Madaktari waelezea sababu zinazowafanya wanawake kuugua Magonjwa ya Akili kuliko Wanaume. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 22 April 2018

Madaktari waelezea sababu zinazowafanya wanawake kuugua Magonjwa ya Akili kuliko Wanaume.

 
Wakati tafiti zikionyesha kuwa wanawake huishi muda mrefu kuliko wanaume, imebainika kuwa wanawake huathirika zaidi na magonjwa ya akili aina ya sonona kuliko wanaume.

Wataalamu wa afya wamebaini kuwa wanawake huathiriwa zaidi na magonjwa ya akili ya kundi la sonona na kihoro kwa kuwa huumizwa zaidi na maisha ya ndoa na masuala ya uhusiano ukilinganisha na wanaume.

Mwananchi limefika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kufanya mazungumzo na mtaalamu wa Kitengo cha Afya ya Akili, Dkt Saidi Kuganda aliyesema ingawa hakuna takwimu rasmi za idadi ya jumla ya wanawake au wanaume wanaogua magonjwa ya akili, lakini sonona imebainika kuwaathiri zaidi wanawake.

Sonona ni aina ya ugonjwa wa akili unaotokana na kusononeka na kukata tamaa.

“Lakini kwa upande wa wanaume, wao hupata magonjwa ya akili kutokana na uraibu (addiction) ya dawa za kulevya, bangi au pombe,” alisema Dkt Kuganda

Alisema idadi kubwa ya wanawake waliolazwa katika hospitali hiyo ni wale walioachika au kuumizwa katika uhusiano wa mapenzi.

Dkt Kuganda alifafanua maana ya magonjwa ya akili na kusema, ni yale yanayoathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda katika utashi wake.

“Hivyo mgonjwa anakuwa na tabia au mwenendo ulio tofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila na desturi,” alisema mtalaamu huyo.

Pia aligusia utafiti uliofanyika mwaka 2017 katika hospitali hiyo ukiwahusisha wanawake waliopata kifafa cha mimba ulioonyesha kuwa asilimia 35 ya wanawake hao walikuwa na sonona.

Alisema 2016 walifanya tafiti katika Wilaya ya Temeke kwa wasichana wajawazito wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 19 na kuangalia magonjwa ya kihoro (anxiety) na sonona ambayo ni makundi ya magonjwa ya akili na kubaini kuwa asilimia 20 kati yao walikuwa na sonona na kihoro.

“Zaidi ya asilimia 20 ya wasichana waliofanyiwa utafiti, walikutwa na maradhi ya sonona na wasiwasi,” alisema Dkt Kuganda.

Kwa upande wake, mtaalamu wa afya, Dk Christopher Peterson alisema aliwahi kufanya utafiti na kubaini kuwa mwanamke mmoja kati ya watano ana maradhi ya akili aina ya sonona, huku mwanaume mmoja kati ya 10 ndiye huugua sonona maishani.

“Sonona kitaalamu hutambulika kama ‘depression’, huu ni ugonjwa wa akili ambao mtu anaupata baada ya kupitia matatizo fulani na kumuacha kwenye huzuni au kusononeka kwa muda mrefu,” alifafanua Dkt Peterson.

Mtaalamu wa masuala ya afya ya akili, Profesa John Adams wa Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza anasema wanawake ndiyo wanaosumbuliwa zaidi na maradhi ya sonona.

Anasema utafiti uliochapishwa katika jarida la Monitoring Psychology ambao alishiriki ulionyesha kuwa wanawake wanakabiliwa na matatizo ya akili kwa asilimia 40 zaidi ya wanaume.

“Uchunguzi wa maradhi ya akili unaofanywa kila mwaka nchini Uingereza ambapo majibu kila mwaka yanajirudia yanaonyesha wanawake wana matatizo ya saikolojia kwa asilimia 20 zaidi ya wanaume,” anasema.

Akichambua zaidi kuhusu sababu za wanawake kuathirika zaidi na sonona, mtaalamu wa afya ya akili, Dkt Cassian Nyandindi wa Hospitali ya Mwananyamala alisema wanawake husumbuliwa na sonona kutokana na aina ya maisha wanayoishi.

“Sonona huwasumbua zaidi wanawake kwa sababu ni walezi wa familia, aina ya shughuli zao, inapotokea ndoa kuvunjika wanawake hubeba mzigo mkubwa wa familia,” alisema.

Chanzo cha maradhi ya akili

Akizungumzia sababu za watu kuugua magonjwa ya akili, Dk Kuganda alisema zipo sababu za kibaolojia, maradhi ikiwamo Ukimwi, kifua kikuu na uraibu.

“Wengine tangu wamezaliwa vipashio vya mwili havijakaa sawa (neurotransimitters) ambavyo kazi yake ni kupasha habari, wakati mwingine vinakuwa na tatizo, hivyo vinamuweka mtu katika hatari ya kupata maradhi ya afya ya akili,” alisema.

Alisema maradhi kama Ukimwi, malaria na kifua kikuu huweza kumuathiri mtu kulingana na namna atakavyoyapokea na kukabiliana nayo.

“Maradhi yanasababisha msongo, kwa mfano mtu mwenye presha akifurahi inapanda, akichukia inapanda, asiposamehe inapanda, hivyo anakuwa kwenye hatari ya kupata maradhi ya afya ya akili,” alisema.

Alizungumzia pia sababu za kimazingira ikiwamo misiba au kuachana na mtu uliyempenda.

Dalili za ugonjwa wa akili

Dkt Kuganda amezitaja dalili kuu za maradhi ya afya ya akili akisema zinatofautishwa na mambo mawili.

Jambo la kwanza ni kufanya mambo yasiyo ya kawaida makubwa na yasiyo ya kawaida lakini madogo.

“Kwa mfano, mtu mzima anajisaidia hadharani, mwingine anacheka peke yake,” alisema.

Wapo wanaohisi kuwashwa, kutembewa na vitu ambavyo havipo au kuhisi anakimbizwa.

Alisema kuna watu wengine wakila chakula huhisi harufu tofauti na iliyopo, muda wote wakila wanatema.

No comments:

Post a Comment

Popular