Hoja ya watu wasiojulikana yaibua mvutano Bungeni. - KULUNZI FIKRA

Thursday 3 May 2018

Hoja ya watu wasiojulikana yaibua mvutano Bungeni.

 
Matukio ya utekaji  na kupotea kwa watu yameibua mvutano baina ya wabunge, bungeni leo katika kikao cha kumi na moja cha Bunge Jijini Dodoma.

 Mvutano huo ulianza wakati mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Mhe Almas Maige akichangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya mwaka 2018/19 ya Sh945.5 bilioni.

Katika mchango wake, Mhe Maige amegusia suala la matukio ya watu wasiojulikana akisema;

“Watu wasiojulikana hawa wanaosemwa na wenzetu wa upinzani na huenda watu wasiojulikana wanasema wanafanya kazi upande wa upinzani tu hapana. Mimi nina orodha ya wana CCM waliofanyiwa na watu wasiojulikana.”

Kauli hiyo haikupita hivi hivi, kwani mbunge wa Ukonga (Chadema),  Mhe Mwita Waitara alisimama kumpa taarifa  Mhe Maige akisema idadi ya watu waliotendewa uhalifu na watu wasiojulikana ni wengi, “Kuna utekaji, uonevu katika nchi hii.”

Mwenyekiti wa Bunge, Mhe Najma Giga akamuuliza  Mhe Maige, “Unapokea taarifa hiyo ya mhe Waitara.”

Kabla hajajibu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt  Mwigulu Nchemba akasimama na kusema jeshi la polisi halijateka watu; “Mhe  Maige anaongelea watu wasiojulikana.”

Hoja haikuishia hapo, Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), Mhe James Mbatia naye akasimama na kusema, “Suala la uhalifu, halilinganishwi kwa vyama vya siasa, sisi sote ni Watanzania na jeshi la polisi linalinda usalama wa raia wote.”

Hapo ndipo  Mhe Maige akapewa fursa na Mwenyekiti  Mhe Giga kuendelea kuchangia akisema;

"Mimi siongelei uhalifu, naongelea watu kufanya matukio na hawakamatwi. Mimi nasema watu wanaofanya matukio wakamatwe.”amesema Mhe Maige.

Bado mvutano uliendelea kwani, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mhe  Kunti Yusuph akasimama kumpa taarifa  Mhe Maige kwa kusema;

 “Suala la kusema matukio yaliyofanyika upande wa upinzani na CCM hayafanani, inadhihirisha kwamba Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake imebariki mfumo na matukio haya ili waje waseme Chadema ni wachache na CCM ni wengi. Asante amedhihirisha.” amesema Mhe Yusuph.

Akihitimisha mchango wake kwa eneo hilo, Mhe Maige amesema, “Mimi nashangaa upande ule (wa upinzani) wanakurupuka, mimi naongelea ombi langu kwa Serikali ili kuweza kuwakamata watu wasojulikana.”

No comments:

Post a Comment

Popular