Wanawake waliovishana Pete za uchumba wafikishwa mahakamani. - KULUNZI FIKRA

Saturday, 9 December 2017

Wanawake waliovishana Pete za uchumba wafikishwa mahakamani.

Watu wanne wakiwemo wanawake wawili waliovishana Pete za uchumba wamefikishwa mahakamani jana ijumaa wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kujihusisha na vitendo vinavyoashiria kufanya mapenzi ya jinsia moja kinyume na Sheria.

Mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi, Gway Sumaye washtakiwa Milembe Suleiman (35) na Janeth Shonza (25) mwanafunzi wa sheria chuo kikuu cha mtakatifu Agustino (SAUT) walisomewa shtaka la kufanya vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja.

Wakili wa serikali, Emmanuel Luvinga alidai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Agosti 31 wakiwa katika hoteli ya Pentagon jijini Mwanza, kinyume na kifungu cha sheria namba 138A cha Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 16 kama na marekebisho yake ya mwaka 2002.

Katika shauri hilo namba 548/2017, wakili Luvinga alidai washtakiwa hao waligusanisha ndimi zao ikiwa ishara ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi kinyume cha Sheria.

Mshtakiwa mwingine, Aneth Mkuki (24) mkazi wa jijini Mwanza naye pia alifikishwa mahakamani kwa shtaka hilo hilo na kifungu hicho hicho cha sheria baada ya ya kudaiwa kusherehesha ji siku ya tukio hilo.

Mshtakiwa mwingine wa kiume, Richard Fabian (28) mkazi wa Buzuruga jijini Mwanza yeye anashtakiwa kwa kosa la kusambaza picha ya video za tukio hilo la kuvishana Pete kinyume na sheria ya mtandao kifungu cha 20 kifungu kidogo cha (1) (a) cha sheria ya mitandao namba 14 ya mwaka 2015.

Wakili Jebra Kambole anayewatetea washtakiwa hao, waliomba mahakama iwape dhamana kwa sababu mashtaka yanayowakabili yana dhamana, ombi lililokubaliwa na Hakimu Sumaye lakini alisema hawezi kutoa masharti ya dhamana kwa sababu shauri hilo lilipangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi, Wilbert Chuma ambaye akuwepo.

"Kwa sababu shauri hilo liko mbele ya Hakimu mwingine ambaye hayupo; siwezi kutoa masharti ya dhamana litabidi limsubiri mhusika", alisema Hakimu Sumaye.

Washtakiwa wamerejeshwa mahabusu hadi Desemba 13 shauri hilo litakaposomwa tena.

No comments:

Post a Comment

Popular