Kagera: Askari wa kitengo cha Intelijensia aliyetoweka kwa siku tatu apatikana akiwa amefariki. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 30 August 2017

Kagera: Askari wa kitengo cha Intelijensia aliyetoweka kwa siku tatu apatikana akiwa amefariki.

 
 Askari polisi wa Kituo cha Kati mjini Bukoba, NSO 1114 Koplo Mussa Msanya (44) amekutwa amekufa na mwili wake kuelea ufukweni mwa Ziwa Victoria katika eneo la Kiroyera.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Augustine Ollomi, alisema Agosti 26, mwaka huu, saa sita mchana, mke wa marehemu aitwaye Halima Mussa alifika kituoni hapo na kutoa taarifa za wasiwasi juu ya hali ya mume wake, kwa kuwa alipoamka alikuta karatasi iliyoandikwa namba ya siri ya sanduku dogo (ngwira), ambalo marehemu alikuwa akitunzia nyaraka zake muhimu.

"Baada ya kuchukua kikaratasi hicho, Halima alifungua sanduku hilo na kukuta namba za siri ya akaunti ya benki na kadi ya kutolea fedha pamoja na simu mbili za mkononi lakini hakukuwa na ujumbe mwingine wowote.

"Hali hiyo ilimpa wasiwasi mke huyo, kwani marehemu aliondoka nyumbani kwake akiwa amevalia sare za polisi, hivyo alifikiri yuko kazini", alisema.

Alisema baada ya taarifa hiyo, polisi waliendelea kufanya uchunguzi, ambapo Agosti 28, saa 10.45 jioni walipata taarifa kutoka kwa wafanyabiashara wauza samaki katika eneo hilo, kuwa waliona mwili wa mtu uliokuwa amevaa nguo za polisi ukielea kando mwa Ziwa Victoria, ambapo walishirikiana na kuuopoa, kisha polisi walifika na kuuchukua, kuupeleka hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kagera.

Kwa mujibu wa Kamanda Ollomi, askari huyo alitumikia polisi kwa miaka 18 hadi mauti yalipomkuta na kwamba chanzo cha kifo chake bado hakijajulikana.

Ollomi alisema uchunguzi wa awali mwili wa marehemu unaonyesha haukukutwa na kovu lolote, mbali na kuvimba, hatua inayohisiwa kuwa huenda ilitokana na kifo cha maji.

Alisema wanategemea pindi watakapopata taarifa za daktari, wanaweza kujua chanzo cha kifo hicho, huku akisema uchunguzi unaendelea na kwamba utakapokamilika polisi itatoa taarifa. Na mwili kukabidhiwa kwa ndugu tayari kusafilishwa kwenda mkoani Kigoma kwa mazishi.

No comments:

Post a Comment

Popular