Waziri wa Fedha akiri wananchi kuwa maskini licha ya nchi kuwa na utajiri wa Rasilimali. - KULUNZI FIKRA

Wednesday, 2 May 2018

Waziri wa Fedha akiri wananchi kuwa maskini licha ya nchi kuwa na utajiri wa Rasilimali.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt  Philip Mpango amesema licha ya utajiri wa rasilimali uliopo nchini wananchi wameendelea kuwa maskini.

Akizungumza leo Mei 2,2018,  wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa taasisi ya utafiti wa uchumi na jamii (ESRF) Dar es salaam, Dkt Mpango aliyemwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametaja sababu kubwa kuwa ni kutokuwepo kwa uwiano kati ya ukuaji wa uchumi na sekta ya Kilimo.

“Tanzania ni tajiri wa rasilimali. Tunayo maziwa kama Victoria, Tanganyika, Rukwa, Nyasa na mito mingi inayotoa fursa za uvuvi na uzalisha wa umeme. Tuna utajiri wa madini kama dhahabu, almasi, Tanzanite, ruby, bati, chuma, mkaa, uranium, gesi ya asili, helium na mengineyo,” amesema Dkt  Mpango.

Dkt Mpango ameongeza kuwa Tanzania ni kituo kikubwa cha utalii ikiwa na urefu wa kilometa 1,200 za fukwe za bahari, hifadhi za wanyama, huku  ikiwa nchi ya amani na utulivu isiyokuwa na machafuko ya kikabila.

“Hata hivyo, uporaji wa maliasili umesababisha maisha ya Watanzania walio wengi kuwa masikini, huku wachache wakifaidi rasilimali hizo,” amesema Dkt Mpango.

Aidha Dkt Mpango ametaja chanzo cha matatizo hayo kuwa pamoja na ukosefu wa teknolojia ambapo alitoa mfano wa wachimbaji wadogo wa madini wanaoshindwa kupata madini ya kutosha kwa kutokuwa na teknolojia.

No comments:

Post a Comment

Popular