Mambo Matatu yaliyotikisa Vikao vya Bunge Jijini Dodoma. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 29 April 2018

Mambo Matatu yaliyotikisa Vikao vya Bunge Jijini Dodoma.

Uamuzi wa Serikali kutenga Sh495 bilioni katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2018/19 kwa ajili ya kununua ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ni miongoni mwa mambo matano yaliyotikisa mkutano wa 11 wa Bunge la Bajeti unaoendelea Jijini  Dodoma.

Baadhi ya wabunge walisema kuwa ununuzi huo si kigezo cha kulifufua shirika hilo linalomilikiwa na Serikali.

Mambo mengine yaliyotikisa kuanzia Jumatatu hadi juzi ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) maarufu kama reli ya mwendokasi, kufungiwa kwa nyimbo za wasanii, magazeti pamoja na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kutengewa fedha kidogo.

Wabunge watia neno ATC

Michango ya baadhi ya wabunge akiwamo Hussein Bashe wa Nzega na Halima Mdee (Kawe) ni kama ilifungua njia kwa wengine bila kujali itikadi zao kuchangia mambo hayo na kuikosoa Serikali.

Licha ya hoja ya ATCL kuzungumziwa na wabunge wengi kwa njia mbalimbali, mchango wa Mdee uliibua hisia tofauti na kufikia hatua ya mawaziri kumkatiza na kutoa ufafanuzi.

Mbunge huyo alieleza kuwa amesoma taarifa za Msajili wa Hazina na za ATCL zinazoonyesha kuwa shirika hilo lina madeni, haliwezi kujiendesha kibiashara na halijafanyiwa hesabu muda mrefu.

Alisema katika bajeti ya mwaka 2017/18 Serikali ilitenga zaidi ya Sh500 bilioni kununua ndege, mwaka huu wa fedha unaoanzia Julai Mosi imetenga Sh495bilioni, lakini fedha hizo zinapelekwa kununua ndege kwenye shirika alilodai kuwa halina mpango wa biashara.

Hoja hiyo iliwanyanyua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya kutoa ufafanuzi huku wabunge zaidi wakitaka ATCL kukodi ndege siyo kununua mpya.

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde alihoji sababu za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutofanya ukaguzi wa hesabu za ATCL na kuungwa mkono na wabunge wa chama hicho, James Ole Millya (Simanjiro) na John Heche (Tarime Vijijini).

Hoja hizo zilimfanya Waziri wa wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa kutoa ufafanuzi akibainisha kuwa ATCL ilikuwa haijakaguliwa tangu mwaka 2007 hadi 2015, na kwamba ukaguzi baada ya kukamilika, unaendelea kufanyika wa mwaka 2015/16 na 2016/17.

Pia alisema gharama za kukodi ndege ni kubwa ilhali kununua mpya kuna unafuu kwa Taifa.

Ujenzi wa reli ya kisasa

Suala la ujenzi wa reli ya kisasa lilitikisa siku tatu za mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano huku hoja ya Bashe ya kutaka Sh100 bilioni zilizotengwa kujenga reli hiyo kutoka Isaka kwenda Rusumo, ikiungwa mkono na wabunge wengi.

Waliomuunga mkono mbunge huyo ni Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini), James Mbatia (Vunjo), John Heche (Tarime Vijijini), Magdalena Sakaya (Kaliua) na Daniel Nsanzugwako (Kasulu Mjini).

Katika hoja yake hiyo, Bashe alisema kwa mujibu wa Ilani ya CCM, ujenzi wa reli hiyo ni kutoka Dar es Salaam-Tabora, Tabora-Mwanza, Tabora-Kigoma, Kaliua-Mpanda-Kalemii na Uvinza-Msogati, na si Isaka-Rusumo na kutaka kiasi hicho kielekezwe katika ujenzi wa reli hiyo eneo la Makutopora-Tabora.

Licha ya kubanwa na wabunge, Profesa Mbarawa alisema reli haiwezi kujengwa kwa Sh100 bilioni na kwamba fedha ni kwa ajili ya kulipa fidia na upembuzi yakinifu.

Kufungiwa magazeti

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Devotha Minja alihoji utaratibu wa magazeti kutakiwa kuhuisha leseni kila mwaka na kubainisha kuwa huo ni mpango wa Serikali kutaka kuvibana vyombo vya habari vinavyoikosoa huku vile vinavyoipamba vikilindwa.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema jambo hilo linafanyika kwa kuwa awali kulikuwa na utitiri wa magazeti ambayo yalikuwa hayachapishwi na kubainisha kuwa magazeti yanafungiwa kwa mujibu wa sheria.

Waziri huyo pia alitolea ufafanuzi hoja ya wabunge na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Bodi ya Ithibati ya Wanahabari kutoanza kazi, akibainisha kuwa uanzishwaji wa bodi hiyo unategemea zaidi vyombo vya habari na kubainisha kuwa Serikali haiwezi kuianzisha kuepuka watu kuiona kuwa ni mali ya Serikali.

Kufungiwa nyimbo za wasanii

Amina Mollel (viti maalumu-CCM) na mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku maarufu Musukuma walikuwa miongoni mwa wabunge waliohoji sababu za Serikali kufungia nyimbo za wasanii bila kuthamini juhudi kubwa zilizofanywa na wasanii hao.

“Kipindi cha hivi karibuni kumeibuka fungiafungia. Mnafungia nyimbo kwa sababu ya mpasuo wakati mnakaa na kutazama nyimbo za akina Rihanna kwenye Youtube,” alisema Musukuma.

Naye Tauhida Nyimbo (viti maalumu-CCM) alisema, “Wasanii wanaonewa, inapaswa Basata (Baraza la Taifa la Sanaa), kabla wasanii hawajatoa nyimbo mjue maudhui yake. Wasanii wanatumia tungo tata katika nyimbo zao kaeni nao si kufungia tu.”

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alisema kuna kanuni zinazowataka wasanii kupeleka nyimbo zao Basata kabla ya kuzitoa.

Ujenzi wa barabara

Hoja nyingine iliyoibuliwa na wabunge ni Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kutengewa fedha ndogo ikiwa ni pungufu kwa zile zinazopelekwa Wakala wa Barabara (Tanroads).

Katika hoja hiyo Kamati ya Bunge ya Miundombinu ilishauri Tarura kutengewa asilimia 40 na Tanroads asilimia 60 kutokana na barabara za vijijini kutopitika.

Kuhusu hoja hiyo, Profesa Mbarawa alisema mtandao wa barabara unaosimamiwa na Tanroads una urefu wa kilomita 36,257.97, kati ya kilomita hizo, 9,264.57 ni za lami.

No comments:

Post a Comment

Popular