Wachumi waelezea mbinu za Taifa kuondokana Utegemezi. - KULUNZI FIKRA

Friday 2 March 2018

Wachumi waelezea mbinu za Taifa kuondokana Utegemezi.

Wakati kiwango cha utegemezi kiumri kwa Watanzania ni asilimia 92, wataalamu wa uchumi wameshauri mbinu zinazoweza kutumika kuondokana na hali hiyo ili kufikia Tanzania ya uchumi wa viwanda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi jana, wachumi hao walisema ni hatari kwa Taifa lolote duniani kuwa na kiwango kikubwa cha utegemezi pamoja na kuwatumia wataalamu maeneo sahihi ya taaluma zao.

Juzi, taarifa ya makisio ya idadi ya watu nchini iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na kuzinduliwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ilieleza kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 54.2 milioni huku ongezeko kwa mwaka likiwa ni wastani wa watu 1.6 milioni.

Dkt  Mpango alisema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, kiwango cha utegemezi kinaonyesha kati ya Watanzania 100 wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanategemewa na watu 92 wenye umri wa chini ya miaka 15 na juu ya 65 ikilinganishwa na asilimia 40 ya nchi zinazoendelea.

Alisema kiwango kikubwa cha utegemezi kinachotokana na idadi kubwa ya watoto ni changamoto kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani, huku akieleza kwamba sera ya maendeleo ya watu hailazimishi kuzaa idadi fulani ya watoto isipokuwa inatahadharisha wazazi kupata watoto wanaoweza kumudu kuwalea.

Jana, walipotakiwa kuchambua utegemezi huo na maana yake kiuchumi, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salam (UDSM), Benedict Mongula alisema suala la utegemezi si geni hasa katika suala la idadi ya watu huku akieleza namna ya kulitatua.

“Tukuze uchumi wetu kwa kuongeza uwekezaji na uzalishaji ikiwamo kuongeza juhudi na maarifa, kuongeza tija ya uzalishaji katika eneo la kilimo ili kisaidie na tunapoingia katika uchumi wa viwanda tuingie kwa makini tusije kuingia na kurudi kama huko nyuma,” alisema Profesa Mongula na kuongeza:

“Tuongeze uwekezaji hasa wa Watanzania wenyewe na kutoka nje, viwanda vyetu tunavyoanzisha tuvitafutie soko la kutosha. Tuhakikishe kunakuwa na sera maalumu ya kuvisaidia viwanda kuendelea. Sera nzuri katika kilimo ili wakulima wadogo na wakubwa waweze kunufaika", alisema Profesa Mongula.

Profesa Mongula anaungwa mkono na Profesa mwingine wa uchumi wa chuo hicho, Haji Semboja aliyesema hakuna haja ya kulalamika na utegemezi kwani Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwamo ardhi, madini, bahari na nyinginezo ambazo zikitumika vizuri zitamaliza suala la ukosefu wa ajira.

Alisema kinachotakiwa kufanyika ni Bunge, Mahakama na Serikali kusimamia na kutekeleza sera na sheria zilizopo kwa ukamilifu na watendaji wanaosimamia taasisi mbalimbali kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Wakati mwingine mambo yanashindwa kutekelezwa na kubaki kurukaruka au kurukia rukia kutokana na aina ya watendaji tuliona nao, mfano mimi ni Profesa wa eneo fulani, lakini nakuwa nasimamia taasisi isiyoendana na taaluma yangu, ndiyo utakuta narukaruka au narukiarukia mara hili mara lile,” alisema Profesa Semboja na kuongeza:

“Tanzania haina tatizo sasa na kwamba ni maskini hapana, rasilimali tulizonazo na namna tunavyozitumia. Tatizo ni ku- transform (kubadilisha) tulichonacho. Kuna maeneo mengine hayaendi vizuri. Ukiona hayaendi ukifuatilia ni suala la utawala. Wanaopaswa kukaa pale utagundua si wa professional (wataalamu wa fani) yao na ingependeza kuona watu sahihi eneo fulani ili kuepuka kurukiarukia mambo.”

Mchumi kutoka Taasisi ya Tanzania Music (Tamufo), Dk Donald Kisanga alisema kiuhalisia baadhi ya mila na desturi zilizopo zinachangia kuwapo kwa kundi kubwa la utegemezi jambo linalohatarisha uchumi.

“Serikali inahitaji rasilimali watu iliyoelimika, hivyo lazima kuwekeza kwenye elimu,” alisema.

Pia, alishauri kuwapo kwa mfumo wa kuandaa mazingira mazuri ya watu kujiajiri badala ya kubweteka na kusubiria ajira rasmi zinazowafanya waendelee kuwa tegemezi wakati zinapokosekana

Mtaalamu wa uchumi kutoka Taasisi ya Nnyaka Production, Dkt Godwin Maimu alisema athari za utegemezi ni kubwa hasa wakati huu ambao Serikali ina mikakati ya kuingia kwenye uchumi wa viwanda.

“Utegemezi unaathiri mitaji, unahamisha fedha za uwekezaji kuwa za matumizi na hii ni hatari kubwa kiuchumi, wanaotegemewa hawataweza kuendelea kuzalisha kwa sababu kila kinachopatikana kinaingia kwenye matumizi,” alisema Dkt Msimu. 

Alisema hakuna taifa lolote linaloweza kuendelea duniani kama kundi la utegemezi ni kubwa kuliko la wanaotegemewa.

Ili kuondokana na dhana hiyo ya utegemezi, Dkt  Maimu alisema lazima Serikali ikubali kubadilisha mitalaa yake ya kufundishia na kuwekeza kwenye elimu ya vitendo badala ya nadharia inayotumika sasa.

Dkt Maimu alisema wanafunzi wanapomaliza masomo yao wanapaswa kuwa na ujuzi utakaowasaidia kujitegemea, kwa sababu wengi watakuwa wamefundishwa ili wanapohitimu waweze kujitegemea.

“Wanafunzi wasifundishwe kukariri, walau elimu nadharia iwe kwa asilimia 30 tu na vitendo iwe asilimia 70. Hii itasaidia kuondokana na utegemezi kwa sababu baada ya miaka kadhaa wanafunzi watakaokuwa wanahitimu watakuwa na ujuzi,” alisema Maimu.

Alisema hakuna taifa lolote linaloweza kujivunia kasi ya maendeleo kama watu wake wataendelea kuzaliana kupita kiasi.

Dkt Maimu alisema utegemezi unanyima wigo mpana wa uwekezaji kwa sababu wanaotegemewa kuwekeza hubaki kwenye hatua ya chini, hivyo kutoingia kwenye ushindani wa kiuchumi kwa kuwa mitaji yao haitaweza kukua.

Alisema ipo haja kwa jamii kuelimishwa namna ya kuwaandaa watoto wao kujitegemea hasa wanapofikia umri wa kutakiwa kufanya hivyo.

“Kuna wategemezi ambao umri wao sio wa kuwa tegemezi hawa lazima watengenezewe mazingira ya kutokuwa tegemezi, hata kwa kupelekwa kwenye vyuo vya ufundi ili mwisho wa siku, utegemezi huu uondoke,” alisema Dkt Maimu.

Katika ukurasa wetu wa facebook, baadhi ya wachangiaji wamezungumzia idadi hiyo ambapo Leung Ka Yan alisema “lugha rahisi asilimia 92 ya watanzania hawana uwezo wa kuishi kwa kujitegemea wenyewe.”

No comments:

Post a Comment

Popular