utaendelea na uzalishaji kama kawaida. Mkakakti uliopo ni kuhakikisha unazalisha madini hayo bila mchanga.

Kutokana na kupungua kwa shughuli mgodi wa Bulyanhulu, makisio ya Acacia ya uzalishaji yatapungua kwa wakia 100,000 kutoka kati ya 850,000 mpaka 900,000 zilizokadiriwa awali. Matarajio hayo mapya yatachangiwa pia na kushuka kwa uzalishaji katika mgodi wa North Mara ambao vibali vya wakandarasi wa uchimbaji ardhini vimecheleweshwa.

Kutokana na mabadiliko hayo, Acacia inasema haitaweza kuziba pengo la dhahabu na shaba iliyomo kwenye makinikia, hivyo italazimika kuuza madini yote inayochimba badala ya asilimia 35 ya uzalishaji wote kama ilivyokuwa inafanya awali.

Kampuni hiyo ya uchimbaji madini imesema inatumaini mazungumzo yanayoendelea kati ya Serikali na Barrick Gold, kampuni ambayo ni mwanahisa mkuu wa Acacia, yatatao suluhisho zuri kwa pande zote mbili.

Na, baada ya kukamilisha mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika Bulyanhulu, Acacia inaamini itarejea kwenye ufanisi wake mwanzoni mwa mwaka ujao kwa kuwa ni mwishoni mwa mwezi uliopita ilikuwa na fedha taslimu dola 107 milioni (zaidi ya Sh235.4 bilioni) wakati madeni yake ni yalikuwa dola 71 milioni (zaidi ya Sh156.2 bilioni).

Acacia

Tangu kuanzishwa kwake, takriban miongo miwili iliyopita Acacia inasema imewekeza zaidi ya Sh8.8 trilioni kuendeleza migodi mitatu inayoimiliki huku ikitumia zaidi ya Sh3 bilioni kufanikisha shughuli mbalimbali za kibiashara. Inasema imewekeza zaidi ya Sh165 bilioni kwenye miradi ya jamii inayozunguka migodi hiyo na imelipa kodi na mrabaha wa zaidi ya Sh2.2 trilioni.

Kwa miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, inasema imelipa kodi na mrabaha wa Sh117 bilioni na kuanzisha miradi iliyowanufaisha zaidi ya wananchi 40,000 wanaozunguka migodi yake. Inabainisha kwamba zaidi ya wakandarasi na wafanyakazi 5,000 wanafanya nayo kazi mbalimbali hivyo kuchangia asilimia 1.6 ya Pato la Taifa (GDP).

No comments:

Post a Comment

Popular