Watumishi watatu wa TRA Wahojiwa. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 15 April 2018

Watumishi watatu wa TRA Wahojiwa.

Watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Arusha wamehojiwa na kikosi maalumu kutoka mamlaka hiyo makao makuu jijini Dar es salaam kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa sanjari na kutofuata maadili ya kazi.

Akizungumza na kulunzifikra blog, Leo Aprili 15, 2018 kuhusu kuhojiwa kwa watumishi hao, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa walipa  kodi wa TRA, Richard Kayombo amesema hawezi kulizungumzia kwani ni kinyume na taratibu za kazi.

Naye Meneja wa TRA mkoani Arusha, Faustine Mdesa alipotafutwa hakukana wala kukubali kuhojiwa huko akisema watumishi wengi wanahojiwa na huenda wanaofanya kazi hawakupita ofisini kwake.

Watumishi hao ambao majina yao yamehifadhiwa kutokana na kutopatikana kuzungumzia tukio hilo, wamenyang’anywa mawasiliano ya simu zao za mkononi sanjari na nywilwa (password) zao za barua pepe binafsi.

Taarifa kutoka ndani ya mamlaka hiyo zimeeleza kitendo cha kuhojiwa kwa watumishi hao kimewashtua baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo huku baadhi yao wakihofia kuhojiwa wakati wowote na kikosi hicho maalumu.

No comments:

Post a Comment

Popular