Mkuchika afunguka kuhusu watumishi wa darasa la saba kutorejeshwa Kazini. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 3 May 2018

Mkuchika afunguka kuhusu watumishi wa darasa la saba kutorejeshwa Kazini.

 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Mhe  George Mkuchika amesema watumishi waliotakiwa kurejeshwa kazini wanapaswa kuwa wamerejeshwa.

Mhe Mkuchika alisema hayo Jana alipojibu swali la mwandishi wetu  aliyetaka kujua kauli ya Serikali kutokana na malalamiko ya watumishi wa darasa la saba ambao wanadai bado hawajarejeshwa licha ya agizo la Serikali.

“Ninachojua wamesharudi kazini na yule ambaye hajarudi atakuwa na sababu na ameelezwa,” alisema  Mhe Mkuchika.

Mhe Mkuchika alisema, “Sababu ndizo zinaweza kumfanya akaenda kwa viongozi wake lakini kama hajaridhika, kuna Tume ya Utumishi wa Umma ambayo mwenyekiti wake ni jaji mstaafu wa Mahakama Kuu.”

Mhe Mkuchika alisema akifika huko, yeye na mwajiri wake watasikilizwa ni kwa nini hajarudishwa kazini.

Juzi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani mkoani Pwani, yalitolewa malalamiko kuwa agizo la Serikali la kuwarejesha kazini watumishi hao halijatekelezwa. Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi mkoani Pwani, Kinyogoli Ramadhani alizitaka mamlaka husika kutekeleza agizo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alisema, “Nasikitika nimesikia hapa kuwa bado wale watumishi wa darasa la saba waliotakiwa kurejeshwa hawajareshwa. Nawaagiza wakurugenzi wote mkalifanyie kazi agizo la Serikali mara moja kwa kupingana nalo ni kushindana na Serikali kitu kinachoweza kuleta matatizo kwenu.”

Aidha, kaimu ofisa utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, Protas Dibogo amesimamishwa kazi kwa kutowarudisha kazini watumishi walioondolewa kazini kimakosa kutokana na kutokuwa na elimu ya kidato cha nne.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Peter Nyalali juzi kupitia kituo cha televisheni cha Azam, akizungumza na watumishi hao alitangaza uamuzi huo akiagiza warudishwe kazini kama Serikali iliyoelekeza.

Halmashauri ya Bumbuli iliwasimamisha watendaji wa vijiji 41 ambao ofisa huyo alisema barua zao zina upungufu.

No comments:

Post a Comment

Popular