Wabunge wa chadema na wafuasi 37 wamepata dhamana. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 9 December 2017

Wabunge wa chadema na wafuasi 37 wamepata dhamana.

Mahakama ya Hakimu mkazi mkoani Morogoro imetupilia mbali hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya wabunge Suzan Kiwanga (Mlimba) na Peter Lijualikali (Kilombero) na washtakiwa wengine 37 waliofikishwa mahakamani hapo kwa makosa nane.

Mbele ya Hakimu, Ivan Msaki mahakama ilitupilia mbali kiapo hicho na kuelezea kuwa washtakiwa wote dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakao saini barua za dhamana ya sh milioni 5 na pia barua za dhamana lazima zisainiwe na wenyeviti wa serikali za vijiji ama maofisa watendaji wa vijiji.

Katika kiapo kilichowasilishwa awali mahakamani hapo na upande wa mashtaka kupitia wanasheria wa serikali, Sunday Hyera na Edga Bantulaki alielezea sababu walizodai kuwa ni za msingi za kupinga dhamana na kwamba kuwepo nje kwa washtakiwa kunaweza kuharibu upelelezi wa kesi hiyo.

Kufuatia hoja hiyo upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili wanne wakiongozwa na wakili  Peter Kibatala, uliamua kuwasilisha hati ya kiapo hicho kwa madai kuwa kiliandikwa bila ya kuzingatia misingi na matakwa ya kisheria.

Wakili Kibatala alidai kuwa miongoni mwa mapungufu yaliyokuwemo kwenye kiapo hicho ni pamoja na kutokuonyesha majina ya mkuu wa polisi kwa wilaya Malinyi (OCD) ambaye alitajwa kwenye kiapo hicho kama chanzo kilichotoa taarifa zilizotengeneza mashtaka yanayowakabili wabunge hao na wafuasi 37 wa chadema.

Wakili Kibatala alidai kuwa mapungufu mengine yaliyokuwepo kwenye kiapo hicho ni utofauti wa tarehe ya kuandika kiapo hicho na kusainiwa na hivyo waliomba mahakama kuzingatia mapungufu hayo.

Kutokana na mvutano huo wa kisheria baina ya pande hizo mbili Hakimu Msaki aliamua kupitia hoja za msingi za kisheria na hivyo kubaini mapungufu yaliyopo kwenye kiapo hicho na kuelezea kuwa mapungufu hayo hayawezi kurekebishwa na kwamba kazi ya mahakama ni kutafsiri sheria na si kufundisha namna ya kuandika kiapo.

Kabla ya kupewa dhamana washtakiwa hao walikaa rumande kwa siku kumi na mbili hali iliyosababisha kesi hiyo kuvuta hisia za watu wengi hususani viongozi na wanachama wa chadema waliokuwa wakifulika mahakamani hapo kufuatilia kesi

No comments:

Post a Comment

Popular