Ahadi ya Nyongeza nono ya Mishahara kwa Wafanyakazi yazidi kuibua Mijadala. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 2 May 2018

Ahadi ya Nyongeza nono ya Mishahara kwa Wafanyakazi yazidi kuibua Mijadala.

 
Ahadi ya nyongeza nono ya mishahara kwa wafanyakazi iliyotolewa na Rais  Dkt John Pombe Magufuli imeibua mjadala.

Juzi, Rais alizungumza na wafanyakazi nchini katika Siku ya Wafanyakazi Duniani na wengi walitarajia tamko lake la nyongeza ya mishahara, lakini kiongozi huyo aliwaambia wawe wavumilivu na atafanya hivyo kabla ya kuondoka madarakani.

Kwa sasa, Rais alisema hatarajii kuongeza mishahara kutokana na Serikali anayoiongoza kutingwa na majukumu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rais  Magufuli alisema, “Na mimi nataka niwaeleze, kupandisha kwangu kutakuwa si kwa Sh10,000. Kutakuwa kupandisha kwelikweli.”

Walichosema wabunge

Jana wakati Bunge likiendelea mjini Dodoma, wabunge SMhe ixtus Mapunda (Mbinga Mjini-CCM) na  Mhe Mussa Sima wa Singida Mjini (CCM), waliomba mwongozo wa Spika wakitumia kanuni ya 67(8) inayohusu jambo lililotokea hivi karibuni wakiitaka Serikali kutoa majibu ni lini mishahara itapanda.

Mhe Mapunda alikuwa wa kwanza kuzungumza akisema,“…Kuondoa umaskini wa kipato, kuna uhusiano wa moja kwa moja na ongezeko la mishahara ya watumishi wa Serikali wa pande zote.”

“Na kwa kuwa Jana (juzi), siku ya Mei Mosi Rais aliji ‘commit’ kuwa ongezeko la mishahara pamoja na mambo mengine litazingatia hali halisi ya uchumi, uwezo wa Taifa na uwezo halisi wa Serikali, Serikali inatoa kauli gani, lini mishahara hiyo itapanda kwa sababu suala hili jana limeacha sintofahamu kwa wananchi?" alihoji Mhe Mapunda.

Mhe Sima licha ya kumpongeza Rais Magufuli kwa hotuba aliyoitoa alisema, “Lakini kama Bunge, tungetaka kujua ni lini sasa watumishi hawa watapandishiwa mishahara.”

Akijibu miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mhe  Andrew Chenge alisema hata yeye alimsikiliza vizuri Rais akielezea suala hilo na kwa kuwa ni swali linalohusu masilahi ya wafanyakazi wa Tanzania alisema, “Mkiwa na kiongozi msema kweli, alisema kwa sasa hawezi kuongeza mishahara na hali itakaporuhusu ataongeza na amesema hali ikiwa nzuri, ataongeza kwelikweli, sasa ni lini, mnaiachia Serikali na Serikali mnaweza kupata nafasi nzuri mkalielezea na mkawapa matumaini.”

Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mbunge wa Ukonga (Chadema),  Mhe Mwita Waitara alizungumzia nyongeza ya mishahara akisema, “Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta anasema ataongeza asilimia tano, sisi huku hakuna.”

Kisha akaongeza, “Mwaka Jana (Rais) aliahidi ataongeza lakini Jana (juzi) mlisikia alivyosema.”

Kauli hiyo ilimfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama kusimama lakini kabla ya kuzungumza alikatishwa na Chenge aliyesema, “Hivi aliwaaminisha kwamba hataongeza, mimi nilimsikiliza. Hakusema hivyo na mwaka jana mheshimiwa Rais hakuahidi, kama una ushahidi lete hapa.”

Akizungumza na Mwandishi wetu nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Kaliua (CUF), Mhe Magdalena Sakaya alisema umefika wakati Rais Magufuli aongeze mishahara kwa kuwa kinyume cha hilo atakuwa na watumishi wasiokuwa na morali ya kazi.

Alisema maisha ya miaka miwili iliyopita ni tofauti na sasa.

“Mtu aliyekuwa anapata mfano Sh500,000 kwa mwezi mwaka jana, mwaka huu haiwezi kutosha. Umeme, maji na kila kitu kimepanda. Kwa hiyo wanapaswa kuongezwa mshahara ambao ni haki yao,” alisema Mhe Sakaya.

Mhe Sakaya ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa CUF aliongeza, “Unaweza kujenga barabara, ukajenga hiyo miundombinu inayosemwa, lakini kama huna watumishi wenye moyo wa kufanya kazi itakuwa kazi bure.”

“Ndiyo maana Jana (juzi), baada ya Rais Magufuli kusema hataongeza mishahara, utaona wafanyakazi walivyoonyesha nyuso za huzuni, za kutaka tamaa. Kwa hiyo sisi kama wabunge tunahitaji kujua ni lini hawa wafanyakazi wataongezewa mishahara.”

Mbunge wa Ulanga (CCM), Mhe Goodluck Mlinga alisema, “Kupanga ni kuchagua, kwa hiyo wafanyakazi wavute subira kama alivyosema Rais, atawaongeza mishahara.”

Mbunge wa Nanyamba (CCM),  Mhe Abdallah Chikota alisema kumekuwa na matarajio kuwa Serikali itaongeza mishahara, hivyo watumishi wa umma wanasubiri Serikali itasema nini kuhusu suala hilo.

“Ni muda mrefu sasa mishahara ya watumishi haijapandishwa, muda sasa umefika wa kutekeleza jambo hilo lakini kwa kuwa chungu kilichopo kinatumika katika ujenzi wa miundombinu, ujenzi wa reli ya kisasa na mingine ambayo kimsingi ndiyo itakayoleta fedha, sasa ni kuendelea kusubiri,” alisema Mhe Chikota.

Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mhe Ruth Mollel alisema kushindwa kuongeza mishahara ya watumishi wa umma ni dalili kwamba uchumi haukui au uwekezaji unaofanyika haufanyiki kwa kuangalia umuhimu wa rasilimali watu katika uendeshaji wa uchumi, jambo ambalo linaufanya uwekezaji huo kutokuwa na maana kwa jamii.

“Tukumbushane moja ya kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa dhana ya maendeleo ya nchi ni lazima ionekane kwa watu na si kwa vitu,” alisema Mhe Mollel.

Mhe Mollel alisema uboreshaji wa masilahi ya watumishi wa umma umeendelea kutegemea utashi binafsi wa viongozi wa nchi.

“Hakuna mfumo madhubuti wa kusimamia na kutekeleza mipango inayolinda masilahi ya watumishi wa umma,” alisema Mhe Mollel.

“Tukumbuke kwamba kuna chombo cha Serikali ambacho kazi yake ni kujadiliana na vyama vya wafanyakazi kuhusiana na ongezeko la mishahara kwa watumishi, lakini kutokana na udhaifu wa miundo na mifumo ya Serikali taasisi hiyo imekuwa dhaifu kuweza kukutana na kutimiza majukumu yake,” alisema Mhe Mollel.

Maoni ya wafanyakazi

Baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na gazeti hili walikuwa na mitazamo tofauti kuhusu kauli ya Rais, baadhi wakisema wanasubiri kwa hamu ongezeko hilo, huku wengine wakieleza kukata tamaa.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwandege iliyopo mkoani Pwani, Azania Kimeru alisema hawezi kupingana na kauli ya Serikali na anachosubiri ni utekelezaji wa ahadi ya nyongeza ya mshahara.

“Binafsi nimeilewa Serikali ila ninachoomba ahadi ya kuongezewa mishahara iwe ya kweli, hiyo miradi ikimalizika tuangaliwe na sisi wafanyakazi,” alisema Kimeru.

Mwalimu mkuu wa shule moja ya sekondari iliyopo wilayani Kongwa aliyezungumza kwa sharti la kutotaka Jina litajwe, alisema kauli hiyo imemkatisha tamaa.

“Matarajio yetu jana (juzi) yalikuwa kuongezewa mishahara lakini tumaini letu likakatika baada ya kusikia kuwa kwa sasa hakuna nyongeza,” alisema Mwalimu huyo.

Alisema kazi wanayoifanya ni kubwa kuliko mshahara wanaoupata, hivyo wanaiomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma.

“Ahadi ni deni, tunaamini Serikali itatekeleza, tunasubiri miradi ikamilike lakini tumekata tamaa,” alisema Mwalimu huyo.

Kauli ya mwalimu huyo iliungwa mkono na mwalimu mmoja wa shule ya msingi iliyopo jijini Dar es Salaam aliyesema, “Kinachokatisha tamaa ni mazingira magumu ya kufanyia kazi. Kama hapa Dar es Salaam ulipe usafiri, fedha ya kula mchana, watoto nyumbani wanahitaji kula, mawazo yanazidi kuongezeka ukifikiria mshahara ulivyo mdogo.”

Muuguzi katika Hospitali ya Amana mkoani Dar es Salaam, Teresia Akida alisema: “Siwezi kuzungumza chochote kwa kuwa tumeshaahidiwa kuongezewa mshahara, hivyo tunasubiri.”

Dereva wa mojawapo ya manispaa za Jiji la Dar es Salaam aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema alishindwa kuendelea kufuatilia maadhimisho ya Mei Mosi juzi kupitia televisheni baada ya kusikia hakuna nyongeza ya mshahara.

Viongozi vyama vya wafanyakazi

Baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi waliozungumza na Mwananchi, walisema jambo hilo linahitaji kikao cha pamoja ili kupata majibu, huku mwingine akiwaonea huruma wafanyakazi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Majumbani, Watoa Huduma na Mahoteli (Chodawu), Said Wamba alisema tamko la kuomba nyongeza ya mshahara lilikuwa la vyama vyote vya wafanyakazi, hivyo majibu yatategemea makubaliano ya pamoja.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (Tuico) Mkoa wa Kinondoni, Mansoor Ramadhani alisema uzalishaji mzuri sehemu ya kazi unategemea zaidi motisha ya mfanyakazi ikiwamo nyongeza ya mshahara.

“Wengi walikuwa na shauku ya kujua ongezeko la mshahara lakini kauli waliyoisikia ni kama iliwavunja moyo, tija na ufanisi kazini unategemea pia namna mfanyakazi anavyopewa motisha,” alisema

No comments:

Post a Comment

Popular