Waziri mkuu atoa onyo kwa Wabunge. - KULUNZI FIKRA

Thursday, 19 April 2018

Waziri mkuu atoa onyo kwa Wabunge.

 
Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wabunge na viongozi wengine kuacha tabia ya kuingiza siasa kwa watu wanaoishi mabondeni kwa kuwatetea kutohama maeneo hayo jambo ambalo linawapelekea kupata madhara pindi mvua kubwa zinaponyesha kama ilivyo sasa.

Waziri mkuu ametoa kauli hiyo leo Aprili 19, 2018 Bungeni mjini  Dodoma kwenye kikao cha 13 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la Mbunge wa Temeke Mhe  Abdalla Mtolea ambapo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuhakikisha madhara yanayojitokeza katika jiji la Dar es Salaam na mvua kudhibitiwa?

"kupitia Manispaa za jiji la Dar es Salaam na serikali yake kupitia wizara zake zinazo mipango ya kuboresha miundombinu katika miji yetu katika makao makuu ya mikoa na maeneo yote yale yanayokaliwa na watu wengi ikiwepo DSM. Tunayo miradi sasa ambayo itaweza kuboresha miundombinu ikiwepo na bonde la Msimbazi ambalo linaleta madhara mengi", amesema Waziri mkuu.

"Mara kadhaa tumeshuhudia mvua hizi zinapoleta madhara kwa wale walioko mabondeni pamoja na serikali kuwaambia waondoke mabondeni tumekuwa tukiingilia sana utendaji kwa kuingiza siasa za kuwataka watu wabaki huku wengine wakijafanya wanawaonea huruma na kushindwa kutoka katika mabonde kutokana na utetezi unaotoka kwa watu wenye mapenzi yao binafsi", amesema Waziri mkuu.

Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema,"Nitoe wito kama ambavyo tunaendelea kutoa wito na Waheshimiwa Wabunge kupitia Bunge hili tuwasii watanzania na kuwataka wote wanaoishi mabondeni wahame kwasababu mvua hizi zinapokuja wanapata madhara makubwa na hatimaye sasa hata katika kuwaokoa inakuwa shida. Kwa hiyo ni vizuri sasa tukashirikiana",amesema Waziri mkuu.

Pamoja na hayo, Waziri mkuu ameendelea kwa kusema "serikali kwa upande wake inaanda fedha kuhakikisha kwamba ile miundombinu ya mabonde ina boreshwa ili maji yaweze kupita kwa ulaini. Lakini watu waliokaa katika mabonde na yale maeneo yote waliyokataziwa waanze kuondoka mapema ili wasiweze kupata madhara pindi mvua nyingi zinapojitokeza".

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewapa pole wananchi wote walioweza kupata maafa ya aina yeyote yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini

No comments:

Post a Comment

Popular