ACT-wazalendo wamemwandikia barua Waziri wa Ardhi. - KULUNZI FIKRA

Sunday, 18 March 2018

ACT-wazalendo wamemwandikia barua Waziri wa Ardhi.

 
Chama cha ACT-Wazalendo, kimesema kimemwandikia barua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuingilia kati ukiukwaji wa sheria unaofanywa na watendaji wa serikali wenye dhamana ya kutekeleza sheria ya ardhi na kutokufanyika kwa mpango bora wa matumizi ya ardhi za vijiji.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Leo Jumapili Machi 18 2018, kuhusu tathmini ya ziara yake katika kata zinazoongozwa na ACT-Wazalendo, Kiongozi wa chama hicho, Mhe  Zitto Kabwe amesema migogoro mingi ya ardhi husababishwa na wanaotajwa kama wawekezaji katika vijiji kugawiwa maeneo ya wananchi ya uzalishaji.

“Aidha uhifadhi umekuwa ukiingilia ardhi za vijiji na kuchukua maeneo makubwa ya vijiji katika baadhi ya vijiji na kusababisha adha kwa wananchi kunyang’anywa ardhi zao, mazao na mifugo huku wakipigwa kwa kisingizio cha kuvamia maeneo ya hifadhi na baadhi yao kutozwa faini kubwa", amesema Mhe Zitto kabwe.

“Mifano hai inapatikana katika kata za Mbwawa Kibaha, Tomondo jimbo la Morogoro Kusini, Kata ya Bugaga Kasulu, Msambara Kasulu na Kata ya Buhigwe jimbo la Buhigwe, Kutokana na hali hiyo, tumemwandikia Waziri Lukuvi aingilie suala hili”” amesema  Mhe Zitto kabwe.

Mhe Zitto  kabwe amesema licha ya juhudi za Waziri Lukuvi kushughulikia migogoro ya Ardhi, chama chake kinaamini kuwa Serikali kwa kiasi kikubwa inashirikiana na watu wenye fedha kupora ardhi za wananchi wanyonge.

“Serikali itazame upya namna ya kushughulika na migogoro ya ardhi na hasa kuwapa wananchi mashamba pori yote ambayo wawekezaji waliyapora kutoka kwa wananchi,” amesema Mhe Zitto kabwe.

No comments:

Post a Comment

Popular