Msigwa atoa sababu za kumsifia Rais Magufuli. - KULUNZI FIKRA

Thursday 3 May 2018

Msigwa atoa sababu za kumsifia Rais Magufuli.

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amemsifu Rais John Magufuli kwa kupeleka fedha za maendeleo katika halmashauri yake bila ya kubagua, lakini amesema video iliyosambaa mitandaoni haitoi picha halisi ya alichosema.

Video hiyo fupi inamuonyesha Mchungaji Msigwa akizungumza kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika Ikulu ya Iringa juzi na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wa kisiasa na kidini.

“Na Mhe  Rais umekuwa ukisisitiza kwenye hotuba zako kwamba wewe hujali vyama na hili limedhihirika kwa kweli kwamba hujali vyama,” anasema Mchungaji Msigwa katika video hiyo huku waalikwa wakimpigia makofi.

“Umesaidia sana. Bahati mbaya hawakukupangia ratiba ya kufungua miradi. Hela za kutoka kwako zimekuja nyingi. Amezungumza Mhe (Waziri wa Mambo ya Nje, Augustine) Mahiga, tuna barabara nzuri", amesema Mchungaji Msigwa katika video hiyo.

“Katika kipindi chako ambacho umekuwa Rais tumejenga barabara ya lami ya mradi wa World Bank kutoka Mlandege mpaka kwa mkuu wa wilaya, karibu Sh3.5 bilioni, tuna stendi nzuri iko hapo chini Ipogolo, karibu Sh3 bilioni. Tuna maji. Kwa hiyo kuna vitu vimefanyika", amesema Mchungaji Msigwa katika video hiyo.

“Kwa kweli Mhe Rais hupendelei, hata sisi wa Chadema unaleta hela. Kwa hiyo wewe hujali vyama. Unaleta hela. Kwa hiyo wewe huwa hujali vyama hilo nikupongeze sana.”amesema Mchungaji Msigwa katika video hiyo.

Wakati Mchungaji Msigwa  akisema hayo, picha zinaonyesha waalikwa wakiangua vicheko na sauti zao zinasikika wakati akihitimisha hotuba yake.

Mchungaji Msigwa ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Serikali ya Awamu ya Tano na alipotafutwa kuelezea kwa kirefu alichokizungumza alisema, “Wamechukua kipande kidogo ambacho nilisema hela zimeletwa Manispaa ya Iringa, lakini wameacha kipande kikubwa ambacho nilizungumza kwamba hata kama madiwani wameondoka, Manispaa ya Iringa imekuwa nzuri, imekuwa bora,” alisema jana.

“(Wanachama wa Chadema na Ukawa) Wasione kama kuna mtu hapa ameyumba au nimesalimu amri. Mapambano bado yanaendelea, hiyo ndiyo hoja", alisema Mchungaji Msigwa.

Kuhusu alichokizungumza, Mchungaji Msigwa alisema kauli yake ilimaanisha kuwa Manispaa ya Iringa imekuwa bora katika kipindi hiki ambacho imekuwa chini ya Chadema kwa kuwa Rais amekuwa akipeleka fedha bila ya kujali vyama, lakini akashangaa kwamba ratiba yake mkoani Iringa haikujumuisha kutembelea miradi mikubwa kama barabara, machinjio kubwa kuliko zote Tanzania, stendi na mambo mengine.

“Kuna miradi mingi imefanyika chini ya uongozi wetu ambayo haihusiani na uwepo wa CCM ambao wapo katika manispaa hii na kumekuwa na dhana kuwa watu wakiwa Chadema au kiongozi akiwa Chadema, hakuna maendeleo na ndio maana madiwani wamekuwa wakihama,” alisema Mchungaji Msigwa.

“Kwa mfano, tuna barabara ambayo imejengwa kwa Sh3.5 bilioni na ambayo haikuwapo. Tumejenga katika kipindi hiki ambacho manispaa inaongozwa na Chadema",alisema Mchungaji Msigwa.

Pia  Mchungaji Msigwa alisema kuna machinjio ambayo itakuwa kubwa kuliko zote katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, pamoja na stendi ya mabasi iliyokamilika.

Viongozi wa kidini, kimila wamsifu Rais Magufuli

Katika hatua nyingine, viongozi mkoani Iringa, ambao ni pamoja na madiwani, viongozi wa vyama vya siasa, wa dini na wa kimila wamempongeza Rais Magufuli kwa jitihada alizozielekeza katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa, kama ununuzi wa ndege kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa lengo la kuimarisha utalii, ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa umeme wa Mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), ujenzi wa viwanja vya ndege, bandari, barabara na madaraja, ambavyo vitaimarisha uchumi na kujenga heshima ya nchi.

“Mhe Rais nchi yetu ina vivutio vya utalii, ina rasilimali nyingi, haya unayofanya sasa yanakwenda kuitangaza nchi yetu, ndege zetu zinaporuka zikiwa zimechorwa mnyama Twiga na zimeandikwa ‘The Wings of Kilimanjaro’ zinaitangaza nchi yetu, treni itainua uchumi wetu, tunakupongeza sana na tunakushukuru sana,” alisema Salim Asas, mjumbe wa Halmashauri Kuu na kaimu mwenyekiti CCM mkoani Iringa.

Katika hafla hiyo, ambayo pia ilihudhuriwa na mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli na baadhi ya mawaziri, Rais Magufuli aliwashukuru viongozi hao na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mkoa wa Iringa kusukuma maendeleo.

 Rais Magufuli alizindua barabara.

Jana, Rais Magufuli alihitimisha ziara yake mkoani Iringa kwa kuzindua barabara ya Iyovi – Iringa – Mafinga yenye urefu wa kilomita 218.6 iliyojengwa kwa mkopo nafuu kutoka Serikali ya Denmark na kugharimu Sh282 bilioni.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Mafuguli   ameiomba Denmark kupitia Danida kufadhili ujenzi wa barabara ya Igumbiro – Kihesa yenye urefu wa kilomita kumi na moja ambayo itasaidia magari yatokayo Kusini mwa Tanzania kwenda Dodoma kutopita katikati ya mji wa Iringa ili kuepusha msongamano na athari za ajali zinazoweza kutokea.

Rais Magufuli amesema mpango huo ulikuwapo tangu alipokuwa Wizara ya Ujenzi na kufafanua kwamba malori yanayopita katikati ya mji wa Iringa yamekuwa yakisababisha ajali.

“Nakuomba Balozi, hili mlichukue kama la urgent (haraka). Mkitusaidia kama mkopo sisi tuko tayari, mkitupa kama grant (msaada) tutashukuru zaidi. Kwa hiyo tunaomba utufikishie hili. Ikiwezekana barabara hiyo tutaiita Camilla Road,” alisema Rais Magufuli huku wananchi wakipiga makofi", alisema Rais Magufuli.

Awali, naibu Balozi wa Denmark nchini, Camilla Christensen alieleza kufurahishwa kwake na kukamilika kwa ujenzi huo na kusisitiza kuwa uhusiano wa Tanzania na Denmark ulioanza miaka 50 iliyopita utaendelea kudumishwa hususani katika vipaumbele vinavyohusu uchumi na fedha, afya, ajira na uboreshaji wa biashara.

Awali, Rais Magufuli alizindua kiwanda cha kutengeneza chakula cha kuku cha Silverland Tanzania Ltd na kuwapongeza viongozi kwa kuvutia uwekezaji wa viwanda ambavyo sasa vimefikia 2,963.

No comments:

Post a Comment

Popular