Mambo yatakayo amua kesi ya uchaguzi wa Urais mahakama kuu Kenya - KULUNZI FIKRA

Saturday 26 August 2017

Mambo yatakayo amua kesi ya uchaguzi wa Urais mahakama kuu Kenya

 
USAHIHI wa fomu zilizotumika katika kuandaa matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Kenya itakuwa ni kiini cha mabishano katika Mahakama Kuu wakati shauri la Raila Odinga dhidi ya kuchaguliwa kwa Rais Uhuru Kenyatta litakapoanza kusikilizwa.

Wakati mahakama ikiingia ngwe ya pili ya mpambano huo juu ya matokeo ya uchaguzi wa rais leo jioni, swali juu ya iwapo mapungufu yaliyoonyeshwa katika fomu za taarifa yatatosha kubadili matokeo ya uchaguzi huo.

Mfumo wa kompyuta za IEBC

Pia kuna swali iwapo Rais Uhuru Kenyatta alitumia madaraka yake vibaya kuamua matokeo ya uchaguzi huo na iwapo tume ya uchaguzi na mipaka ya nchi hiyo inapaswa kukabidhi zaidi ya vifaa 40,883 vilivyotumika kuwatambua wapiga kura na kutuma matokeo.

Sehemu ya kwanza ya shauri hilo ilimalizika siku ya Ijumaa jioni, huku pande zote tatu katika mgogoro huo zikiwasilisha maelezo kwa maandishi – Raila Odinga, Rais Uhuru Kenyatta na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

Sabato
Sehemu ya pili inatarajiwa kuanza saa moja jioni leo wakati shauri la awali litakaposikilizwa.

Shughuli za mahakama zitachelewa kuanza kwa sababu Jaji Mkuu David Maraga, muumini wa madhehebu ya kisabato, atakuwa anaheshimu siku hiyo.

Katika shauri la awali, majaji wataamua ni masuala gani yanapaswa kufanyiwa maamuzi, nani mwingine anapaswa kuingia katika kesi hiyo na nini kinapaswa kufanywa na tume juu ya vifaa vya uchaguzi.

Tume tayari imekwishaweka fomu zote za 34A, 34B na 34C, lakini timu ya Raila Odinga inataka vifaa vyote pamoja na mfumo wa kompyuta kuwasilishwa kwa ajili ya uchunguzi.

Wizi
Pande zote zimeonyesha kujiamini kwamba zitaweza kuwashawishi majaji saba wa Mahakama Kuu ili kufanya uamuzi mzuri kwa upande wao.

Nasa, kupitia kwa mwanasheria wake James Orengo, ilisema iko tayari kuonyesha “uchafu na wizi wa kutisha” uliofanywa na tume ya uchaguzi katika uchaguzi wa Agosti 8 mwaka huu, huku Jubilee kupitia kwa Ahmednasir Abdullahi ilisema wako tayari kusambaratisha ushahidi wowote utakaowasilishwa na wapinzani wao.

Baada ya kuwasilisha maelezo yao Ijumaa, timu ya kisheria ya Odinga ilisema kwamba iligundua kwamba uwasilishaji mzima wa matokeo uliharibiwa ili kumpa Rais Kenyatta nafasi nzuri ya kushinda.

Mfumo wa Taarifa
Odinga amesisitiza katika maelezo yake kwamba kuna tofauti kubwa kati ya matokeo yaliyopo katika fomu na yale yaliyotolewa na tume kwa njia ya mtandao wa kompyuta.

Anadai kwamba ameona fomu zote za 34A ambazo zilipelekwa kwake kutoka katika maeneo mbalimbali ya uchaguzi na mawakala wa chama chake na kuthibitishwa kwamba kuna tofauti kubwa ya matokeo katika fomu za 34B na yale yaliyowekwa katika mtandao wa tume ya uchaguzi.

Pia Odinga amerudia madai yake kwamba mfumo wa kielekroniki wa tume uliharibiwa kwa maksudi uli kubadili matokeo.

Anasema kwamba tofauti hizo sio za bahati mbaya, bali zilipangwa.

Kupitia hati ya kiapo ya Omar Yusuph Mohamed, Odinga anasema atadhihirisha namna tume iliruhusu kuharibiwa au kuingiliwa kwa mfumo wake wa taarifa ili kutengeneza matokeo.

Majumuisho ya kura

“Tayari nimesoma hii hati ya kiapo juu ya namna ambavyo tume ilivyoruhusu mifumo yake ya kielektroniki kuharibiwa ili kuzidisha idadi ya kura zilizokataliwa katika njia ambayo itaathiri idadi ya kura zangu na zile za Uhuru Muigai Kenyatta,” Odinga alisema katika maelezo.

Waziri huyo mkuu wa zamani wa Kenya anasema kwamba uchambuzi wa timu yake uligundua kwamba matokeo yaliyokuwa yanarushwa kwa njia ya televisheni katika kituo kikuu cha majumuisho ya kura hayakuwa matokeo yaliyokuwa yanahesabiwa, kujumuishwa, kuthibitishwa, na kuwasilishwa kutoka vituo vya majumuisho ya kura kutoka nchi nzima.

Anasisitiza kwamba matokeo yalitengenezwa na kompyuta.

Anaongeza kuwa uchaguzi uliandaliwa kwa kumpendelea Rais Uhuru Kenyatta, hivyo kukiuka matakwa ya wananchi wa Kenya.

Mapungufu
Wakati wa shauri la awali, wanasheria wa Odinga wanatarajiwa kuiomba mahakama kuitaka tume ya uchaguzi kuwasilisha au kuruhusu mifumo yake ya kompyuta iliyotumika wakati wa uchaguzi, mifumo ya ulinzi wa kompyuta na teknolojia zote zilizotumika kufanyiwa uchunguzi.

Kwa upande mwingine, wanasheria wa upande wa tume ya uchaguzi wanatarajiwa kuitaka mahakama iitake Nasa kuthibitisha madai yao juu ya fomu za uchaguzi.

Tume hiyo pia inasema kwamba taarifa ambazo ziliingizwa katika vifaa vya kutuma matokeo ya awali zilikuwa ni takwimu na sio matokeo halisi.

Tume inasema katika majibu yake kwa madai ya Nasa kwamba kama kulikuwa na mapungufu yoyote katika uchaguzi wa urais, mapungufu hayo hayakuwa yanatosha kubadili matokeo ya mwisho ya uchaguzi.

Ushahidi
Kutoka kwenye majibu yake, tume inaona madai ya Nasa kama yasiyojitisheleza na ya ujumla, hivyo kushindwa kufikia kiwango kinachotakiwa kisheria.

Wakati Nasa ikidai kwamba uchaguzi wa Urais uliendeshwa vibaya na uliogubikwa na mapungufu mengi ambayo hayajali nani alitangazwa kuwa mshindi, tume inadai kwamba madai hayo hayana ushahidi wowote.

Tume imeonyesha kwamba itawataka majaji saba watakaokuwa wanasikiliza shauri hilo kuitaka Nasa kuthibitisha madai yake kwamba idadi ya fomu za 34B hazikuonyesha majina ya wasimamizi wa uchaguzi na kwamba hazikuwa na muhuri ya tume ya uchaguzi.

Madai ya Nasa
Pia inataka timu ya Odinga kutakiwa kutoa ushahidi kwamba idadi kubwa ya fomu za 34A na 34B hazikuwa na sahihi za mawakala wala sababu hazikuwekwa ni kwa nini walikataa kusaini fomu hizo.

“Kwa vyovyote vile, kukataa kwa mawakala kusaini fomu hizo hakubadilishi matokeo yaliyotangazwa,” tume inasema.

Nasa pia inapaswa kuthibitisha kwamba mtu mmoja alikuwa anasimamia vituo vingi vya upigia kura katika maeneo tofauti.

Tume inaeleza kwamba utaratibu uliotumika baada ya kuhesabu kura katika kila kituo kati ya vituo hivyo 40,883 vya kupiga kura, uliendana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba matokeo yaliyotangazwa katika jimbo la uchaguzi yalikuwa ni ya mwisho.




No comments:

Post a Comment

Popular