Wabunge wataka Serikali kuondoa changamoto katika Wizara ya Elimu. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 2 May 2018

Wabunge wataka Serikali kuondoa changamoto katika Wizara ya Elimu.

 
Mbunge wa Jimbo la Vunjo (NCCR), Mhe  James Mbatia amesema Serikali inapaswa kukubali kwamba Taifa linakabiliwa na tatizo la elimu na inapaswa ikubali kufanya mabadiliko ili kuinusuru nchi kwa kuwa na wasomi wasiokuwa na uwezo.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu kwa 2018/19, Mhe Mbatia amesema itikadi za vyama zinapaswa kuwekwa kando wakati suala la elimu linapojadiliwa.

“Kinga ni bora kuliko tiba, kupitia wizara ya elimu, tunakumbatia ujinga, ufisadi, rushwa na mambo mengine. Watu wanaangamia, hasa ukitumia vitabu mfano wa darasa la pili, unaambiwa unganisha sauti, ni lini sauti inaunganishwa? Na hivi ni vitabu vya sasa vinasambazwa,”amesema Mhe Mbatia.

Mhe Mbatia akichangia wakati akifanya rejea ya vitabu alivyoingia navyo bungeni amesema: “Baadhi ya vitabu havina majina ya uhariri, vitabu vimefanyiwa maboresho lakini bado ni vibovu.

Mhe Mbatia ambaye amechangia huku akitoa mifano nadharia ya kufundisha akiimba na silabi za a, e, i, o, u huku wabunge wa pande zote na mawaziri wakimshangilia amesema: “Rai yangu, turejee katika mjadala wa taifa, tuwe na matokeo ya muda mfupi.”

Mbunge wa Jimbo la  Nchemba (CCM), Mhe Juma Nkamia amesema shule binafsi hazipaswi kuchukuliwa kama washindani: “Tuwachukulie kama sehemu yetu kwa sababu wanasomesha watoto wetu.”

Pia, Mhe Nkamia amezungumzia ratiba za wanafunzi katika shule binafsi na kusema, wanafunzi wanapoamka mapema wanashindwa kumudu masomo yao.

“Mfano mtoto anachukuliwa Mbagala anakwenda kusoma Masaki, mtoto anachukuliwa saa 10 au 11 asubuhi, hivi huyu mtoto anakwenda kusoma au kulala, hili mheshimiwa waziri lichukueni hili na mlifanyie kazi,” amesema Mhe  Nkami.

No comments:

Post a Comment

Popular