Kifo cha mtoto wa Miezi sita kimeibua utata Jijini Mwanza. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 15 April 2018

Kifo cha mtoto wa Miezi sita kimeibua utata Jijini Mwanza.

 
Usiku wa Aprili 3, utabaki katika kumbukumbu za Ashura Theonest (26), mkazi wa mtaa wa Ibanda, Kata ya Nyegezi jijini Mwanza baada ya mtoto wake, Khalfan Lema aliyekuwa na umri wa miezi sita kufariki dunia.

Ashura anasema asubuhi ya Aprili 2 ilikuwa chanzo cha kumpoteza mtoto huyo baada ya kushukiwa na jirani yake kuwa amemuibia simu ya mkononi.

Ilikuwaje?

“Siku hiyo nilikuwa kwa rafiki yangu, nikiwa nimeketi nje nikimsubiri arudi kutoka kwenye starehe zake ghafla mama (anamtaja jina) alikuja akaniambia nimpeleke mtoto ndani kwa kuwa usiku umekuwa mkubwa,” anasimulia Ashura.

Anasema dakika chache baada ya kuingia ndani kwa huyo mama, rafiki yake alirejea, akafungua mlango wa chumba chake wakaingia kulala, lakini baada ya takriban saa moja waliamshwa na yule mama akiwaulizia kuhusu simu yake aliyodai kuwa imepotea.

Ashura anasema jambo hilo lilizua mvutano na kulazimika kuitwa kwa uongozi wa mtaa, ambapo katibu wa mwenyekiti walifika kuwasuluhisha na kuahidi suala hilo litazungumzwa asubuhi.

“Asubuhi kulipokucha, yule mama alikwenda kuripoti polisi Nyegezi na alipopewa RB alikuja kunichukua, badala ya kunipeleka Nyegezi alibadilisha uamuzi na kunitaka twende Igogo ambapo nilifika na kufunguliwa mashtaka ya kuiba simu.”

Anasema pamoja na kukataa kutofanya kitendo hicho na kumtaka askari aliyekuwa akishughulikia suala hilo waende nyumbani kwa rafiki yake wakakague mabegi yake, lakini hakuweza kukubaliwa.

Kutokana na kutokuwa na mtu wa kumuwekea dhamana alilazimika kukaa chumba ambacho alielezwa kuwa ni mahabusu ya wanawake akiwa na mwanaye.

“Nilikaa pale kituoni tangu saa tatu asubuhi hadi kesho yake Aprili 3, saa kumi na mbili jioni baada ya askari aliyekuwa anaingia zamu kukataa kunipokea kutokana na hali ya mwanangu kuwa mbaya,” anasema Ashura.

Kifo cha mwanaye

Ashura anasema anaamini mwanaye alifariki dunia kwa tatizo la njaa, baada ya kukaa takriban saa 33 bila kula chakula chochote wakiwa polisi.

Mzazi huyo anasema walipofikishwa kituoni na mwanaye walikuwa hawajala na walishinda pale bila kula na kwamba, hata maziwa aliyokuwa akimnyonyesha yalikata na kusababisha mtoto kuwa analia kila wakati.

Ashura anasema hali ya mwanaye ilibadilika kitendo kilichomlazimu kuomba kwa askari aliyekuwepo ajidhamini ili ampeleke mtoto huyo hospitali. “Nilimfuata zaidi ya mara tatu nikimsihi aniruhusu nijidhamini ili nimpeleke mwanangu hospitali, lakini alinikatalia akidai kuwa sheria hairuhusu kujidhamini, nisubiri mtu atakayekuja kunidhamini,” anasema.

Anasema ilipofika saa kumi na mbili jioni ya Aprili 3, wakiwa wanakabidhiana zamu maaskari, mmoja wa waliokuwa wanaingia kazini aliona hali ya mtoto si nzuri na akagoma kumpokea.

Jambo hilo lilimlazimu askari aliyekuwa anatoka amruhusu Ashura kwa sharti la kupigwa picha na kurekodiwa kwa simu na maandishi ili asije akakimbia kupoteza ushahidi.

Anasema baada ya kitendo hicho kumalizika, alichukua pikipiki kumuwahisha mtoto Hospitali ya Wilaya Nyamagana ambapo baada ya kumfikisha daktari aliyekuwa zamu alimpokea na kulazimika kumpeleka kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) ambako aliwekewa mashine ya kumsaidia kupumua.

Anasema saa tisa baada ya kufikishwa hospitalini hapo mtoto alifariki dunia huku ugonjwa aliolezwa na daktari kusababisha kifo hicho ukiwa ni nimonia kali iliyosababishwa na baridi.

Ashura ambaye kwasasa yuko kwao mkoani Kagera anasema kitendo hicho hatakisahau na kwamba, hawezi kulipa kisasi isipokuwa anamwachia Mungu.

Wagoma kumzika mtoto

Pamoja na kwamba mtoto huyo alizikwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliofika baada ya kusikia wananchi wa eneo husika wanataka kuandamana hadi polisi kupeleka maiti ya mtoto huyo, jirani wa Ashura anasema kifo hicho kimeliachia kovu jeshi hilo na hakitasahaulika. Jirani huyo, Mrisho Idd anasema wanawalaumu polisi kwa kushindwa kumruhusu Ashura ajidhamini wakati mtoto wake alikuwa katika hali mbaya.

“Tulishangaa kwani hata kaburi lenyewe lilichimbwa kwa usimamizi wa polisi na baada ya shehe wa msikiti wa mtaa wa Ibada kumaliza kumswalia (marehemu), walichukua mwili wa na kuuingiza kwenye gari lao kisha kuongozana kwenda makaburini kuupumzisha,” anasema .

Anasema kitendo cha polisi kusimamia mazishi hayo ni baada ya wanajamii kususia kuzika wakiwatuhumu walinda usalama hao kusababisha kifo hicho.

Mmiliki wa nyumba aliyofikia Ashura, Mathias Nyasesu alisema mzazi huyo hakuwa mpangaji wake na kwamba, alikuwa akiishi na rafiki yake.

Anasema baada ya mazishi kumalizika, mama aliyemshtaki Ashura kwa kosa la kuiba simu alifukuzwa kwenye mtaa huo na juhudi za kulunzifikra blog kumpata zilishindikana.

No comments:

Post a Comment

Popular