Madudu uwanja wa ndege Dar es salaam yaishitua kamati ya bunge PAC,yaagiza ukaguzi maalum wa CAG - KULUNZI FIKRA

Wednesday 30 August 2017

Madudu uwanja wa ndege Dar es salaam yaishitua kamati ya bunge PAC,yaagiza ukaguzi maalum wa CAG

 Kamati ya bunge ya PAC imetoa maagizo kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) baada ya Mkurugenzi wake Salim Msangi kuwasilisha taarifa ya kifedha ikiwa na mapungufu makubwa ya kisheria na kukosa viwango vya kimataifa.Taarifa hiyo inayoonekana kuwa na mapungufu mengi na dalili za "kupikwa" zimewashitua wabunge na hivyo kuamuru uchunguzi na ukaguzi maalumu kufanywa katika mamlaka hiyo.

Kamati hiyo pia imetoa malalamiko kwa uongozi wa TAA kwa kuzembea kuboresha uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere Dsm,ambapo wabunge wamehoji uchakavu wa jengo,joto sehemu ya abiria na hali ya paa kuvuja.Hali hii imeonekana kuitia aibu serikali na kuleta aibu kwa Taifa,kwani eneo la kiwanja popote duniani huonekana kama taswira ya nchi.

Jambo jingine lililoibua mjadala kwenye kamati ya PAC ni UBINAFSISHAJI wa Kampuni ya Maendeleo ya Kiwanja cha Ndege Kilimanjaro (KADCO), umehojiwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa umegubikwa na utata, hali ambayo baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wametaka wapewe maelezo ya serikali, vinginevyo suala hilo litahamishiwa bungeni lijadiliwe.

Hayo yalibainika jana katika kikao kati ya wajumbe wa PAC na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Miongoni mwa mambo ambayo wajumbe walisema yana utata, ni pamoja na CAG kubaini kuwa licha ya serikali kuwa na hisa asilimia 100 katika Kadco, kampuni hiyo imeendelea kuachiwa kuendesha Kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro (KIA).

 Utata mwingine ni hatua ya KIA kuendeshwa tofauti na viwanja vingine, kwa maana ya kuwa chini ya kampuni hiyo wakati viwanja vya ndege vingine vyote viko chini ya TAA. "Kwa nini hiki kiendeshwe tofauti na viwanja vingine?

Na TAA wanaendesha viwanja vingine na siyo KIA... Tutamuita waziri atueleze kuna nini," alisema mwenyekiti wa kamati, Naghenjwa Kaboyoka ambaye ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema).

Kwa upande wake, Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM) alisema: "Tuwe wazi kuwa huko serikalini kuna watu wanaendesha Kadco wanamaintain status quo kwa sababu wanapata fedha.

Kama Baraza la Mawaziri halitakuwa wazi katika hili, tutawasha moto bungeni.” “Kwa nini hawa TAA wawe na share(hisa) na Kadco wakati hawana mamlaka?” alisema mbunge huyo akirejea maelezo ya Mkurugenzi wa TAA katika kikao hicho aliyesema kuwa suala la Kadco haliwahusu ingawa wana hisa.

 Awali, Mwenyekitiwa Bodi ya TAA, Profesa Ninatubu Lema alipoulizwa na wajumbe wa kamati kuhusu masuala kadhaa ya Kadco, alisema kampuni hiyo iko nje ya mamlaka ya TAA kwa kuwa inaripoti moja kwa moja kwa serikali.

 Miongoni mwa maswali kuhusu Kadco yaliyoulizwa na Kakunda na kufanya wajumbe wengi kuchangia, ni uhusiano wa TAA na kampuni hiyo kama kama wana mkataba wowote. Pia alitaka kufahamu kama kampuni hiyo, imerithiwa na serikali au imeanzishwa upya.
    

No comments:

Post a Comment

Popular