Chadema yasikitishwa na uvamizi wa ofisi ya mawakili - KULUNZI FIKRA

Saturday 26 August 2017

Chadema yasikitishwa na uvamizi wa ofisi ya mawakili

 

           TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa masikitiko taarifa za kuvamiwa kwa ofisi za Kampuni ya Mawakili wa Kujitegemea ya IMMMA ya Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo.

CHADEMA inafahamu kuwa kwa mujibu wa Mikataba ya Kimataifa Mawakili wana haki ya kufanya kazi zao kwa uhuru na faragha wakati wa kutoa huduma zao kwa wateja wao na wananchi kwa ujumla. Ikumbukwe pia kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mawakili (The Advocates Act) Mawakili ni Maafisa wa Mahakama ambao huisaidia Mahakama katika kutenda haki. Kwetu CHADEMA tunaona kuwa hili ni shambulio dhidi ya Mahakama kwani maafisa wake wameshambuliwa.

Kwa hiyo uvamizi wa ofisi za Mawakili unalenga kukiuka misingi ya ya Sheria na Mikataba ya Kimataifa inayolinda haki za Mawakili . Chama kinapenda kutoa rai kwa vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kutoa taarifa kwa umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wahusika wanapelekwa kwenye vyombo vya Sheria ili Sheria zichukue mkondo wake.

Aidha kitendo hiki kimefanywa na watu waoga wanaodhani kuwa kwa kufanya hivyo kutawafanya Mawakili wawe na hofu nchini na washindwe kutimiza wajibu wao, hivyo basi CHADEMA kinawatia moyo Mawakili wote nchini wasikubali kuingia hofu wala woga kutokana na tukio hili bali waendelee kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria.

Mwisho tunapenda kutoa pole za dhati kabisa kwa Kampuni ya Mawakili ya IMMMA pamoja na wafanyakazi wote kutokana na madhara ya tukio hili baya, sisi kama Chama tuko nao pamoja katika kipindi hiki kigumu.

Imetolewa na;

John Mrema

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje.

26 Agosti, 2017

No comments:

Post a Comment

Popular