Uvccm yatangaza vita dhidi ya wakurugenzi wa halmashauri zisizo toa asilimia 5 za vijana - KULUNZI FIKRA

Monday, 24 July 2017

Uvccm yatangaza vita dhidi ya wakurugenzi wa halmashauri zisizo toa asilimia 5 za vijana


Umoja Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa umetangaza kiama dhidi ya Halmashauri zote nchini zisizotoa asilimia 5 ya mikopo kwa Vijana kama ilivyoainishwa na Ilani ya Ushindi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Umoja huo umesema kuwa hakuna Taifa lolote Duniani ambalo linaweza kuajiri Vijana wote badala yake Vijana husaidiwa na Serikali kupitia mbinu Mbalimbali za kuwakwamua kiuchumi ikiwemo kuwapatia mikopo na kuwasaidia kujiajiri.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka (MNEC) Leo Julai 24, 2017 Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza Wakati wa ziara ya siku moja alipokuwa akizungumza na Vijana wa Jumuiya ya Chama hicho (UVCCM) pamoja na  wanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano wa ndani uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Shaka alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinafahamu kuwa Changamoto kubwa ya Vijana nchini ni ukosefu wa ajira lakini Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi inaendelea kutumia njia Mbalimbali ikiwemo kuwashauri Vijana Kujiunga na vikundi Mbalimbali ili wapatiwe mikopo waweze kujiajiri wenyewe.

"Nitakuwa muongo kama nitasema sifahamu changamoto zinazowakabili Vijana wengi kiuchumi kwa wale waliopo ndani ya Chama Cha Mapinduzi ama wale waliopo nje ya CCM lakini Serikali inayotekeleza ilani yetu ya ushindi ya Mwaka  2015 imeeleza vyema namna bora ya kuwasaidia Vijana kujiajiri" Alisema Shaka

Alisema kuwa Vijana na watanzania kwa ujumla wake wanapaswa kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli za kuwaletea maendeleo huku akisifu Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kuanza vyema kuwapatia mikopp Vijana wa Manispaa hiyo.

Alisisitiza kuwa Vijana wanapaswa kuanzisha vikundi vya ujasiriamali, na Vikundi vya uzalishaji Mali, Vitakavyowasaidia wao Vijana, Wanawake na Taifa kwa ujumla kupambana na hali ya kiuchumi katika jamii.

Shaka amewasihi Vijana kurudisha haraka fedha za mikopo pindi wamalizapo matumizi ya fedha hizo ili ziweze kuwasaidia Vijana wengine, zaidi amewasihi Vijana wote kuwa wabunifu kwenye kipato ili waweze kuishawishi Serikali kuwaongeza fedha nyingi katika miradi yao.

Sambamba na hayo pia Shaka amesifu Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela,  sambamba na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kazi kubwa ya kuwashirikisha Vijana katika shughuli za maendeleo wanazozifanya.

No comments:

Post a Comment

Popular