Rais Magufuli asimulia historia ya maisha ya ujana wake. - KULUNZI FIKRA

Tuesday, 5 December 2017

Rais Magufuli asimulia historia ya maisha ya ujana wake.

 Usiku wa Kitendawili unazidi kupamba moto ambapo Rais, Dkt John Pombe Magufuli mnamo Desemba 8, mwaka huu na atafungua siri na malezi yake ya utotoni ambayo ndiyo yaliyomfanya leo hii awe mzalendo wa kweli wa nchi yake.

Rais Magufuli ambaye atakuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Kampeni ya Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’ atafunguka kuhusu  maisha yake aliyoyapitia na kumfanya leo kuwa mzalendo wa kweli ndani ya Tanzania, na mwenye kuhimiza kila Mtanzania kuwa mzalendo wa kweli wa nchi yake.

Siku hiyo, Watanzania watasikia kauli za viongozi mbalimbali wastaafu na walioko madarakani kuhusu harakati za Tanzania kupata uhuru, na kupinga kabisa ukabila licha ya Tanzania kuwa na makabila 120.

Viongozi hao wa zamani watakuwa wamekaa chini kwenye mikeka ya asili na vigoda, na kuelezea namna serikali na viongozi wake walivyoweza kuondoa mambo ya ukabila ambao bado unazitesa nchi nyingi za Afrika.

Akizungumza na kituo kimoja cha habari katika Kipindi cha Tanzania Mpya, Mrisho Mpoto amesema kuwa;

“Rais, Dkt Magufuli atapata fursa ya kueleza maisha yake ya utoto na namna alivyoweza kusimama katika mstari ambao kila mmoja kwa sasa akiangalia matendo yake anaona rais kweli ni mzalendo wa kweli.

“Tutakuwa na Rais, Dkt John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na wote watapata fursa ya kueleza mawili machache kuhusu namna walivyoweza kuwa wazalendo wa kweli wa nchi yao.

“Tumeomba protocol zisiwe kali sana kwa upande wa Watanzania na viongozi ili watu wafunguke, tunataka Rais wetu atuambie kwa nini ni mzalendo wa kweli, kwa nini ana uchungu na Watanzania wa chini ambao ni wanyonge zaidi. Kwa nini anahamasisha kuwa Tanzania ya Viwanda?

Mpoto aliongezea kuwa: “Tutakaa kwenye mikeka na vigoda, tutakula ugali wa muhogo, kisamvu na madafu, Majaliwa pale, Mama Samia pale, ukumbi wenyewe umetengenezwa kama kuna vijiji na mitaa, Mhe atapita pale kwenda kusalimia kijiji cha jirani watuambie tu wamewezaje kuondoa suala la ukabila, nchi za wenzetu wanapigana kila siku. Hakika tuna kila sababu ya kuwa wamoja na kuimba wimbo mmoja wa Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’.”

Usiku wa Kitendawili umeanzishwa na msanii Mpoto baada ya kuachia wimbo wake ‘Kitendawili’ na kuamua kuanzisha usiku huo, kwa ajili ya kuwakutanisha wadau na kujadili kuhusu Uzalendo.

Baada ya uzinduzi, kampeni hiyo itakuwa ikifanyika kila mwaka sambamba na maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati, Julis Kambarage Nyerere, na itakuwa ikizunguka katika mikoa mbalimbali kupaza sauti kuhusu uzalendo.

Kampeni ya uzalendo itazungumzia kudhibiti na kukomesha mmomonyoko wa maadili kwa viongozi wa umma, kupunguza tuhuma za rushwa, ufisadi, ubadhilifu wa mali za umma na kuongeza hali ya kufanya kazi na Uzalendo.

No comments:

Post a Comment

Popular