Asilimia 30 ya wabunge wa Bunge la Tanzania hawajulikani walisoma wapi au wana taaluma gani - KULUNZI FIKRA

Thursday 24 August 2017

Asilimia 30 ya wabunge wa Bunge la Tanzania hawajulikani walisoma wapi au wana taaluma gani

ASILIMIA 30 ya wabunge wa Bunge la Tanzania hawajulikani walisoma wapi au wana taaluma gani; huku ikijulikana rasmi kwamba angalau wabunge 16 wana elimu ya shule ya msingi, utafiti wa Raia Mwema umebainisha.

Bunge lina tovuti yake rasmi, www.parliament.co.tz, ambako wasifu wa kuzaliwa na kielimu wa wabunge wote huwekwa baada ya kuwasilishwa kwao na wabunge wenyewe.

Hata hivyo, hadi kufikia juzi Jumatatu, kuna wabunge; wapya na wa zamani, ambao hadi sasa hawajatoa taarifa zao kamili – ikiwamo hata tarehe ya kuzaliwa kwao na wapi walizaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo rasmi za Bunge, takribani wabunge 119, hawajawasilisha taarifa zao kamili bungeni na hivyo hadi sasa hazijawekwa, na sababu za kutofanya hivyo hazijawekwa wazi.

Mmoja wa maofisa wa juu wa Bunge aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina yake, alisema wabunge wote wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao kwa ajili ya kuwekwa kwenye tovuti hiyo lakini wengine wameamua; kwa sababu zao wenyewe, kutoweka taarifa zao hizo hadharani.

Katika wabunge hao 119, wengine hawajatoa taarifa yoyote kuhusu kuanzia kuzaliwa kwao, wengine wameandika walipozaliwa lakini hawajasema waliposoma, wengine wamesema waliposoma lakini hawasemi walisomea kitu gani.

“Wabunge wote wanatakiwa kuleta taarifa zao kwa ajili ya sisi kuziweka kwenye tovuti. Lakini hawalazimishwi kisheria kutuletea wasifu huo. Kama hujaona wasifu wa mbunge, maana yake ni kwamba wasifu huo haujatumwa kwetu,” alisema kigogo huyo wa Bunge.

Hali ya kitaaluma ikoje bungeni?

Katika mahojiano ambayo Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliwahi kufanya na Raia Mwema mapema mwaka huu, alieleza kuhusu changamoto ya kielimu ndani ya taasisi hiyo ambayo kwa sasa sifa ya mbunge ni kujua kusoma na kuandika.

Ndugai alisema suala hilo linaweza kujadiliwa na kuongeza sifa zaidi ili kuwafanya waweze kumudu vema majukumu ya kuisimamia serikali, ingawa Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa, alitoa maoni kwamba Bunge linatakiwa kuakisi hali ilivyo kitaifa na halitakiwi kuwa la wasomi au matajiri tu.

Taarifa rasmi za kwenye tovuti hiyo zinaonyesha kwamba taaluma inayoongoza kwa kuwa na wabunge wengi ni walimu ambao idadi yao imefikia 43 ikifuatiwa kwa karibu na taaluma ya masomo ya biashara (Commerce) ambayo ina wabunge 41. Taasisi hiyo pia ina wabunge 31 waliosoma masomo ya sheria kwa viwango mbalimbali.

Hata hivyo, idadi hii inaweza isiwe rasmi sana kwa sababu kuna uwezekano miongoni mwa wabunge ambao hawajaleta taarifa zao, wana mojawapo ya taaluma hizi ambazo zimetajwa.

Miongoni mwa wabunge maarufu ambao taarifa zao za kitaaluma hazipo katika tovuti hiyo ya Bunge ni Freeman Mbowe, Abdallah Bulembo, Godbless Lema, Mussa Azzan Zungu, John Mnyika, Ahmed Shabiby, Livingstone Lusinde, Martha Mlata na wengine.

Tovuti hiyo inaonyesha kwamba Bunge sasa lina jumla ya wabunge 22 wenye elimu ya kiwango cha shahada tatu (uzamivu); kiwango kinachoelezwa kuwa cha juu katika historia ya Bunge hilo.

Baadhi ya wabunge mashuhuri wenye shahada ya uzamivu ni pamoja na Dk. Harrison Mwakyembe, Profesa Sospeter Muhongo, Profesa Palamagamba Kabudi, Dk. Philip Mpango, Dk. Joyce Ndalichako, Dk. Augustine Mahiga na Dk. Ashantu Kijaji.

Hata hivyo, Raia Mwema limebaini majina ya wasomi wabobezi wa kiwango cha PhD waliopo ndani ya Bunge lakini hawajulikani sana kama wanavyojulikana waliotajwa hapo juu.

Kwa mfano, kuna mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Dk. Immaculate Semesi, ambaye ni mbobezi katika sayansi ya maji; akiwa amefanya tafiti mbalimbali za kisayansi zenye kiwango cha kimataifa katika eneo hilo.

Kuna majina yasiyo maarufu sana kama ya akina Dk. Oran Njeza (Mbeya Vijijini), Dk. Pudensiana Kikwembe (Kavuu), Profesa Norman Sigalla (Makete), Dk. Ali Yusuf Selemani (Mgogoni), Dk. Japhet Hasunga (Vwawa) na wengine.

Wabunge 16 ambao tovuti ya Bunge imethibitisha rasmi kwamba wana kiwango cha elimu ya msingi ni Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku (Msukuma) ambaye ameandika alipata elimu yake hiyo katika Shule ya Msingi Fulwe, Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani (Profesa Maji Marefu) aliyesoma katika Shule ya Msingi Kwamndolwa na mwenzake wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda.

Wabunge wengine ambao tovuti ya Bunge imeonyesha kwamba wana elimu ya msingi ni Mbunge wa Rungwe (CCM), Saul Amon (S.H Amon), Aziz Abood, Suzane Kiwanga, Mbunge wa Makambako (CCM), Deo Sanga (Jah People), Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba, Mbunge wa Chaani, Khamis Yahya Machano, Mbunge wa Makunduchi (CCM), Haji Ameir Haji na Mbunge wa Paje (CCM), Jaffar Sanya Jussa.

Wengine ni Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mwantumu Dau, Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara (Bwege), Mbunge wa Nyang’wale (CCM), Hussein Nassor Amar na Mbunge wa Kilosa (CCM), Mbaraka Bawaziri.

Taarifa hizi zinatoa maelezo mawili kuhusu Bunge ambayo sasa hayana shaka. Mosi kwamba asilimia kubwa ya wabunge ambao ni wafanyabiashara wakubwa, hawana kiwango kikubwa cha elimu.

Wabunge matajiri kama vile Abood anayemiliki makampuni kadhaa na vyombo vya usafiri, Kishimba anayefahamika kwa kumiliki maduka makubwa ya bidhaa na Amon ambaye maduka yake ya S.H Amon yako karibu katika miji mbalimbali hapa nchini, wana elimu ya msingi tu.

Pia, wabunge wengi wa Bunge la Tanzania wenye asili ya kiasia, pia hawana kiwango kikubwa cha elimu ya darasani. Baadhi ya wabunge hao ambao kiwango chao cha elimu hakijavuka kidato cha nne ni Mbunge wa Mvomero, Suleiman Murrad, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, Mansoor Hirani, Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Khadija Qassm na Mbunge wa Mpendae (CCM), Salim Turky.

Pia, kwa kulinganisha, wabunge wa Viti Maalumu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanaonekana kuwa na elimu kubwa zaidi kulinganisha na wale wa vyama vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).

Kwa wastani, mbunge wa Viti Maalumu kwa Chadema ana kiwango cha elimu cha shahada moja wakati kwa CCM na CUF kiwango ni sekondari.
                        

No comments:

Post a Comment

Popular