Ujenzi wa uwanja wa ndege Dar es salaam kukamilika mwenzi Septemba. - KULUNZI FIKRA

Friday, 8 December 2017

Ujenzi wa uwanja wa ndege Dar es salaam kukamilika mwenzi Septemba.

UJENZI wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JKIA), Terminal 3 hadi sasa umefikia asilimia 67 huku ukitarajiwa kukamilika Septemba mwakani na hivyo kuwezesha zaidi ya abiria milioni sita kuhudumiwa pindi utakapokamilika.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo jana unaogharimu kiasi cha Sh bilioni 560, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alidai kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo unaotekelezwa na Kampuni ya ‘BAM Internatinal’ ya nchini Uholanzi.

Mbarawa alisema tofauti na miezi mitatu iliyopita alipotembelea kukagua ujenzihuo, kwa sasa mkandarasi wa ujenzi huo ameonesha kuongeza kasi tofauti na ilivyokuwa awali, hatua aliyodai kuwa inaleta matumaini kuwa utakamilika ndani ya muda huo wa miezi kumi uliobakia.

“Mradi huu ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi kwa Taifa letu, hivyo ni muhimu mkandarasi ukazidi kuongeza kasi ili uanze kazi mara moja, fedha za malipo zipo hakuna shida zinalipwa kila inapohitajika,” alisema Profesa Mbarawa Alisema ujenzi huo pindi utakapoanza kazi utaongeza idadi ya abiria kutoka milioni mbili wanaohudumiwa Terminal 2 kwa sasa hadi milioni sita watakaohudumiwa katika uwanja huo huku idadi ya ndege nazo zikitajwa kuongezeka, pamoja na sehemu kuwahudumia abiria.

“Kwa ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 1300 hadi 1400, zitakuwa na uwezo kutua kwa wakati mmoja bila shida huku zile zinazobeba abiria 110 hadi 120 zikiweza kuhudumiwa kuanzia 21 kwa wakati mmoja,” aliongeza Prof. Mbarawa Maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaonekana kukamilika ni pamoja na sehemu ya kuruka na kutua ndege huku jengo la abiria ujenzi wake ukionekana kukamilika kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela alisema uwanja huo utakapokamilika utakuwa na vifaa mbalimbali vya ukaguzi vitakavyoweza kudhibiti aina mbalimbali za udanganyifu ikiwemo kuzuia magendo. Naye Balozi wa Uholanzi nchini, Jeroen Verheul alisema licha ya kuwa mradi huo kuwa muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, pia utazidi kuongeza ushirikiano baina ya nchi yake na Tanzania sambamba na kukuza utalii.

No comments:

Post a Comment

Popular