Watu watumia simu ya mkuu wa Wilaya kufanyia utapeli. - KULUNZI FIKRA

Saturday 3 March 2018

Watu watumia simu ya mkuu wa Wilaya kufanyia utapeli.

 
Watu wanaosadikiwa kuwa matapeli wametumia simu ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo kutapeli zaidi ya Sh4 milioni.

Akizungumza na mwandishi wa habari jana, Regina alisema matapeli hao waliifunga namba yake ya Airtel (0784 2124xx) Februari 22 na kuisajili upya na kuanza kutapeli fedha kwa kutumia jina lake.

“Ilikuwa Alhamisi saa 11:55 jioni nilipokea ujumbe kwenye simu yangu ukinifahamisha kwamba simu yangu inafanyiwa usajili upya na baada ya ujumbe sikuweza tena kupokea wala kupiga simu,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Alisema alipoona hivyo alihisi kuna tatizo ndipo alipowasiliana na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) na kumfahamisha kilichotokea ili awafahamishe Airtel na kuchukua hatua zaidi.

Regina alisema baada ya kuwasiliana na OCD naye alifanya jitihada binafsi za kuwafahamisha Airtel ili kuifunga namba hiyo ya simu.

“Nasikitika Airtel hawakufanikiwa kufunga simu yangu kwa wakati hivyo hao watu wakaendelea kufanya utapeli kwa kuandika ujumbe kwa watu wa karibu yangu kuomba fedha hadi kesho yake (siku iliyofuata) saa nne nilipofika mwenyewe Airtel ndipo walipoifunga namba yangu,” alisema Regina.

Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema hawezi kutoa ufafanuzi kwa kuwa hana taarifa kuhusu jambo hilo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuna rafiki zake wawili walifika ofisini kwake wakitaka awalipe fedha walizotapeliwa kwa kutumia namba yake kwa kuwa wao walimkopesha yeye na hawakujua kama ni matapeli.

Alisema amejikuta katika migogoro ya hapa na pale na ndugu na marafiki kutokana na tukio hilo lakini amewataka wote kuripoti polisi ili waweze kusaidiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amethibitisha tukio hilo akisema polisi wameshawakamata watu watatu.

“Tumegundua huu ni mtandao wa wahalifu na hadi sasa tunawashikilia watu watatu, bado tunaendelea kuwatafuta wengine,” alisema.

Kamanda Matei alisema majina ya watuhumiwa yatatolewa watakapowakamata wote wanaotafutwa kwa kuwa kuyatoa sasa kunaweza kuharibu uchunguzi.

DC Regina amewashauri watumiaji wa simu kuwa makini na hasa wanapoombwa fedha kupitia mitandao akiwataka wajiridhishe kwanza ndipo watume.

No comments:

Post a Comment

Popular