Mwalimu mkuu ampiga Kofi Mwalimu mwenzake. - KULUNZI FIKRA

Saturday 17 February 2018

Mwalimu mkuu ampiga Kofi Mwalimu mwenzake.

katika hali isiyo ya kawaida Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabwe  iliyoko mwambao mwa Ziwa Tanganyika, Nkasi mkoani Rukwa, Jackson Mussa, amemtandika kofi mwalimu mwenzake, Emmanuel Mbemba, mbele ya wanafunzi wake.

Akizungumzia tukio hilo, Mratibu Elimu Kata ya Kabwe, Geofrey Mtafya, alisema tukio la kupigwa kofi mwalimu huyo, lilitokea juzi asubuhi  majira ya saa 4:00 asubuhi  na kusababisha taharuki kubwa kwa wanafunzi na walimu wengine wa shule hiyo.

Mtafya alisema siku ya tukio hilo, Mwalimu Mbemba alikwenda ofisini kwa Mkuu wa shule kuomba  ruhusu ili awapeleke wanafunzi kwenye ziara ya mafunzo kwa kutembelea fukwe za Ziwa Tanganyika.

Mkuu huyo wa shule alimtaka mwalimu huyo aandike barua ya kiofisi na alifanya hivyo. Aliipokea barua hiyo na kumwahidi mwalimu huyo kuwa  baada ya muda si mrefu atampatia  majibu kwa maandishi.

alisema baada ya kusubiri kwa muda bila majibu,  Mwalimu Mbemba ambaye  anafundisha Kidato cha tatu  somo la Jiografia, alimfuata  mkuu wake  wa shule na kumkumbusha kuwa bado anasubiri. Mkuu wa shule alijibu kuwa  alikuwa bado hajaandika barua ya  ruhusa kwa kuwa alikuwa na majukumu mengine.

Baada ya muda mrefu tena kupita, mwalimu huyo wa Jiografia alimfuata Mkuu wa Shule ikiwa ni mara ya tatu  na kumweleza kuwa anachelewa kwenda kwenye ziara ya mafunzo na wanafunzi, kitendo kilichomkasirisha mkuu huyo wa shule, ndipo alipomfuata na  kumkaba  koo  Mwalimu Mbemba  mbele ya wanafunzi  na akaanza kumzaba  vibao mfululizo.

Taarifa kutoka shuleni hapo zinaeleza  kuwa  wanafunzi wa shule hiyo walishuhudia tukio hilo huku baadhi yao walianza kupiga kelele hatua iliyosababisha walimu wengine kwenda kuamua na kuwaachanisha walimu hao waliokuwa wamekwidana mashati.

Mwalimu  Mbemba alitoa taarifa kwa kiongozi wa Chama Cha Walimu (CWT) mahali pa Kazi, Elia Elia ambaye alimwarifu Ofisa Mtendaji Kata  ya Kabwe, Geoffrey Kuzumbi  ambaye aliitisha kikao cha dharura shuleni hapo.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho  zinaeleza kuwa Mkuu wa Shule huyo alikana kumpiga kofi mwalimu mwenzake bali alidai kuwa alimkaba koo tu.  Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Nkasi, Abel Ntupwa, alikiri  kutokea kwa tukio hilo na kukemea kitendo hicho kuwa ni utovu wa nidhamu  huku akiahidi kutolea  uamuzi wiki ijayo baada ya kupatiwa ripoti kamili.

No comments:

Post a Comment

Popular