Baraza la Maaskofu Katoliki wazidi kushinikiza kuhusu katiba mpya. . - KULUNZI FIKRA

Saturday 3 March 2018

Baraza la Maaskofu Katoliki wazidi kushinikiza kuhusu katiba mpya. .

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limesema majadiliano ni msingi wa kudumisha amani, heshima na utu wa binadamu kabla na baada ya uchaguzi.

Pia limesema, kama wananchi wanapaza sauti kuhitaji mchakato wa Katiba ulioanza, Serikali haina budi kuuendeleza.

Hayo yamesemwa leo Machi 2, 2018 na Naibu Katibu Mkuu wa TEC, Padri Daniel Dule kwa niaba ya Katibu Mkuu wa baraza hilo, Padri Raymond Saba wakati akifungua kongamano la kujadili Katiba na ujenzi wa amani wakati wa uchaguzi, lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Padri Dulle amesema majadiliano yoyote yale yanahitaji kuwapo na kufanyika ili kudumisha amani, heshima na kujenga Taifa linaloheshimiana.

Amesema mchakato wa Katiba ulianza vizuri lakini mwisho wake haukuwa wenye umoja hivyo kusisitiza kuwapo kwa mazungumzo ili kupata Katiba iliyobeba mawazo ya wananchi.

"Majadiliano yanalenga kudumisha amani na kuheshimiana na si wachache wanajadiliana na wengine hawashirikishwi, hivyo hayaleti tija kwa jamii na Taifa," amesema Padri Dulle.

Amesema Taifa linapaswa kuwa na umoja na ushirikiano na kuheshimu utu wa binadamu hata kama anayezungumza mna tofauti lakini utu wake unapaswa kuheshimiwa.

"Makovu na chuki za kisiasa hasa baada ya uchaguzi hayapaswi kuwapo. Tujenge Taifa la kuaminiana na kuheshimiana na hili, litakuwapo kama kutakuwa na majadiliano," amesema Padri Dulle.

"Makovu haya ya wanasiasa yanaathiri jamii inayotuzunguka na ili kujenga Taifa lenye umoja mazungumzo kama haya ya leo yana tija kubwa."

Amesema kanisa kama wadau wa haki na amani walipata mwaliko wa kushiriki kongamano kwani wana mchango mkubwa katika hilo.

Kuhusu mchakato wa Katiba uliokwama, PadrI Dulle amesema; "Suala ni nia, Katiba si ya mtu mmoja, yawezekana kikundi kikubwa kinahitaji na kidogo hakitaki, kama wananchi wengi wanataka iwepo basi iendelezwe ili kutii kiu ya wananchi hao."

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema hitaji la kuandika Katiba mpya huanza baada ya Uchaguzi Mkuu kutokana na mambo mengi hutokea yanayohitaji kurekebishwa.

Amesema Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa 2005 na 2010 ulibaini changamoto kadhaa ambazo jawabu lake ni kuwapo kwa Katiba mpya inayojibu mahitaji.

"Tunakwenda katika Uchaguzi Mkuu 2020, tufanye kitu ili tuwe na uchaguzi wa amani na haki bila kumwaga damu au kusababisha uvunjifu wa amani," amesema Henga.

No comments:

Post a Comment

Popular