Radi yaua na kujerui watoto. - KULUNZI FIKRA

Wednesday 21 February 2018

Radi yaua na kujerui watoto.

Radi  ambayo haikuambatana na mvua wala upepo mkali imesababisha vifo na majeruhi katika kijiji cha Chingunduli, wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi.

Wakieleza tukio hilo kutoka katika kijiji hicho kwa sharti la kutotajwa majina yao kwenye habari hii, baadhi ya mashuhuda walisema radi hiyo ambayo haikuambatana na mvua wala upepo mkali ilisababisha vifo vya watoto wawili na kujeruhi wengine wawili kijijini hapo.

 "Hao watoto walikuwa wanacheza mpira karibu na nyumbani hapa, kulikuwa na dalili ya mvua. Hata hivyo haikunyesha , ila ghafla ilipiga radi iliyowajeruhi. Watoto hao walikuwa zaidi ya kuminatano, wote walianguka nakupoteza fahamu. Wengine walizunduka  lakini wanne hawakuzinduka ikalazimika wapelekwe hospitali, "alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Walisema baada ya kufikishwa hospitali ilibainika watoto wawili kati ya wanne   walikuwa wamefariki.

Mganga wa zamu wa hospitali ya wilaya ya Nachingwea aliyekutwa na Muungwana hosipitalini hapo, Dkt Jakson Swai, licha ya kutoingia kwa undani kueleza tukio hilo kwamadai kwamba sio msemaji, alikiri kuwa hosipitali hiyo ilipokea watu wanne ambao niwavulana waliojeruhiwa na radi.

Hata hivyo wawili kati yao wamefariki na miili yao ilikuwa imepelekwa katika kijiji cha Chingunduli ambako lilitokea tukio hilo.

"Nimeingia saa mbili hii(saa mbili ya usiku wa jana) nimekuta taarifa hiyo kwenye majalada. Wawili wanaendelea na matibabu, hata hivyo mmoja kati yao hali yake sio mzuri sana. Kwa maelezo ya kina mtafute kaimu mganga mkuu au mganga mfawidhi," alisema Dkt Swai.

 Juhudi za kuwapata mtendaji wa kijiji cha Chingunduli, kaimu mganga mkuu na mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Nachingwea hazikufanikiwa.

No comments:

Post a Comment

Popular