Waziri mkuu atoa maagizo mazito kwa Takukuru. - KULUNZI FIKRA

Friday 16 February 2018

Waziri mkuu atoa maagizo mazito kwa Takukuru.

 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mwanza, mhandisi Ernest Makale kumkamata mkandarasi wa kampuni ya Palimon baada ya kushindwa kukamilisha mradi wa maji wa Sh2.06 bilioni.

Taarifa kutoka ofisi ya waziri mkuu imesema kuwa Majaliwa amechukua uamuzi huo leo Februari 16, 2018 wakati akizungumza na watumishi na wananchi kwenye kijiji cha Igumangobo wilayani Kwimba.

Inaeleza kuwa mkandarasi huyo alianza ujenzi wa mradi huo Oktoba 28, 2013 na alitakiwa kukamilisha Mei 28, 2014.

Majaliwa amesema kitendo cha mkandarasi kutokamilisha mradi huo kwa wakati licha ya kupewa fedha hakivumiliki, hivyo ameitaka TAKUKURU kutafuta popote alipo na kumhoji.

Ametoa agizo hilo baada ya wananchi wa vijiji vya Mhande, Shirima na Izizimba ‘B’ ambao mradi huo unatekelezwa katika vijiji vyao kumuomba waziri mkuu awasaidie ili mradi wao ukamilike na wao wapate huduma ya maji.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kwimba kutotumia fedha za miradi ya maendeleo kulipana posho.

“Fedha zinazopelekwa si za kulipana posho ni za maboresho na Serikali inataka wananchi wahudumiwe wasipate shida,” amesema.

Awali, Majaliwa alifungua mradi wa maji wa kijiji cha Igumangobo kilichopo Tarafa ya Mwamashimba wilayani Kwimba. Chanzo cha maji hayo ni Ziwa Victoria.

No comments:

Post a Comment

Popular